Luka 22 - Swahili Revised Union VersionMpango wa kumwua Yesu 1 Ikakaribia sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, iitwayo sikukuu ya Pasaka. 2 Na wakuu wa makuhani na waandishi walikuwa wakitafuta njia ya kumwua; maana walikuwa wakiwaogopa watu. 3 Shetani akamwingia Yuda, aitwaye Iskarioti, naye ni mmoja wa wale Kumi na Wawili. 4 Akaondoka, akaenda akasema na wakuu wa makuhani na majemadari, jinsi atakavyoweza kumtia mikononi mwao. 5 Wakafurahi, wakapatana naye kumpa fedha. 6 Akakubali, akatafuta nafasi ya kumsaliti kwao pasipokuwapo mkutano. Maandalizi ya Pasaka 7 Ikafika siku ya mikate isiyotiwa chachu, ambayo ilipasa kuchinja Pasaka. 8 Akawatuma Petro na Yohana, akisema, Nendeni, mkatuandalie Pasaka tupate kuila. 9 Wakamwambia, Wataka tuandae wapi? 10 Akawaambia, Tazama, mtakapoingia mjini mtakutana na mwanamume akiwa amebeba mtungi wa maji; mfuateni mkaingie katika nyumba atakayoingia yeye. 11 Na mtamwambia mwenye nyumba, Mwalimu akuambia, Kiko wapi chumba cha wageni, nipate kula Pasaka humo pamoja na wanafunzi wangu? 12 Naye atawaonesha chumba kikubwa ghorofani, kimekwisha tayarishwa; andaeni humo. 13 Wakaenda, wakaona kama alivyowaambia, wakaiandaa Pasaka. Kuanzishwa kwa chakula cha Bwana 14 Na saa ilipofika aliketi chakulani, yeye na wale mitume pamoja naye. 15 Akawaambia, Nimetamani sana kuila Pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu; 16 kwa maana nawaambia ya kwamba siili tena hadi itakapotimizwa katika ufalme wa Mungu. 17 Akapokea kikombe, akashukuru, akasema, Twaeni hiki, mgawanye ninyi kwa ninyi; 18 Maana nawaambia ya kwamba tangu sasa sinywi mazao ya mzabibu hadi ufalme wa Mungu utakapokuja. 19 Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, [Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. 20 Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.] 21 Lakini, tazama, mkono wake yeye anayenisaliti upo hapa pamoja nami mezani, 22 Kwa kuwa Mwana wa Adamu aenda zake kama ilivyokusudiwa; lakini, ole wake mtu yule amsalitiye! 23 Wakaanza kuulizana wao kwa wao, ni yupi miongoni mwao atakayelitenda jambo hilo. Mashindano kuhusu ukubwa 24 Yakatokea mashindano kati yao, kwamba ni nani anayehesabiwa kuwa mkubwa. 25 Akawaambia, Wafalme wa Mataifa huwatawala, na wenye mamlaka juu yao huitwa Wenye fadhili; 26 lakini kwenu ninyi sivyo; bali aliye mkubwa kwenu na awe kama aliye mdogo; na mwenye kuongoza kama yule atumikaye. 27 Maana aliye mkubwa ni yupi? Yeye aketiye chakulani, au yule atumikaye? Siye yule aketiye chakulani? Lakini mimi kati yenu ni kama atumikaye. 28 Nanyi ndinyi mliodumu pamoja nami katika majaribu yangu. 29 Nami nawawekea ninyi ufalme, kama vile Baba yangu alivyoniwekea mimi; 30 mpate kula na kunywa mezani pangu katika ufalme wangu; na kuketi katika viti vya enzi, huku mkiyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli. Yesu atabiri kuhusu Petro kumkana 31 Akasema, Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; 32 lakini nimekuombea wewe ili imani yako isipungue; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako. 33 Akamwambia, Bwana, niwapo pamoja nawe, mimi ni tayari kwenda gerezani au hata kifoni. 34 Akasema, Nakuambia, Petro, jogoo hatawika leo, kabla wewe hujanikana mara tatu ya kuwa hunijui. Mfuko, mkoba, na upanga 35 Akawauliza, Je! Hapo nilipowatuma hamna mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu? Wakasema, La! 36 Akawaambia, Lakini sasa mwenye mfuko na auchukue, na mkoba vivyo hivyo; naye asiye na upanga, na auze joho lake akanunue. 37 Kwa kuwa nawaambia, hayo yaliyoandikwa hayana budi kutimizwa kwangu; ya kuwa, Alihesabiwa pamoja na wahalifu. Kwa sababu yanipasayo yanao mwisho wake. 38 Wakasema, Bwana, tazama, hapa pana panga mbili. Akawaambia, Basi. Yesu aomba katika mlima wa Mizeituni 39 Akatoka akaenda mpaka mlima wa Mizeituni kama ilivyokuwa desturi yake; wanafunzi wake nao wakafuatana naye. 40 Alipofika mahali pale aliwaambia, Ombeni kwamba msiingie majaribuni. 41 Mwenyewe akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba, 42 akisema, Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; lakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke. [ 43 Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu. 44 Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba; jasho yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchini.] 45 Alipoondoka katika kuomba kwake, akawajia wanafunzi wake, akawakuta wamelala usingizi kwa huzuni. 46 Akawaambia, Mbona mmelala usingizi? Ondokeni, mkaombe, msije mkaingia majaribuni. Kusalitiwa na kukamatwa kwa Yesu 47 Basi alipokuwa katika kusema, tazama, mkutano wa watu, na yule aitwaye Yuda, ambaye ni mmoja wa wale Kumi na Wawili, amewatangulia. Akamkaribia Yesu ili kumbusu. 48 Yesu akamwambia, Yuda, wamsaliti Mwana wa Adamu kwa kumbusu? 49 Na wale waliokuwa karibu naye walipoona yatakayotokea, walisema, Bwana, tuwapige kwa upanga? 50 Mmoja wao akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio la kulia. 51 Yesu akajibu akasema, Muwe radhi kwa hili. Akamgusa sikio, akamponya. 52 Yesu akawaambia wakuu wa makuhani, na maofisa wa hekalu, na wazee, waliokuja juu yake, Je! Mmekuja mkiwa na panga na marungu kama kukamata mnyang'anyi? 53 Kila siku nilipokuwa pamoja nanyi hekaluni hamkuninyoshea mikono, lakini hii ndiyo saa yenu, na mamlaka ya giza. Petro amkana Yesu 54 Wakamkamata, wakamchukua, wakaenda naye nyumbani kwa Kuhani Mkuu. Na Petro alimfuata kwa mbali. 55 Na walipokwisha washa moto katikati ya kiwanja, waliketi pamoja, naye Petro akaketi kati yao. 56 Ndipo mjakazi mmoja akamwona ameketi akiwa katika mwanga, akamkazia macho akasema, Na huyu alikuwa pamoja naye. 57 Akakana, akisema, Ee mwanamke, simjui. 58 Muda mfupi baadaye mtu mwingine alimwona akasema, Wewe nawe u mmoja wao. Petro akasema, Ee mtu, si mimi. 59 Halafu, yapata saa moja, mtu mwingine alikazia akisema, Hakika na huyu alikuwa pamoja naye, kwa kuwa yeye pia ni Mgalilaya. 60 Petro akasema, Ee mtu, sijui usemalo. Na papo hapo alipokuwa katika kusema, jogoo aliwika. 61 Bwana akageuka akamtazama Petro. Petro akalikumbuka lile neno la Bwana jinsi alivyomwambia, Leo kabla hajawika jogoo utanikana mara tatu. 62 Akatoka nje akalia kwa majonzi. Kumdhihaki na kumpiga Yesu 63 Na wale watu waliokuwa wakimshika Yesu walimfanyia dhihaka, wakampiga. 64 Wakamfunika macho, kisha wakamwulizauliza wakisema, Tabiri, ni nani aliyekupiga? 65 Wakamtolea na maneno mengine mengi ya kumtukana. Yesu mbele ya baraza 66 Kulipokucha, walikutanika jamii ya wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, wakamleta katika baraza yao, wakisema, 67 Kama wewe ndiwe Kristo, tuambie. Akawaambia, Nikiwaambia, hamtasadikia. 68 Tena, nikiwauliza, hamtajibu. 69 Lakini tangu sasa Mwana wa Adamu atakuwa ameketi upande wa kulia wa Mungu Mwenyezi. 70 Wakasema wote, Basi, wewe ndiwe Mwana wa Mungu? Akawaambia, Ninyi mwasema kwamba mimi ndiye. 71 Wakasema, Basi, tuna haja gani tena ya ushuhuda? Maana, sisi wenyewe tumesikia maneno ya kinywa chake. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya