Mwanzo 5 - Swahili Revised Union VersionWazawa wa Adamu 1 Hiki ndicho kitabu cha vizazi vya Adamu. Siku ile Mungu alipoumba mtu, kwa sura ya Mungu alimfanya; 2 mwanamume na mwanamke aliwaumba, akawabariki akawaita jina lao Adamu, siku ile walipoumbwa. 3 Adamu akaishi miaka mia moja na thelathini, akazaa mwana kwa sura yake, kwa mfano wake, akamwita jina lake Sethi. 4 Siku za Adamu baada ya kumzaa Sethi zilikuwa miaka mia nane, akazaa wana, wa kiume na wa kike. 5 Siku zote za Adamu alizoishi ni miaka mia tisa na thelathini, naye akafa. 6 Sethi akaishi miaka mia moja na mitano, akamzaa Enoshi. 7 Sethi akaishi baada ya kumzaa Enoshi miaka mia nane na saba, akazaa wana, wa kiume na wa kike. 8 Siku zote za Sethi ni miaka mia tisa na kumi na miwili, akafa. 9 Enoshi akaishi miaka tisini, akamzaa Kenani. 10 Enoshi akaishi baada ya kumzaa Kenani miaka mia nane na kumi na mitano, akazaa wana, wa kiume na wa kike. 11 Siku zote za Enoshi ni miaka mia tisa na mitano, akafa. 12 Kenani akaishi miaka sabini, akamzaa Mahalaleli. 13 Kenani akaishi baada ya kumzaa Mahalaleli miaka mia nane na arubaini, akazaa wana, wa kiume na wa kike. 14 Siku zote za Kenani ni miaka mia tisa na kumi, akafa. 15 Mahalaleli akaishi miaka sitini na mitano, akamzaa Yaredi. 16 Mahalaleli akaishi baada ya kumzaa Yaredi miaka mia nane na thelathini, akazaa wana, wa kiume na wa kike. 17 Siku zote za Mahalaleli ni miaka mia nane na tisini na mitano, akafa. 18 Yaredi akaishi miaka mia moja na sitini na miwili, akamzaa Henoko. 19 Yaredi akaishi baada ya kumzaa Henoko miaka mia nane, akazaa wana, wa kiume na wa kike. 20 Siku zote za Yaredi ni miaka mia tisa na sitini na miwili, akafa. 21 Henoko akaishi miaka sitini na mitano, akamzaa Methusela. 22 Henoko akaenda pamoja na Mungu. Baada ya kumzaa Methusela aliishi miaka mia tatu, akazaa wana, wa kiume na wa kike. 23 Siku zote za Henoko ni miaka mia tatu na sitini na mitano. 24 Henoko akaenda pamoja na Mungu, naye akatoweka, maana Mungu alimtwaa. 25 Methusela akaishi miaka mia moja na themanini na saba, akamzaa Lameki. 26 Methusela akaishi baada ya kumzaa Lameki miaka mia saba na themanini na miwili, akazaa wana, wa kiume na wa kike. 27 Siku zote za Methusela ni miaka mia tisa na sitini na tisa, akafa. 28 Lameki akaishi miaka mia moja na themanini na miwili, akazaa mwana. 29 Akamwita jina lake Nuhu, akinena, Huyu ndiye atakayetufariji kwa kazi yetu na kwa taabu ya mikono yetu katika nchi aliyoilaani BWANA. 30 Lameki akaishi baada ya kumzaa Nuhu miaka mia tano na tisini na mitano, akazaa wana, wa kiume na wa kike. 31 Siku zote za Lameki ni miaka mia saba na sabini na saba, akafa. 32 Baada ya Nuhu kufikisha umri wa miaka mia tano, aliwazaa Shemu, na Hamu, na Yafethi. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya