Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Methali 27 - Swahili Revised Union Version

1 Usijisifu kwa ajili ya kesho; Kwa maana hujui yatakayozaliwa na siku moja.

2 Mwingine na akusifu wala si kinywa chako mwenyewe; Mtu mgeni wala si midomo yako wewe.

3 Jiwe ni zito, na mchanga hulemea; Lakini ghadhabu ya mpumbavu ni nzito kuliko hivi vyote viwili.

4 Ghadhabu ni kali, na hasira ni gharika; Lakini ni nani awezaye kusimama mbele ya wivu.

5 Lawama ya wazi ni heri, Kuliko upendo uliositirika.

6 Majeraha utiwazo na rafiki ni ya kweli; Bali busu la adui ni udanganyifu.

7 Nafsi iliyoshiba hukinai sega la asali; Bali nafsi yenye njaa huona kila kitu kichungu kuwa kitamu.

8 Kama ndege aendaye huku na huko mbali na kitundu chake; Ndivyo alivyo mtu aendaye huku na huko mbali na mahali pake.

9 Marhamu na manukato huufurahisha moyo; Kadhalika utamu wa rafiki ya mtu utokao katika kusudi la moyo wake.

10 Usimwache rafiki yako mwenyewe, wala rafiki ya baba yako, Wala usiende nyumbani mwa ndugu yako siku ya msiba wako. Afadhali jirani aliye karibu kuliko ndugu aliye mbali.

11 Mwanangu, uwe na hekima na kunifurahisha moyo wangu; Ili nipate kumjibu anilaumuye.

12 Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha; Bali wajinga huendelea mbele wakaumia.

13 Twaa nguo yake amdhaminiye mgeni; Mtoza rehani aliye mdhamini wa malaya.

14 Mtu ambarikiye mwenzake kwa sauti kuu asubuhi na mapema; Itahesabiwa kuwa ni laana kwake.

15 Matone daima kudondoka siku ya mvua nyingi, Na mwanamke mgomvi ni sawasawa;

16 Atakaye kumzuia huyo huuzuia upepo; Na mkono wake wa kulia hukuta mafuta.

17 Chuma hunoa chuma; Ndivyo mtu aunoavyo uso wa rafiki yake.

18 Yeye autunzaye mtini atakula matunda yake; Naye amhudumiaye bwana wake ataheshimiwa.

19 Kama uso ufananavyo na uso katika maji; Kadhalika moyo wa mtu na mwenzake.

20 Kuzimu na Uharibifu havishibi; Wala macho ya wanadamu hayashibi.

21 Kalibu ni kwa fedha, na tanuri kwa dhahabu; Na mtu hujaribiwa kwa sifa zake.

22 Hata ukimtwanga mpumbavu kwa mchi kinuni pamoja na ngano; Upumbavu wake hautamtoka.

23 Fanya bidii kuijua hali ya makundi yako; Na kuwaangalia sana ng'ombe wako.

24 Kwa maana mali haziwi za milele; Na taji je! Ladumu tangu kizazi hata kizazi?

25 Manyasi hukatwa, na majani mabichi huchipua, Na mboga ya mlimani hukusanywa.

26 Wana-kondoo hufaa kwa mavazi yako; Na mbuzi ni thamani ya shamba.

27 Tena yatakuwapo maziwa ya mbuzi, Ya kukutosha kwa chakula chako, Na chakula cha watu wa nyumbani mwako, Na posho la vijakazi vyako.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo