Methali 10 - Swahili Revised Union VersionKITABU CHA PILI Mithali za Sulemani 1 Mwana mwenye hekima humfurahisha babaye; Bali mwana mpumbavu ni mzigo wa mamaye. 2 Hazina za uovu hazifaidii kitu; Bali haki huokoa na mauti. 3 BWANA hataiacha nafsi ya mwenye haki ife na njaa; Bali tamaa ya mtu mwovu huisukumia mbali. 4 Atendaye mambo kwa mkono mlegevu huwa maskini; Bali mkono wake aliye na bidii hutajirisha. 5 Akusanyaye wakati wa joto ni mwana mwenye hekima; Bali asinziaye wakati wa mavuno ni mwana mwenye kuaibisha. 6 Baraka humkalia mwenye haki kichwani; Bali jeuri hufunika kinywa chake mtu mwovu. 7 Kuwakumbuka wenye haki huwa na baraka; Bali jina la mtu mwovu litaoza. 8 Aliye na akili moyoni mwake atapokea agizo; Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka. 9 Aendaye kwa unyofu huenda salama; Bali apotoshaye njia zake atajulikana. 10 Akonyezaye kwa jicho huleta masikitiko; Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka. 11 Kinywa chake mwenye haki ni chemchemi ya uzima; Bali jeuri hufunika kinywa chake mtu mwovu, 12 Kuchukiana huleta fitina; Bali kupendana husitiri makosa yote. 13 Hekima hupatikana midomoni mwa mwenye ufahamu; Bali fimbo hufaa kwa mgongo wake asiye na ufahamu. 14 Watu wenye akili huweka akiba ya maarifa; Bali kinywa cha mpumbavu ni uangamivu ulio karibu. 15 Mali ya tajiri ndio ngome yake; Ufukara wa maskini ndio umwangamizao. 16 Kazi yake mwenye haki huuelekea uzima; Mazao ya wabaya huielekea dhambi. 17 Akubaliye kurudiwa huwa katika njia ya uzima; Bali yeye aachaye maonyo hukosa. 18 Yeye afichaye chuki ana midomo ya uongo, Na yeye asingiziaye ni mpumbavu. 19 Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu; Bali yeye azuiaye midomo yake hufanya akili. 20 Ulimi wa mwenye haki ni kama fedha safi; Moyo wa mtu mbaya haufai kitu. 21 Midomo ya mwenye haki hulisha watu wengi; Bali wapumbavu hufa kwa kuwa hawana ufahamu. 22 Baraka ya BWANA hutajirisha, Wala hachanganyi huzuni nayo. 23 Kwa mpumbavu kutenda maovu ni kama mchezo; Bali mtu mwenye ufahamu ana hekima. 24 Aogopacho mtu asiye haki ndicho kitakachomjilia; Na wenye haki watapewa matakwa yao. 25 Kisulisuli kikiisha pita asiye haki hayuko tena; Bali mwenye haki ni msingi wa milele. 26 Kama siki menoni, na kama moshi machoni, Ndivyo alivyo mtu mvivu kwa hao waliomwajiri. 27 Kumcha BWANA kwaongeza siku za mtu; Bali miaka yao wasio haki itapunguzwa. 28 Matumaini yao wenye haki yatakuwa furaha; Bali matarajio yao wasio haki yatapotea. 29 Njia ya BWANA ni kimbilio lake mtu mkamilifu; Bali ni uharibifu kwao watendao maovu. 30 Mwenye haki hataondolewa milele; Bali wasio haki hawatakaa katika nchi. 31 Kinywa cha mwenye haki hutoa hekima; Bali ulimi wa ukaidi utakatiliwa mbali. 32 Midomo ya mwenye haki huyajua yatakayokubaliwa; Bali kinywa chao wasio haki hunena ukaidi. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya