Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Methali 12 - Swahili Revised Union Version

1 Kila apendaye mafundisho hupenda maarifa; Bali yeye achukiaye kulaumiwa ni kama mnyama.

2 Mtu mwema atapata upendeleo kwa BWANA; Bali mtu wa hila atahukumiwa naye.

3 Mtu hatathibitika kwa njia ya uovu; Shina la mwenye haki halitaondolewa kamwe.

4 Mwanamke mwema ni taji la mumewe; Bali aaibishaye ni kama kuoza mifupani mwake.

5 Mawazo ya mwenye haki ni adili; Bali mashauri ya mtu mwovu ni hadaa.

6 Maneno ya waovu huotea damu; Bali kinywa cha wanyofu kitawaokoa.

7 Waovu huangamia, hata hawako tena; Bali nyumba ya mwenye haki itasimama.

8 Mtu atasifiwa kwa kadiri ya akili zake; Bali mwenye moyo wa ukaidi atadharauliwa.

9 Afadhali mtu anayedharauliwa, ikiwa ana mtumwa, Kuliko ajisifuye, ikiwa anahitaji chakula.

10 Mwenye haki huufikiri uhai wa mnyama wake; Bali huruma za mtu mwovu ni ukatili.

11 Alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele; Bali afuataye mambo ya upuzi hana ufahamu.

12 Asiye haki hutamani nyavu za wabaya; Bali shina lao wenye haki huleta matunda.

13 Katika kosa la midomo kuna mtego kwa mbaya; Bali mwenye haki atatoka katika taabu.

14 Mtu atashiba mema kwa matunda ya kinywa chake; Na atarudishiwa matendo ya mikono yake.

15 Njia ya mpumbavu imenyoka machoni pake mwenyewe; Bali yeye aliye na hekima husikiliza shauri.

16 Ghadhabu ya mpumbavu hujulikana mara; Bali mtu mwerevu husitiri aibu.

17 Atamkaye maneno ya kweli hufunua haki; Bali shahidi wa uongo hutamka hila.

18 Kuna anenaye bila kufikiri, kama kuchoma kwa upanga; Bali ulimi wa mwenye haki ni afya.

19 Mdomo wa kweli utathibitishwa milele; Bali ulimi wa uongo ni wa kitambo tu.

20 Hila imo mioyoni mwao wafikirio uovu; Bali wafanyao mashauri ya amani, kwao kuna furaha.

21 Mwenye haki hatapatikana na msiba wowote; Bali wasio haki watajazwa mabaya.

22 Midomo ya uongo ni chukizo kwa BWANA; Bali watendao uaminifu ndio furaha yake.

23 Mwanadamu mwenye busara husitiri maarifa; Bali moyo wa wapumbavu hutangaza upumbavu.

24 Mkono wa mwenye bidii utatawala; Bali mvivu atalipishwa kodi.

25 Uzito katika moyo wa mtu huuinamisha; Bali neno jema huufurahisha.

26 Mwenye haki ni kiongozi wa mwenzake; Bali njia ya wasio haki huwakosesha.

27 Mtu mvivu hapiki mawindo yake; Bali mwenye bidii anazo mali za thamani.

28 Katika njia ya haki kuna uhai; Wala hakuna mauti katika mapito yake.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo