Methali 13 - Swahili Revised Union Version1 Mwana mwenye hekima husikiliza mausia ya babaye; Bali mwenye dharau hasikilizi maonyo. 2 Mtu atakula mema kwa matunda ya kinywa chake; Bali nafsi ya mtu haini itakula jeuri. 3 Yeye alindaye kinywa chake huilinda nafsi yake; Bali afunuaye midomo yake atapata uharibifu. 4 Nafsi ya mtu mvivu hutamani asipate kitu; Bali nafsi ya mwenye bidii itanenepeshwa. 5 Mwenye haki huchukia kusema uongo; Bali mtu mbaya huwa karaha, hupatwa na aibu. 6 Haki humlinda yeye aliye mnyofu katika njia yake; Bali ubaya humwangusha mwenye dhambi. 7 Kuna mtu anayejitajirisha, lakini hana kitu; Kuna anayejifanya kuwa maskini, lakini ana mali nyingi. 8 Fidia ya nafsi ya mtu ni utajiri wake; Bali mtu maskini hasikii ogofyo lolote. 9 Nuru ya mwenye haki yang'aa sana; Bali taa ya mtu mbaya itazimika. 10 Kiburi huleta mashindano tu; Bali hekima hukaa nao wanaoshauriana. 11 Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka; Bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa. 12 Kilichotarajiwa kikikawia kuja, moyo huugua. Bali haja ya mtu ikipatikana, ni mti wa uzima. 13 Kila anayelidharau neno hujiletea uharibifu; Bali yeye anayeiogopa amri atapewa thawabu. 14 Sheria ya mwenye akili ni chemchemi ya uzima, Ili kuepukana na tanzi za mauti. 15 Ufahamu mwema huleta upendeleo; Bali njia ya muasi huangamiza. 16 Kila aliye na busara hutenda kazi kwa maarifa; Bali mpumbavu hueneza upumbavu. 17 Mjumbe mbaya huanguka maovuni; Bali mjumbe mwaminifu ni afya. 18 Umaskini na fedheha zitampata yeye akataaye kurudiwa; Bali yeye aangaliaye maonyo ataheshimiwa. 19 Haja iliyopatikana ni tamu nafsini mwa mtu; Bali kujitenga na maovu ni chukizo kwa wapumbavu. 20 Nenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia. 21 Uovu huwafuatia wenye dhambi; Bali mwenye haki atalipwa mema. 22 Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi; Na mali ya mkosaji huwa akiba kwa mwenye haki. 23 Chakula kingi chapatikana kwa ukulima wa maskini; Bali viko viharibiwavyo kwa sababu ya dhuluma. 24 Yeye asiyetumia fimbo yake humchukia mwanawe; Bali yeye ampendaye humrudi mapema. 25 Mwenye haki hula akaishibisha nafsi yake; Bali tumbo la mtu mbaya litaona njaa. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya