Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Mwanzo 41 - Swahili Revised Union Version


Yusufu afasiri ndoto ya Farao

1 Ikawa, baada ya miaka miwili mizima, Farao akaota ndoto; na tazama, amesimama kando ya mto.

2 Na tazama, ng'ombe saba wazuri, wanono, walipanda kutoka mtoni, wakajilisha manyasini.

3 Na tazama, ng'ombe saba wengine wakapanda nyuma yao kutoka mtoni, wabaya, wamekonda, wakasimama karibu na wale ng'ombe wengine ukingoni mwa mto.

4 Kisha hao ng'ombe wabaya waliokonda wakawala wale ng'ombe saba wazuri, wanono. Basi Farao akaamka.

5 Akalala, akaota ndoto mara ya pili. Tazama, masuke saba yalimea katika bua moja, makubwa, mema.

6 Na tazama, masuke saba membamba, yamekaushwa na upepo wa mashariki, yakatokeza baada yao.

7 Kisha hayo masuke membamba saba yakayala yale masuke saba makubwa yaliyojaa. Basi Farao akaamka, kumbe! Ni ndoto tu.

8 Hata asubuhi roho yake ikafadhaika; akapeleka watu kuwaita waganga wote wa Misri, na watu wote wenye hekima walioko. Farao akawahadithia ndoto yake, wala hakuna aliyeweza kumfasiria Farao mambo hayo.

9 Basi mkuu wa wanyweshaji akamwambia Farao akisema, Nayakumbuka makosa yangu leo.

10 Farao aliwakasirikia watumishi wake, akanitia nifungwe nyumbani mwa mkuu wa askari walinzi, mimi na mkuu wa waokaji.

11 Tukaota ndoto usiku mmoja, mimi na yeye; kila mtu kwa tafsiri ya ndoto yake tukaota.

12 Na huko pamoja nasi palikuwa na kijana; Mwebrania, mtumishi wa mkuu wa askari, tukamhadithia, naye akatufasiria ndoto zetu; akamfasiria kila mtu kama ilivyokuwa ndoto yake.

13 Ikawa, kama vile alivyotufasiria ndivyo ilivyotokea; mimi nilirudishwa katika kazi yangu, na yeye alitundikwa.

14 Ndipo Farao akatuma watu kumwita Yusufu, wakamleta upesi kutoka gerezani. Akanyoa, akabadili nguo zake, na kuingia kwa Farao.

15 Farao akamwambia Yusufu, Nimeota ndoto, wala hakuna awezaye kunifasiria; nami nimesikia habari zako, ya kwamba, usikiapo ndoto, waweza kuifasiri.

16 Yusufu akamjibu Farao, akisema, Si mimi; Mungu atampa Farao majibu ya amani.

17 Farao akamwambia Yusufu, Katika ndoto yangu nilikuwa nimesimama ukingoni mwa mto;

18 na tazama, ng'ombe saba wanatoka mtoni, wanono, wazuri, wakajilisha nyasini.

19 Kisha, tazama, ng'ombe saba wengine wakapanda baada yao, dhaifu, wabaya sana, wamekonda; katika nchi yote ya Misri sijaona kama hao kwa udhaifu.

20 Na hao ng'ombe waliokonda, wabaya, wakawala wale ng'ombe saba wa kwanza, wale wanono.

21 Na walipowala haikutambulikana ya kwamba wamewala, bali wakaonekana wabaya kama kwanza. Basi nikaamka.

22 Kisha nikaona katika ndoto yangu, na tazama, masuke saba yanatokeza katika bua moja, mema, yamejaa.

23 Na tazama, masuke saba membamba, dhaifu, yamekaushwa na upepo wa mashariki, yakatokeza baada yao.

24 Na hayo masuke dhaifu yakameza yale masuke saba mema. Nami nikawaambia hao waganga, wala hakuna aliyeweza kunionesha maana yake.

25 Yusufu akamwambia Farao, Ndoto ya Farao ni moja; Mungu amemwonesha Farao atakayoyafanya hivi karibuni.

26 Wale ng'ombe saba wema ni miaka saba; na yale masuke saba mema ni miaka saba. Ndoto ni moja.

27 Na wale ng'ombe saba, dhaifu, wabaya, waliopanda baada yao, ni miaka saba; na yale masuke saba matupu yaliyokaushwa na upepo wa mashariki, yatakuwa miaka saba ya njaa.

28 Ndivyo nilivyomwambia Farao, ya kwamba Mungu amemwonesha Farao atakayoyafanya hivi karibu.

29 Tazama, miaka saba ya shibe inakuja, katika nchi yote ya Misri.

30 Kisha kutakuja miaka saba ya njaa baada yake; na shibe ile yote itasahauliwa katika nchi ya Misri, na njaa itaiharibu nchi.

31 Wala shibe ile haitajulikana katika nchi kwa sababu ya njaa inayokuja baadaye, maana itakuwa kali sana.

32 Na ndoto ya Farao kwa vile ilivyokuja mara mbili, ni kwa sababu neno hilo Mungu amelithibitisha, na Mungu atalitimiza upesi.

33 Basi, Farao na ajitafutie mtu wa akili na hekima amweke juu ya nchi ya Misri.

34 Farao na afanye hivi, tena akaweke wasimamizi juu ya nchi, na kutwaa sehemu ya tano katika nchi ya Misri, katika miaka hii saba ya kushiba.

35 Na wakusanye chakula chote cha miaka hii myema ijayo, wakaweke akiba ya nafaka mkononi mwa Farao wakakilinde kuwa chakula katika miji.

36 Na hicho chakula kitakuwa akiba ya nchi kwa ajili ya miaka hiyo saba ya njaa, itakayokuwa katika nchi ya Misri, nchi isiharibike kwa njaa.

37 Neno hilo likawa jema machoni pa Farao, na machoni pa watumishi wake wote.

38 Farao akawaambia watumishi wake, Tupate wapi mtu kama huyu, mwenye Roho ya Mungu ndani yake?

39 Farao akamwambia Yusufu, Kwa kuwa Mungu amekufahamisha hayo yote, hapana mwenye akili na hekima kama wewe.

40 Basi wewe utakuwa msimamizi wa nyumba yangu, na kwa neno lako watu wangu watatawaliwa. Katika kiti cha enzi tu nitakuwa mkuu kuliko wewe.

41 Farao akamwambia Yusufu, Tazama, nimekuweka juu ya nchi yote ya Misri.

42 Farao akavua pete yake ya mhuri mkononi mwake, akaitia mkononi mwa Yusufu; akamvika mavazi ya kitani nzuri, na kumtia mkufu wa dhahabu shingoni mwake.

43 Akampandisha katika gari lake la pili alilokuwa nalo. Na watu wakapiga kelele mbele yake, Pigeni magoti. Hivyo akamweka juu ya nchi yote ya Misri.

44 Farao akamwambia Yusufu, Mimi ni Farao, na bila amri yako, mtu asiinue mkono wala mguu katika nchi yote ya Misri.

45 Farao akamwita Yusufu, Safenath-panea; akamwoza Asenathi, binti Potifera, kuhani wa Oni, kuwa mkewe. Na Yusufu akaenda huku na huko katika nchi yote ya Misri.

46 Naye Yusufu alikuwa mwenye miaka thelathini, aliposimama mbele ya Farao, mfalme wa Misri. Yusufu akatoka mbele ya uso wa Farao, akasafiri katika nchi yote ya Misri.

47 Ikawa katika miaka ile saba ya shibe, nchi ilitoa mazao mengi kabla ya kuja kwa miaka ya njaa.

48 Akakusanya chakula chote cha miaka ile saba katika nchi ya Misri. Akaweka chakula katika miji; chakula cha mashamba yaliyouzunguka kila mji, akakiweka ndani yake.

49 Yusufu akakusanya nafaka kama mchanga wa pwani, nyingi mno, hata akaacha kuhesabu, maana ilikuwa haina hesabu.

50 Kabla ya kuja miaka ya njaa, Asenathi, binti Potifera, kuhani wa Oni, alimzalia Yusufu wana wawili.

51 Yusufu akamwita jina lake yule aliyezaliwa kwanza, Manase, maana alisema, Mungu amenisahaulisha taabu zangu zote, na nyumba yote ya baba yangu.

52 Na wa pili akamwita jina lake Efraimu, maana alisema, Mungu amenipa uzazi katika nchi ya mateso yangu.

53 Miaka ile saba ya shibe ikaisha katika nchi ya Misri,

54 ikaanza kuja miaka ile saba ya njaa, kama vile Yusufu alivyosema. Kukawa na njaa katika nchi zote, bali katika nchi yote ya Misri palikuwa na chakula.

55 Na nchi yote ya Misri ilipoona njaa, watu walimlilia Farao awape chakula. Farao akawaambia Wamisri wote, Nendeni kwa Yusufu; atakavyowaambia, fanyeni.

56 Njaa ikawa katika dunia yote pia. Yusufu akazifungua ghala zote, akawauzia Wamisri. Njaa ikawa nzito katika nchi ya Misri.

57 Watu wa nchi zote wakaja Misri kwa Yusufu; ili wanunue nafaka; kwa sababu njaa imekuwa nzito katika dunia yote.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo