Methali 15 - Swahili Revised Union Version1 Jawabu la upole hugeuza hasira; Bali neno liumizalo huchochea ghadhabu. 2 Ulimi wa mwenye hekima hutamka maarifa vizuri; Bali vinywa vya wapumbavu humwaga upumbavu. 3 Macho ya BWANA yako kila mahali; Yakimchunguza mbaya na mwema. 4 Ulimi safi ni mti wa uzima; Bali ukorofi wa ulimi huvunja moyo. 5 Mpumbavu hudharau kurudiwa na babaye; Bali yeye aangaliaye maonyo hupata busara. 6 Katika nyumba ya mwenye haki mna akiba nyingi; Bali mapato ya mtu mbaya huwa taabu tu. 7 Midomo ya mwenye haki hueneza maarifa; Bali moyo wa mpumbavu haufanyi hivyo. 8 Sadaka ya mtu mbaya ni chukizo kwa BWANA; Bali maombi ya mtu mnyofu ni furaha yake. 9 Njia ya mtu mbaya ni chukizo kwa BWANA; Bali humpenda mtu afuatiaye wema. 10 Adhabu kali ina yeye aiachaye njia; Naye achukiaye kukemewa atakufa. 11 Kuzimu na Uharibifu viko wazi mbele za BWANA; Si zaidi basi, mioyo ya wanadamu? 12 Mwenye mzaha hapendi kukaripiwa; Wala yeye hawaendei wenye hekima. 13 Moyo wa furaha huchangamsha uso; Bali kwa huzuni ya moyo roho hupondeka. 14 Moyo wa mwenye ufahamu hutafuta maarifa; Bali kinywa cha wapumbavu hula upumbavu. 15 Siku zote za mtu ateswaye ni mbaya; Bali ukunjufu wa moyo ni karamu ya daima. 16 Kuwa na mali chache pamoja na kumcha BWANA; Ni bora kuliko mali nyingi pamoja na taabu. 17 Chakula cha mboga palipo na upendo; Ni bora kuliko ng'ombe aliyenona pamoja na kuchukiana. 18 Mtu wa hasira huchochea ugomvi; Bali asiye mwepesi wa hasira hutuliza mashindano. 19 Njia ya mtu mvivu ni kama boma la miiba; Bali mapito yao wenye unyofu hufanyika njia kuu. 20 Mwana mwenye hekima humfurahisha babaye; Bali mpumbavu humdharau mamaye. 21 Upumbavu ni furaha kwake aliyepungukiwa na akili; Bali mwenye ufahamu huunyosha mwenendo wake. 22 Pasipo ushauri mipango vuhunjika; Bali kwa wingi wa washauri huthibitika. 23 Mtu hulifurahia jibu la kinywa chake; Na neno linenwalo wakati wa kufaa ni jema kama nini! 24 Kwa mtu mwenye akili njia ya uhai huenda juu; Ili atoke katika kuzimu chini. 25 BWANA ataing'oa nyumba ya mwenye kiburi; Bali atauthibitisha mpaka wa mjane. 26 Ushauri mbaya ni chukizo kwa BWANA; Bali maneno yapendezayo ni safi. 27 Atamaniye faida huifadhaisha nyumba yake mwenyewe; Bali achukiaye zawadi ataishi. 28 Moyo wa mwenye haki hufikiri jinsi atakavyojibu; Bali kinywa cha wasio haki humwaga mabaya. 29 BWANA yuko mbali na wasio haki; Bali huisikia sala ya mwenye haki. 30 Mng'ao wa macho huufurahisha moyo; Habari njema huinenepesha mifupa. 31 Sikio lisikilizalo lawama yenye uhai Litakaa kati yao wenye hekima. 32 Akataaye maonyo huidharau nafsi yake mwenyewe; Bali yeye asikilizaye lawama hujipatia ufahamu. 33 Kumcha BWANA ni maonyo ya hekima; Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya