Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

2 Samueli 22 - Swahili Revised Union Version


Wimbo wa Shukrani wa Daudi

1 Basi Daudi akamwambia BWANA maneno ya wimbo huu, siku ile BWANA alipomwokoa mikononi mwa adui zake wote, na mkononi mwa Sauli;

2 akasema, BWANA ndiye jabali langu, na ngome yangu, na mwokozi wangu,

3 Mungu wa mwamba wangu, nitamwamini yeye; Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, mnara wangu, na kimbilio langu; Mwokozi wangu, waniokoa na jeuri.

4 Nitamwita BWANA astahiliye kusifiwa; Hivyo nitaokoka na adui zangu.

5 Maana mawimbi ya mauti yalinizunguka, Mafuriko ya uovu yakanitia hofu.

6 Kamba za kuzimu zilinizunguka; Mitego ya mauti ikanikabili.

7 Katika shida yangu nilimwita BWANA, Naam, nikamlalamikia Mungu wangu; Naye akaisikia sauti yangu hekaluni mwake, Kilio changu kikaingia masikioni mwake.

8 Ndipo nchi ilipotikisika na kutetemeka, Misingi ya mbinguni ikasukasuka Na kutikisika, kwa sababu alikuwa na ghadhabu.

9 Kukapanda moshi kutoka puani mwake, Moto ukatoka kinywani mwake ukala; Makaa yakawashwa nao.

10 Aliziinamisha mbingu akashuka; Kukawa na giza kuu chini ya miguu yake.

11 Akapanda juu ya kerubi akaruka; Naam, alionekana juu ya mabawa ya upepo.

12 Akafanya giza hema zake za kumzunguka, Makusanyiko ya maji, mawingu makuu ya mbinguni.

13 Toka mwangaza uliokuwa mbele zake Makaa ya moto yakawashwa.

14 BWANA alipiga radi toka mbinguni, Naye Aliye Juu akaitoa sauti yake.

15 Akapiga mishale, akawatawanya; Umeme, naye akawatimua.

16 Ndipo ilipoonekana mikondo ya bahari, Misingi ya ulimwengu ikafichuliwa, Kwa kukemea kwake BWANA, Kwa mvumo wa pumzi ya puani mwake.

17 Alipeleka kutoka juu, akanishika; Akanitoa katika maji mengi;

18 Akaniokoa na adui yangu mwenye nguvu, Na wale walionichukia; Maana walikuwa na nguvu kuliko mimi.

19 Walinikabili siku ya msiba wangu; Lakini BWANA alikuwa tegemeo langu.

20 Akanitoa akanipeleka panapo nafasi; Aliniponya kwa kuwa alipendezwa nami.

21 BWANA alinitendea kulingana na haki yangu; Kulingana na usafi wa mikono yangu akanilipa.

22 Maana nimezishika njia za BWANA, Wala sikumwasi Mungu wangu.

23 Maana hukumu zake zote zilikuwa mbele yangu; Na kuhusu amri zake, sikuziacha.

24 Nami nilikuwa mkamilifu kwake, Nikajilinda na uovu wangu.

25 Basi BWANA amenilipa kulingana na haki yangu; Kulingana na usafi wa mikono yangu mbele zake.

26 Kwa mtu mwenye fadhili utakuwa mwenye fadhili Kwa mkamilifu utajionesha kuwa mkamilifu;

27 Kwake ajitakasaye utajionesha kuwa mtakatifu; Na kwa mpotovu utajionesha kuwa mkaidi.

28 Na watu wanaoonewa wewe utawaokoa; Ila macho yako huwapinga wenye kiburi, uwadhili.

29 Kwa kuwa wewe u taa yangu, Ee BWANA; Na BWANA ataniangazia giza langu.

30 Maana kwa msaada wako nafuatia jeshi; Kwa msaada wa Mungu wangu ninaruka ukuta.

31 Mungu njia yake ni kamilifu; Ahadi ya BWANA imehakikishwa; Yeye ndiye ngao yao Wote wanaomkimbilia.

32 Maana ni nani aliye Mungu, ila BWANA? Ni nani aliye mwamba, ila Mungu wetu?

33 Mungu ndiye ngome yangu yenye nguvu; Naye huwaongoza wakamilifu katika njia yake.

34 Huifanya miguu yangu kuwa kama ya kulungu; Na kunisimamisha mahali pangu pa juu.

35 Ananifundisha mikono yangu vita; Hata mikono yangu inaupanda upinde wa shaba.

36 Nawe umenipa ngao ya wokovu wako; Na unyenyekevu wako umenikuza.

37 Umezifanyia nafasi hatua zangu, Wala miguu yangu haikuteleza.

38 Nimewafuatia adui zangu, na kuwaangamiza; Wala sikurudi nyuma hadi walipokomeshwa.

39 Nami nimewakomesha na kuwapiga wasiweze kusimama; Naam, wameanguka chini ya miguu yangu.

40 Maana umenijaza nguvu ya kupigana vita; Ukawafanya adui zangu wafifie chini yangu.

41 Naam, adui zangu umewafanya wanipe visogo, Ili niwakatilie mbali wanaonichukia.

42 Walitazama, lakini hapakuwa na wa kuwaokoa; Walimwita BWANA, lakini hakuwajibu.

43 Ndipo nikawaponda kama mavumbi ya nchi, Nikawakanyaga kama matope ya njiani, nikawatawanya.

44 Nawe umeniokoa na mashindano ya watu wangu; Umenihifadhi niwe kichwa cha mataifa; Watu nisiowajua watanitumikia.

45 Wageni walinijia wakinyenyekea; Mara tu waliposikia habari zangu, Walinitii.

46 Wageni nao waliishiwa nguvu, Wakatoka katika ngome zao wakitetemeka.

47 BWANA yu hai; Na ahimidiwe mwamba wangu; Na atukuzwe Mungu wangu, mwamba wa wokovu wangu;

48 Naam, Mungu anilipiziaye kisasi, Na kuwatweza watu chini yangu,

49 Na kuniokoa kutoka kwa adui zangu; Naam, waniinua juu yao walioniinukia; Ukaniokoa kutoka kwa watu wajeuri.

50 Basi, BWANA, nitakushukuru kati ya mataifa, Nami nitaliimbia jina lako.

51 Yeye ni mnara wa wokovu kwa mfalme wake; Amfanyia fadhili masihi wake, Kwa Daudi na wazawa wake, hata milele.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo