Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Mwanzo 24 - Swahili Revised Union Version


Ndoa ya Isaka na Rebeka

1 Basi Abrahamu alikuwa mzee mwenye miaka mingi, na BWANA alikuwa amembariki Abrahamu katika vitu vyote.

2 Abrahamu akamwambia mtumishi wake, mzee wa nyumba yake, aliyetawala vitu vyake vyote, Tafadhali uutie mkono wako chini ya paja langu,

3 nami nitakuapisha kwa BWANA, Mungu wa mbingu, na Mungu wa nchi, kwamba hutamtwalia mwanangu mke katika binti za Wakanaani ambao nakaa kati yao;

4 bali nenda hata nchi yangu, na kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu Isaka mke.

5 Yule mtumishi akamwambia, Labda yule mwanamke hatakubali kufuatana nami mpaka nchi hii, je! Nimrudishe mwanao mpaka nchi ulikotoka?

6 Abrahamu akamwambia, Ujihadhari, usimrudishe mwanangu huko.

7 BWANA, Mungu wa mbingu, aliyenitoa katika nyumba ya babangu, na kusema nami katika nchi niliyozaliwa, aliniapia akisema, Nitawapa uzao wako nchi hii; yeye atamtuma malaika wake mbele yako, nawe utamtwalia mwanangu mke kutoka huko;

8 na yule mwanamke asipokubali kufuatana nawe, basi, utafunguliwa kiapo changu hiki; lakini usimrudishe mwanangu huko.

9 Yule mtumishi akaweka mkono wake chini ya paja la Abrahamu bwana wake, akamwapia katika neno hilo.

10 Kisha huyo mtumishi akatwaa ngamia kumi katika ngamia za bwana wake akaenda zake, maana mali zote za bwana wake zilikuwa mkononi mwake, akaondoka, akaja mpaka Mesopotamia, mpaka mji wa Nahori.

11 Akawapigisha magoti ngamia nje ya mji karibu na kisima cha maji wakati wa jioni, wakati ambapo wanawake wanakwenda kuteka maji.

12 Naye akasema, Ee BWANA, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, nakuomba mambo yangu uyajalie yawe heri leo, ukamfadhili bwana wangu Abrahamu.

13 Tazama! Nimesimama karibu na kisima cha maji, na binti za watu wa mjini wanatoka kuteka maji,

14 basi na iwe hivi; yule msichana nitakayemwambia, Tua mtungi wako, nakuomba, ninywe; naye akasema, Unywe, nami nitawanywesha na ngamia zako pia; basi huyu na awe ndiye uliyemchagulia mtumishi wako Isaka; na kwa hayo nitajua ya kuwa umemfadhili bwana wangu.

15 Ikawa, kabla hajaisha kunena, tazama, Rebeka anatokea, binti wa Bethueli mwana wa Milka, mkewe Nahori, ndugu wa Abrahamu, naye ana mtungi begani pake.

16 Naye yule msichana alikuwa mzuri sana uso wake, bikira, wala mwanamume hajamjua bado; akashuka kisimani, akajaza mtungi wake, akapanda.

17 Ndipo yule mtumishi akapiga mbio kwenda kumlaki, akasema, Tafadhali unipe maji kidogo katika mtungi wako ninywe.

18 Naye akasema, Unywe, bwana wangu, akafanya haraka, akatua mtungi wake mkononi mwake, akamnywesha.

19 Hata alipokwisha kumnywesha akasema, Na ngamia wako nitawatekea, hadi watakapokwisha kunywa.

20 Akafanya haraka, akamwaga maji ya mtungi wake katika birika, akapiga mbio kisimani ateke, akawatekea ngamia wake wote.

21 Basi yule mtu akamkazia macho, akanyamaza, ili ajue kama BWANA ameifanikisha safari yake ama sivyo.

22 Ikawa, ngamia walipokwisha kunywa, yule mtu akatwaa pete ya dhahabu, uzani wake ulikuwa nusu shekeli, na vikuku viwili kwa mikono yake, uzani wake ulikuwa shekeli kumi za dhahabu,

23 akasema, U binti wa nani wewe? Tafadhali uniambie. Je! Iko nafasi katika nyumba ya baba yako tupate mahali pa kukaa kwa muda?

24 Akasema, Mimi ni binti wa Bethueli mwana wa Milka, aliyemzalia Nahori.

25 Tena akamwambia, Kwetu kuna majani na malisho ya kutosha, na mahali pa kukaa wageni.

26 Yule mtu akainama akamsujudu BWANA.

27 Akasema, Na atukuzwe BWANA, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, ambaye hakuacha rehema zake na kweli yake kwa bwana wangu. BWANA akaniongoza mimi nami njiani hata nyumba ya nduguze bwana wangu.

28 Basi yule msichana akapiga mbio, akawaambia watu wa nyumba ya mama yake mambo hayo.

29 Na Rebeka alikuwa na kaka, jina lake Labani. Labani akatoka mbio kumwendea yule mtu kisimani.

30 Ikawa, alipoiona ile pete, na vikuku mikononi mwa dada yake, akasikia maneno ya Rebeka dada yake, akisema, Hivyo ndivyo alivyoniambia mtu huyo, basi akamjia mtu yule, na tazama, amesimama karibu na ngamia kisimani.

31 Akasema, Karibu, wewe uliyebarikiwa na BWANA, mbona unasimama nje? Kwa maana nimeiweka nyumba tayari, na nafasi kwa ngamia.

32 Na mtu yule akaingia katika nyumba, akawafungua ngamia; naye akatoa majani na malisho kwa ngamia, na maji ya kuoshea miguu yake, na miguu ya watu waliokuwa pamoja naye.

33 Akaandaliwa chakula, lakini akasema, Sili mpaka niseme kwanza maneno yangu. Akamwambia, Haya, sema.

34 Akasema, Mimi ni mtumwa wa Abrahamu,

35 na BWANA amembarikia sana bwana wangu, amekuwa mtu mkuu; amempa kondoo, na ng'ombe, na fedha, na dhahabu, na watumishi, na wajakazi, na ngamia, na punda.

36 Naye Sara, mkewe bwana wangu, akamzalia bwana wangu mwana wa kiume, katika uzee wake; naye amempa yote aliyo nayo.

37 Kisha bwana wangu akaniapisha akisema, Usimtwalie mwanangu mke wa binti za Wakanaani, ambao nakaa katika nchi yao.

38 Ila uende mpaka nyumbani kwa babangu, na kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu mke.

39 Nikamwambia bwana wangu, Labda huyo mwanamke hatafuatana nami.

40 Akaniambia, BWANA, ambaye naenenda machoni pake, atatuma malaika wake pamoja nawe, atafanikisha njia yako; nawe umtwalie mwanangu mke katika jamaa zangu, na wa nyumba ya babangu.

41 Ndipo utafunguliwa kiapo changu hapo utakapowafikia jamaa zangu; hata wasipokupa msichana huyo, utafunguliwa kiapo changu.

42 Nami nikaja leo kisimani, nikasema, Ee BWANA, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, ukinifanikishia sasa njia yangu niendayo mimi,

43 tazama! Nimesimama karibu na kisima cha maji; basi na iwe hivi, msichana ajaye kuteka maji, nikamwambia, Nipe, nakuomba, maji kidogo katika mtungi wako ninywe,

44 naye akaniambia, Unywe wewe, na ngamia wako pia nitawatekea, huyo na awe ndiye mke BWANA aliyemwekea mwana wa bwana wangu.

45 Hata kabla sijaisha kusema moyoni mwangu, tazama! Rebeka akatokea, na mtungi begani mwake. Akashuka kisimani akateka. Nami nikamwambia, Tafadhali nipe maji ninywe.

46 Akafanya haraka akatua mtungi wake chini, akasema, Unywe, na ngamia wako nitawanywesha pia; basi nikanywa, akawanywesha na ngamia nao.

47 Kisha nikamwuliza, U binti wa nani wewe? Naye akasema, Mimi ni binti Bethueli, mwana wa Nahori, Milka aliyemzalia. Nami nikamtia kishaufu puani mwake na vikuku mikononi mwake.

48 Nikainama, nikamsujudia BWANA, nikamtukuza BWANA, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, aliyeniongoza njiani, nimtwalie mwana wa bwana wangu binti wa ndugu yake.

49 Basi, kama mnataka kumfanyia rehema na kweli bwana wangu, niambieni kama sivyo, niambieni; ili nigeuke upande wa kulia au wa kushoto.

50 Ndipo Labani na Bethueli wakajibu wakasema, Neno hili limetoka kwa BWANA, wala sisi hatuwezi kukuambia neno jema wala baya.

51 Tazama, huyo Rebeka yuko mbele yako, umchukue, ukaende zako awe mke wa mwana wa bwana wako, kama alivyosema BWANA.

52 Ikawa mtumishi wa Abrahamu aliposikia maneno yao, akainama hata nchi mbele za BWANA.

53 Kisha huyo mtumishi akatoa vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na mavazi, akampa Rebeka; na vitu vya thamani akampa nduguye na mamaye pia.

54 Wakala, wakanywa, yeye na watu waliokuwa pamoja naye, nao wakakaa usiku. Wakaondoka asubuhi, naye akasema, Nipeni ruhusa niende kwa bwana wangu.

55 Kaka yake na mama yake wakasema, Msichana na akae kwetu kama siku kumi, zisipungue, baadaye aende.

56 Naye akawaambia, Msinikawilishe, mradi BWANA amefanikisha njia yangu; nipeni ruhusa niende kwa bwana wangu.

57 Wakasema, Na tumwite huyo msichana, tumwulize mwenyewe.

58 Wakamwita Rebeka wakamwuliza, Je! Utakwenda na mtu huyu? Akasema, Nitakwenda.

59 Ndipo wakampeleka Rebeka dada yao, na yaya wake, na mtumishi wa Abrahamu, na watu wake.

60 Wakambariki Rebeka, wakamwambia, Dada yetu, wewe uwe mama wa elfu kumi, mara elfu nyingi, na wazao wako waurithi mlango wa hao wawachukiao.

61 Rebeka akaondoka na vijakazi wake, nao wakapanda juu ya ngamia, wakamfuata yule mtu. Naye huyo mtumishi akamchukua Rebeka akaenda zake.

62 Basi Isaka alikuwa amekuja kwa njia ya Beer-lahai-roi, maana alikaa katika nchi ya kusini.

63 Isaka akatoka ili kutafakari shambani wakati wa jioni; akainua macho yake, akaona, kuna ngamia wanakuja.

64 Rebeka akainua macho, naye alipomwona Isaka, alishuka juu ya ngamia.

65 Akamwambia mtumishi, Ni nani mtu huyu ajaye shambani kutulaki? Mtumishi akasema, Huyu ndiye bwana wangu. Basi akatwaa shela yake akajifunika.

66 Yule mtumishi akamwambia Isaka mambo yote aliyoyatenda.

67 Isaka akamwingiza Rebeka katika hema ya mama yake, Sara, akamtwaa Rebeka, akawa mkewe, akampenda; Isaka akafarijika kwa ajili ya kufa kwa mama yake.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo