Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Methali 18 - Swahili Revised Union Version

1 Ajitengaye na wenzake hutafuta matakwa yake mwenyewe; Hushindana na kila shauri jema.

2 Mpumbavu hapendezwi na ufahamu; Ila moyo wake udhihirike tu.

3 Ajapo asiye haki, huja dharau pia; Na pamoja na aibu huja lawama.

4 Maneno ya kinywa cha mtu ni kama maji ya vilindi; Kijito kibubujikacho; chemchemi ya hekima.

5 Kukubali uso wake asiye haki si vizuri; Wala kumpotosha mwenye haki hukumuni.

6 Midomo ya mpumbavu huingia katika fitina, Na kinywa chake huita mapigo.

7 Kinywa cha mpumbavu ni uharibifu wake, Na midomo yake ni mtego wa nafsi yake.

8 Maneno ya mchongezi ni kama vitoweo; Nayo hushukia pande za ndani za tumbo.

9 Yeye naye aliye mvivu katika kazi yake, Ni ndugu yake aliye mharibifu.

10 Jina la BWANA ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama.

11 Mali ya mtu tajiri ni mji wake wa nguvu; Ni kama ukuta mrefu katika mawazo yake.

12 Kabla ya uharibifu moyo wa mwanadamu hujivuna; Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu.

13 Yeye ajibuye kabla hajasikia, Ni upumbavu na aibu kwake.

14 Roho ya mtu itastahimili udhaifu wake; Bali roho iliyovunjika nani awezaye kuistahimili?

15 Moyo wa mwenye busara hupata maarifa; Na sikio la mwenye hekima hutafuta maarifa.

16 Zawadi ya mtu humpatia nafasi; Humleta mbele ya watu wakuu.

17 Ajiteteaye kwanza huonekana kuwa ana haki; Lakini jirani yake huja na kumchunguza.

18 Kura hukomesha mashindano; Hukata maneno ya wakuu.

19 Ndugu aliyechukizwa ni mgumu kuliko mji wa nguvu; Na mashindano ni kama mapingo ya ngome.

20 Tumbo la mtu litajazwa matunda ya kinywa chake; Atashiba mazao ya midomo yake.

21 Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake.

22 Apataye mke apata kitu chema; Naye ajipatia kibali kwa BWANA.

23 Maskini hutumia maombi; Bali tajiri hujibu kwa ukali.

24 Ajifanyiaye marafiki wengi ni kwa maangamizi yake mwenyewe; Lakini yuko rafiki aambatanaye na mtu kuliko ndugu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo