Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Hesabu 3 - Swahili Revised Union Version


Wana wa Haruni

1 Basi vizazi vya Haruni na Musa, siku hiyo BWANA aliyosema na Musa katika mlima wa Sinai, ni hivi.

2 Tena majina ya hao wana wa Haruni ni haya; Nadabu mzaliwa wa kwanza, na Abihu, na Eleazari, na Ithamari.

3 Hayo ndiyo majina ya wana wa Haruni, hao makuhani waliotiwa mafuta, ambao aliwaweka wakfu ili wafanye kazi ya ukuhani.

4 Kisha Nadabu na Abihu walikufa mbele za BWANA, waliposongeza moto wa kigeni mbele za BWANA, katika jangwa la Sinai, nao walikuwa hawana wana; na Eleazari na Ithamari wakafanya kazi ya ukuhani wakati wa uhai wa Haruni baba yao.


Wajibu wa Walawi

5 Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,

6 Lilete karibu kabila la Lawi, ukawaweke mbele ya Haruni kuhani, ili wapate kumtumikia.

7 Nao watamtumikia pamoja na watu wote mbele ya hema ya kukutania, kwa kuhudumu katika maskani.

8 Nao watavitunza vyombo vyote vya hema ya kukutania, na kuwatumikia wana wa Israeli, kwa kuhudumu katika maskani.

9 Nawe utawapa Haruni na wanawe hao Walawi wawe nao; amepewa watu hao kabisa kwa ajili ya wana wa Israeli.

10 Nawe utawaweka Haruni na wanawe, nao wataushika ukuhani wao, na mgeni atakayekaribia atauawa.

11 Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,

12 Mimi, tazama, nimewateua Walawi na kuwatoa kati ya wana wa Israeli badala ya kila mzaliwa wa kwanza wote wafunguao tumbo katika wana wa Israeli; na hao Walawi watakuwa wangu;

13 kwa kuwa hao wazaliwa wa kwanza wote ni wangu; katika siku ile niliyowapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri nikajiwekea wakfu wazaliwa wa kwanza wote wa Israeli, wa wanadamu na wa wanyama; watakuwa wangu; mimi ndimi BWANA.


Hesabu ya Walawi

14 Kisha BWANA akanena na Musa huko katika jangwa la Sinai, na kumwambia,

15 Uwahesabu wana wa Lawi kwa kufuata nyumba za baba zao na jamaa zao; kila mwanamume kuanzia umri wa mwezi mmoja na zaidi utawahesabu.

16 Basi Musa akawahesabu kama alivyoagizwa na neno la BWANA.

17 Na wana wa Lawi walikuwa ni hawa kwa majina yao; Gershoni, na Kohathi, na Merari.

18 Na majina ya wana wa Gershoni kwa jamaa zao ni Libni na Shimei.

19 Na wana wa Kohathi kwa jamaa zao ni Amramu, na Ishari, na Hebroni, na Uzieli.

20 Na wana wa Merari kwa jamaa zao ni Mahli, na Mushi. Hizi ndizo jamaa za Walawi kwa nyumba za baba zao.

21 Katika Gershoni walikuwa jamaa ya Walibni, na jamaa ya Washimei, hawa ndio jamaa za Wagershoni.

22 Hao waliohesabiwa kwao, kama hesabu ya wanaume wote, kuanzia umri wa mwezi mmoja na zaidi, hao waliohesabiwa kwao walikuwa elfu saba na mia tano.

23 Jamaa za Wagershoni wapigavyo kambi nyuma ya maskani, upande wa magharibi.

24 Na mkuu wa nyumba ya baba zao Wagershoni atakuwa Eliasafu mwana wa Laeli.

25 Na kazi ya Wageruhoni katika hema ya kukutania ni hiyo ya kuhudumu katika maskani, Hema na kifuniko chake, na pazia la mlango wa hema ya kukutania,

26 na kuta za nguo za ua, na sitara ya mlango wa ua, iliyo karibu na maskani, na karibu na madhabahu pande zote, na kamba zake zitumiwazo kwa matumizi yake yote.

27 Na katika Kohathi ni jamaa ya Waamrami, na jamaa ya Waishari, na jamaa ya Wahebroni, na jamaa ya hao Wauzieli; hizo ni jamaa za Wakohathi.

28 Kama hesabu ya wanaume wote, kuanzia umri wa mwezi mmoja na zaidi, walikuwa elfu nane na mia sita, wenye kuhudumu katika mahali patakatifu.

29 Jamaa za wana wa Kohathi watapiga kambi upande wa kusini wa maskani.

30 Na mkuu wa nyumba ya baba za jamaa za Wakohathi atakuwa Elisafani mwana wa Uzieli.

31 Na vitu watakavyovitunza ni hilo sanduku, na meza, na kinara cha taa, na madhabahu, na vile vyombo vya mahali patakatifu wavitumiavyo katika huduma yao, na pazia, na utumishi wake wote.

32 Na Eleazari mwana wa Haruni kuhani atakuwa mkuu wa hao wakuu wa Walawi, naye atawasimamia hao wahudumu wa mahali patakatifu.

33 Katika Merari ni jamaa ya hao Wamahli, na jamaa ya Wamushi; hizo ni jamaa za Merari.

34 Na hao waliohesabiwa kwao, kama hesabu ya wanaume wote, kuanzia umri wa mwezi mmoja na zaidi, walikuwa elfu sita na mia mbili.

35 Na mkuu wa nyumba ya baba za jamaa za Merari alikuwa Surieli mwana wa Abihaili; hao watapiga kambi upande wa maskani, wa kaskazini.

36 Na usimamizi walioamriwa wana wa Merari ulikuwa ni kutunza mbao za maskani, na mataruma yake, na nguzo zake, na vitako vyake, na vyombo vyake vyote, na utumishi wake wote;

37 na nguzo za ua zilizouzunguka, na vitako yake, na vigingi vyake, na kamba zake.

38 Na hao watakaopanga mbele ya maskani upande wa mashariki, mbele ya hema ya kukutania upande wa kuelekea maawio ya jua, watakuwa hawa, Musa na Haruni na wanawe, wenye kulinda ulinzi wa mahali patakatifu, yaani, huo ulinzi wa wana wa Israeli; na mgeni atakayekaribia atauawa.

39 Hao wote waliohesabiwa katika Walawi, ambao Musa na Haruni waliwahesabu kwa amri ya BWANA, kwa jamaa zao, wanaume wote kuanzia umri wa mwezi mmoja na zaidi, walikuwa elfu ishirini na mbili.


Ukombozi wa mzaliwa wa kwanza

40 Kisha BWANA akamwambia Musa, Uwahesabu wanaume wote wazaliwa wa kwanza katika wana wa Israeli kuanzia umri wa mwezi mmoja na zaidi uyahesabu majina yao.

41 Nawe utawatwaa Walawi kwa ajili yangu mimi (Mimi ndimi BWANA) badala ya hao wazaliwa wa kwanza wote katika wana wa Israeli; na wanyama wa Walawi badala ya wazaliwa wa kwanza wa wanyama wa wana wa Israeli.

42 Musa akahesabu, kama BWANA alivyomwagiza, wazaliwa wa kwanza wote katika wana wa Israeli.

43 Wazaliwa wa kwanza wote walio wanaume kwa hesabu ya majina, kuanzia umri wa mwezi mmoja na zaidi, katika hao waliohesabiwa kwao, walikuwa elfu ishirini na mbili na mia mbili na sabini na watatu.

44 Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,

45 Uwaweke Walawi badala ya wazaliwa wa kwanza katika wana wa Israeli, na wanyama wa Walawi badala ya wanyama wao; na hao Walawi watakuwa wangu mimi; mimi ndimi BWANA.

46 Tena kwa kuwakomboa hao watu mia mbili na sabini na watatu, wa hao wazaliwa wa kwanza wa Israeli, ambao wamezidi ile hesabu ya Walawi,

47 utatwaa shekeli tano kwa kichwa cha kila mtu kwa hiyo shekeli ya mahali patakatifu (shekeli ni gera ishirini);

48 na hizo fedha ambazo walizidi wamekombolewa kwazo utampa Haruni na wanawe.

49 Basi Musa akawatoza fedha za ukombozi, hao waliozidi hesabu ya wale waliokombolewa na Walawi;

50 akatwaa hizo fedha kwa wazaliwa wa kwanza wa wana wa Israeli; shekeli elfu moja na mia tatu na sitini na tano kwa shekeli ya mahali patakatifu;

51 kisha hizo fedha za ukombozi Musa akampa Haruni na wanawe, kama neno la BWANA, kama BWANA alivyomwagiza Musa.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo