Mathayo 27 - Swahili Revised Union VersionYesu aletwa mbele ya Pilato 1 Na ilipokuwa asubuhi, wakuu wa makuhani wote na wazee wa watu wakafanya shauri juu ya Yesu, wapate kumwua; 2 wakamfunga, wakamchukua, wakampeleka kwa Pilato aliyekuwa mtawala. Yuda ajinyonga 3 Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, alipoona ya kuwa amekwisha kuhukumiwa, alijuta, akawarudishia wakuu wa makuhani na wazee vile vipande thelathini vya fedha, akasema, Nilikosa nilipoisaliti damu isiyo na hatia. 4 Wakasema, Basi, haya yatuhusu nini sisi? Yaangalie haya wewe mwenyewe. 5 Akavitupa vile vipande vya fedha katika hekalu, akaondoka; akaenda, akajinyonga. 6 Wakuu wa makuhani wakavitwaa vile vipande vya fedha, wakasema, Si halali kuviweka katika sanduku ya sadaka, kwa kuwa ni fedha ya damu. 7 Wakafanya shauri, wakavitumia kwa kununua shamba la mfinyanzi liwe mahali pa kuzika wageni. 8 Kwa hiyo shamba lile huitwa shamba la damu hata leo. 9 Ndipo likatimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, akisema, Wakavitwaa vipande thelathini vya fedha, kima chake aliyetiwa kima, ambaye baadhi ya Waisraeli walimtia kima; 10 wakavitumia kwa kununua shamba la mfinyanzi, kama Bwana alivyoniagiza. Pilato amhoji Yesu 11 Naye Yesu akasimama mbele ya mtawala; mtawala akamwuliza, akasema, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Yesu akamwambia, Wewe wasema. 12 Lakini aliposhitakiwa na wakuu wa makuhani na wazee, hakujibu hata neno. 13 Ndipo Pilato akamwambia, Husikii ni mambo mangapi wanayoshuhudia juu yako? 14 Asimjibu hata neno moja, hata mtawala akastaajabu sana. 15 Basi wakati wa sikukuu, mtawala desturi yake huwafungulia mkutano mfungwa mmoja waliyemtaka. 16 Basi palikuwa na mfungwa mashuhuri siku zile, aitwaye Baraba. 17 Basi walipokutanika, Pilato akawaambia, Mnataka niwafungulie yupi? Yule Baraba, au Yesu aitwaye Kristo? 18 Kwa maana alijua ya kuwa wamemtoa kwa ajili ya husuda. 19 Na alipokuwa ameketi juu ya kiti cha hukumu, mkewe alimpelekea mjumbe, kumwambia, Usiwe na neno na yule mwenye haki; kwa sababu nimeteswa mengi leo katika ndoto kwa ajili yake. 20 Nao wakuu wa makuhani na wazee wakawashawishi makutano ili wamtake Baraba, na kumwangamiza Yesu. 21 Basi mtawala akajibu, akawaambia, Mnataka niwafungulie yupi kati ya hawa wawili? Wakasema, Baraba. 22 Pilato akawaambia, Basi, nimtendeje Yesu aitwaye Kristo? Wakasema wote, Asulubiwe. 23 Akasema, Kwa nini? Ni ubaya gani alioutenda? Wakazidi sana kupiga kelele, wakisema, Na asulubiwe. Pilato amtoa Yesu asulubiwe 24 Basi Pilato alipoona ya kuwa hafai lolote, bali ghasia inazidi tu, akatwaa maji, akanawa mikono yake mbele ya mkutano, akasema, Mimi sina hatia katika damu ya mtu huyu mwenye haki; yaangalieni haya ninyi wenyewe. 25 Watu wote wakajibu wakasema, Damu yake na iwe juu yetu, na juu ya watoto wetu. 26 Ndipo akawafungulia Baraba; na baada ya kumpiga Yesu mijeledi, akamtoa ili asulubiwe. Askari wamdhihaki Yesu 27 Ndipo askari wa mtawala wakamchukua Yesu ndani ya Praitorio, wakamkusanyikia kikosi kizima. 28 Wakamvua nguo, wakamvika vazi jekundu. 29 Wakasokota taji la miiba, wakaliweka juu ya kichwa chake, na mwanzi katika mkono wake wa kulia; wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki, wakisema, Salamu, Mfalme wa Wayahudi! 30 Kisha wakamtemea mate, wakautwaa ule mwanzi, wakampigapiga kichwani. 31 Walipokwisha kumdhihaki, wakalivua lile vazi, wakamvika mavazi yake, wakamchukua kumsulubisha. Yesu asulubiwa 32 Walipokuwa wakitoka, wakamwona mtu Mkirene, jina lake Simoni; huyu wakamshurutisha auchukue msalaba wake. 33 Na walipofika mahali paitwapo Golgotha, yaani, Fuvu la Kichwa, 34 wakampa kunywa divai iliyochanganyika na nyongo; lakini yeye alipoionja hakutaka kunywa. 35 Walipokwisha kumsulubisha, waligawana mavazi yake, kwa kupiga kura; [ili litimie neno lililonenwa na nabii, Waligawa nguo zangu kati yao, na juu ya vazi langu walipiga kura.] 36 Wakaketi, wakamlinda huko. 37 Wakaweka juu ya kichwa chake mashitaka yake, yaliyoandikwa HUYU NI YESU, MFALME WA WAYAHUDI. 38 Wakati uo huo wanyang'anyi wawili wakasulubiwa pamoja naye, mmoja katika mkono wake wa kulia, na mmoja katika mkono wake wa kushoto. 39 Nao waliokuwa wakipita njiani wakamtukana, wakitikisatikisa vichwa vyao, wakisema, 40 Ewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe nafsi yako; ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, shuka msalabani. 41 Kadhalika na wale wakuu wa makuhani wakamdhihaki pamoja na waandishi na wazee, wakisema, Aliokoa wengine, hawezi kujiokoa mwenyewe. 42 Yeye ni mfalme wa Israeli; na ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini. 43 Amemtegemea Mungu; na amwokoe sasa, kama anamtaka; kwa maana alisema, Mimi ni Mwana wa Mungu. 44 Pia wale wanyang'anyi waliosulubiwa pamoja naye walimshutumu vile vile. Kifo cha Yesu 45 Basi tangu saa sita palikuwa na giza juu ya nchi yote hadi saa tisa. 46 Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? 47 Na baadhi yao waliokuweko, waliposikia, walisema, Huyu anamwita Eliya. 48 Mara mmoja wao akaenda mbio, akatwaa sifongo, akaijaza siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha. 49 Wale wengine wakasema, Acha; na tuone kama Eliya anakuja kumwokoa. 50 Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake. 51 Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hadi chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; 52 makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala; 53 nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi. 54 Basi yule afisa, na hao waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu, walipoliona tetemeko la ardhi na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu. 55 Palikuwa na wanawake wengi pale wakitazama kwa mbali, hao ndio waliomfuata Yesu toka Galilaya, na kumtumikia. 56 Miongoni mwao alikuwamo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo na Yusufu, na mama yao wana wa Zebedayo. Kuzikwa kwa Yesu 57 Na ilipokuwa jioni akafika mtu tajiri wa Arimathaya, jina lake Yusufu, naye mwenyewe alikuwa mwanafunzi wa Yesu; 58 mtu huyu alimwendea Pilato akaomba apewe mwili wa Yesu. Ndipo Pilato akaamuru apewe. 59 Yusufu akautwaa mwili, akauzongazonga katika sanda ya kitani safi, 60 akauweka katika kaburi lake jipya, alilokuwa amelichonga mwambani; akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango wa kaburi, akaenda zake. 61 Na pale walikuwapo Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, wameketi kulielekea kaburi. Ulinzi katika kaburi 62 Hata siku ya pili, ndiyo iliyo baada ya Maandalio, wakuu wa makuhani, na Mafarisayo wakamkusanyikia Pilato, 63 wakasema, Bwana, tumekumbuka kwamba yule mjanja alisema, alipokuwa angali hai, Baada ya siku tatu nitafufuka. 64 Basi amuru kwamba kaburi lilindwe salama hadi siku ya tatu; wasije wanafunzi wake wakamwiba, na kuwaambia watu, Amefufuka katika wafu; na udanganyifu wa mwisho utapita ule wa kwanza. 65 Pilato akawaambia, Mna askari; nendeni mkalilinde salama kadiri mjuavyo. 66 Wakaenda, wakalilinda kaburi salama, kwa kulitia lile jiwe mhuri, pamoja na kuwaweka wale askari walinzi. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya