Luka 23 - Swahili Revised Union VersionYesu mbele ya Pilato 1 Kisha mkutano wote wakasimama, wakampeleka kwa Pilato. 2 Wakaanza kumshitaki, wakisema, Tumemwona huyu akipotosha taifa letu, na kuwazuia watu wasimpe Kaisari kodi, akisema kwamba yeye mwenyewe ni Kristo, mfalme. 3 Pilato akamwuliza, akisema, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Akajibu akamwambia, Wewe wasema. 4 Pilato akawaambia wakuu wa makuhani na mkutano, Sioni neno lililo ovu katika mtu huyu. 5 Nao walisisitiza sana, wakisema, Huwataharakisha watu, akifundisha katika Yudea yote, tokea Galilaya mpaka huku. Yesu mbele ya Herode 6 Pilato aliposikia hayo aliuliza kama huyu ni mtu wa Galilaya. 7 Na alipopata habari ya kuwa yu chini ya mamlaka ya Herode, alimpeleka kwa Herode, kwa kuwa yeye naye alikuwapo Yerusalemu siku zile. 8 Herode alipomwona Yesu alifurahi sana, kwa sababu alikuwa akitaka sana kumwona tangu siku nyingi, maana amesikia habari zake, akatarajia kuona ishara iliyofanywa na yeye. 9 Akamwuliza maneno mengi, yeye asimjibu lolote. 10 Wakuu wa makuhani na waandishi wakasimama wakamshitaki kwa nguvu sana. 11 Basi Herode akamdhalilisha, pamoja na askari wake, akamdhihaki, na kumvika mavazi mazuri; kisha akamrudisha kwa Pilato. 12 Basi siku ile ile Herode na Pilato walipatana kwa urafiki kwa maana hapo kwanza walikuwa na uadui wao kwa wao. Yesu ahukumiwa Kifo 13 Na Pilato akawakutanisha wakuu wa makuhani, na wakubwa, na watu, 14 akawaambia, Mtu huyu mmemleta kwangu kana kwamba anapotosha watu; nami, tazama, nimeamua mambo yake mbele yenu, ila sikuona kwake kosa lolote katika mambo hayo mliyomshitaki; 15 wala hata Herode, kwa maana amemrudisha kwetu; basi tazama, hakuna neno lolote alilolitenda lipasalo kufa. 16 Kwa hiyo nitamrudi, kisha nitamfungua. [ 17 Maana ilimlazimu kuwafungulia mfungwa mmoja wakati wa sikukuu.] 18 Wakapiga kelele wote pamoja, wakisema, Mwondoe huyu, utufungulie Baraba. 19 Naye ni mtu aliyetupwa gerezani kwa ajili ya fitina iliyotokea mjini, na kwa uuaji 20 Basi Pilato alisema nao mara ya pili, kwa vile alivyotaka kumfungua Yesu. 21 Lakini wakapiga kelele, wakisema, Msulubishe. Msulubishe. 22 Akawaambia mara ya tatu, Kwa sababu gani? Huyu ametenda uovu gani? Sikuona kwake hata neno lipasalo kufa. Basi nikiisha kumrudi nitamfungua. 23 Lakini wakatoa sauti zao kwa nguvu sana, wakitaka asulubiwe. Sauti zao zikashinda. 24 Pilato akahukumu kwamba haja yao ifanyike. 25 Akamfungua yule aliyetupwa gerezani kwa ajili ya fitina na uuaji, yule waliyemtaka, akamtoa Yesu wamfanyie watakavyo. Kusulubiwa kwa Yesu 26 Na walipokuwa wakimwondoa walimkamata mtu mmoja, Simoni Mkirene, aliyekuwa ametoka shambani, wakamtwika msalaba, auchukue nyuma yake Yesu. 27 Mkutano mkubwa wa watu wakamfuata, na wanawake waliokuwa wakijipiga vifua na kumwombolezea. 28 Yesu akawageukia, akasema, Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu. 29 Kwa maana tazama, siku zitakuja watakaposema, Heri walio tasa, na matumbo yasiyozaa, na maziwa yasiyonyonyesha. 30 Ndipo watakapoanza kuiambia milima, Tuangukieni, na vilima, Tufunikeni. 31 Kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu? 32 Wakapelekwa na wawili wengine, wahalifu, wauawe pamoja naye. 33 Na walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, ndipo walipomsulubisha yeye, na wale wahalifu, mmoja upande wa kulia, na mmoja upande wa kushoto. 34 Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Wakagawa mavazi yake, wakipiga kura. 35 Watu wakasimama wakitazama. Wale wakuu nao walikuwa wakimfanyia mzaha, wakisema, Aliokoa wengine; na ajiokoe mwenyewe, kama ndiye Kristo wa Mungu, mteule wake. 36 Wale askari nao wakamfanyia dhihaka, wakimwendea na kumletea siki, 37 huku wakisema, Kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi, ujiokoe mwenyewe. 38 Na juu yake palikuwa na anwani; HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI. 39 Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi. 40 Lakini yule wa pili akamjibu akamkemea, akisema, Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo? 41 Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lolote lisilofaa. 42 Kisha akasema, Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako. 43 Yesu akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi. Kifo cha Yesu 44 Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hadi saa tisa, 45 jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati. 46 Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu. 47 Alipokwisha kusema hayo alikata roho. Yule jemadari alipoona yaliyotukia, alimtukuza Mungu, akisema, Hakika yake, mtu huyu alikuwa mwenye haki. 48 Na makutano yote ya watu waliokuwa wamekutanika kutazama mambo hayo, walipoona yaliyotendeka, wakaenda zao kwao, wakijipigapiga vifua. 49 Na wote waliojuana naye, na wale wanawake walioandamana naye toka Galilaya, wakasimama kwa mbali, wakitazama mambo hayo. Kuzikwa kwa Yesu 50 Na tazama, akatoka mtu mmoja, jina lake Yusufu, ambaye ni mtu wa baraza, mtu mwema, mwenye haki; 51 (wala hakulikubali shauri na tendo lao), naye ni mtu wa Arimathaya, mji mmoja wa Wayahudi, tena anautazamia ufalme wa Mungu; 52 mtu huyo alikwenda kwa Pilato, akataka kupewa mwili wa Yesu. 53 Akaushusha, akauzinga sanda ya kitani, akauweka katika kaburi lililochongwa mwambani, ambalo hajalazwa mtu bado ndani yake. 54 Na siku ile ilikuwa siku ya Maandalio, na sabato ikaanza kuingia. 55 Na wale wanawake waliokuja naye toka Galilaya walifuata, wakaliona kaburi, na jinsi mwili wake ulivyowekwa. 56 Wakarudi, wakatayarisha manukato na marhamu. Na siku ya sabato walistarehe kama ilivyoamriwa. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya