Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Methali 11 - Swahili Revised Union Version

1 Mizani ya udanganyifu ni chukizo kwa BWANA; Bali vipimo vilivyo sawasawa humpendeza.

2 Kijapo kiburi ndipo ijapo aibu; Bali hekima hukaa na wanyenyekevu.

3 Ukamilifu wao wenye haki utawaongoza Bali ukaidi wao wenye fitina utawaangamiza.

4 Mali hazifaidii kitu siku ya ghadhabu; Bali haki huokoa na mauti.

5 Haki yake mtu mkamilifu itamwongoza njia yake; Bali mtu mwovu ataanguka kwa uovu wake.

6 Haki yao wenye haki itawaokoa; Bali wafanyao fitina watanaswa kwa hila yao wenyewe.

7 Mtu mwovu atakapokufa, taraja lake linapotea; Na matumaini ya uovu huangamia.

8 Mwenye haki huokolewa katika dhiki, Na mtu mwovu ataiingia badala yake.

9 Asiyemcha Mungu humpoteza jirani yake kwa kinywa chake; Bali wenye haki watapona kwa maarifa.

10 Wenye haki wasitawipo, mji hufurahi; Waovu wanapoangamia, watu hushangilia.

11 Mji hutukuzwa kwa mbaraka wa mwenye haki; Bali mji hupinduliwa kwa kinywa cha mwovu.

12 Asiye na akili humdharau mwenziwe; Bali mtu aliye na ufahamu hunyamaza.

13 Mwenye udaku hupitapita akifunua siri; Bali mwenye roho ya uaminifu husitiri mambo.

14 Pasipo mashauri taifa huanguka; Bali kwa wingi wa washauri huja wokovu.

15 Amdhaminiye mgeni hakosi ataumia; Achukiaye mambo ya dhamana yuko salama.

16 Mwanamke wa adabu huheshimiwa daima; Na watu wakali hushika mali siku zote.

17 Mwenye rehema huitendea mema nafsi yake; Aliye mkali hujisumbua mwili wake.

18 Mtu mwovu hupata mshahara wa udanganyifu; Apandaye haki ana thawabu ya hakika.

19 Haki huelekea uzima; Afuataye maovu hufuata mauti yake mwenyewe.

20 Wenye uhalifu moyoni ni chukizo kwa BWANA; Walio wakamilifu katika njia zao humpendeza.

21 Hakika, mtu mwovu hatakosa adhabu; Bali wazawa wa wenye haki wataokoka.

22 Kama pete ya dhahabu katika pua ya nguruwe, Ndivyo alivyo mwanamke mzuri asiye na akili.

23 Haja ya mwenye haki ni kupata mema tu; Bali kutaraji kwake mtu mwovu huishia katika ghadhabu.

24 Kuna atawanyaye, lakini huongezewa zaidi; Kuna azuiaye isivyo haki, lakini huelekea uhitaji.

25 Nafsi ya mtu mkarimu itastawishwa; Anyweshaye atanyweshwa mwenyewe.

26 Awanyimaye watu nafaka, watu watamlaani; Auzaye nafaka, baraka itakuwa kichwani pake.

27 Atafutaye mema kwa bidii hutafuta fadhili; Atafutaye madhara, hayo yatamjia.

28 Azitegemeaye mali zake ataanguka; Mwenye haki atasitawi kama jani.

29 Ataabishaye nyumba yake mwenyewe ataurithi upepo; Mpumbavu atakuwa mtumwa wa mtu mwenye moyo wa akili.

30 Mazao ya mwenye haki ni mti wa uzima; Na mwenye hekima huvuta roho za watu.

31 Ikiwa, mwenye haki atalipwa duniani; Je, mwovu na mkosaji hawatalipwa mara nyingi zaidi?

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo