Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Mathayo 14 - Swahili Revised Union Version


Kuuawa kwa Yohana Mbatizaji

1 Wakati ule mfalme Herode alisikia habari za Yesu, akawaambia watumishi wake,

2 Huyo ndiye Yohana Mbatizaji; amefufuka katika wafu; na kwa hiyo nguvu hizo zinatenda kazi ndani yake.

3 Maana Herode alikuwa amemkamata Yohana, akamfunga, akamtia gerezani, kwa ajili ya Herodia, mke wa Filipo nduguye.

4 Kwa sababu Yohana alimwambia, Si halali kwako kuwa naye.

5 Naye alipotaka kumwua, aliwaogopa watu, maana walimwona Yohana kuwa nabii.

6 Hata ilipofika sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti ya Herodia alicheza mbele ya watu, akampendeza Herode.

7 Hata akaahidi kwa kiapo ya kwamba atampa lolote atakaloliomba.

8 Naye, huku akichochewa na mamaye, akasema, Nipe hapa katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji.

9 Naye mfalme akasikitika; lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya wale walioketi karamuni pamoja naye, akaamuru apewe;

10 akatuma mtu, akamkata kichwa Yohana mle gerezani.

11 Kichwa chake kikaletwa katika kombe, akapewa yule msichana; akakileta kwa mamaye.

12 Wanafunzi wake wakaenda, wakamchukua yule maiti, wakamzika; kisha wakaenda wakampasha Yesu habari.


Kulishwa kwa watu elfu tano

13 Naye Yesu aliposikia hayo, aliondoka huko katika mashua, akaenda mahali pasipo watu, faraghani. Na makutano waliposikia, walimfuata kwa miguu kutoka mijini mwao.

14 Yesu akatoka, akaona mkutano mkuu, akawahurumia, akawaponya wagonjwa wao.

15 Hata kulipokuwa jioni, wanafunzi wake walimwendea, wakasema, Mahali hapa ni nyika tupu, na saa imekwisha pita; uwaage makutano, waende zao vijijini, wakajinunulie vyakula.

16 Yesu akawaambia, Hawana haja kwenda zao, wapeni ninyi vyakula.

17 Wakamwambia, Hamna kitu hapa ila mikate mitano na samaki wawili.

18 Akasema, Nileteeni hapa.

19 Akawaagiza makutano waketi katika majani; akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akabariki, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi, wanafunzi wakawapa makutano.

20 Wakala wote wakashiba; wakayaokota mabaki ya vipande vya mikate, vikapu kumi na viwili, vimejaa.

21 Nao waliokula walikuwa wanaume wapatao elfu tano, bila kuhesabu wanawake na watoto.


Yesu atembea juu ya maji

22 Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande katika mashua na kutangulia mbele yake kwenda ng'ambo, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano.

23 Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake.

24 Na ile mashua imekwisha kufika katikati ya bahari, inapigwa sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa unawakabili.

25 Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari.

26 Wanafunzi walipomwona akitembea juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni mzimu; wakapiga yowe kwa hofu.

27 Mara Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo, ni mimi; msiogope.

28 Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji.

29 Akasema, Njoo. Petro akashuka katika mashua, akatembea juu ya maji, ili kumwendea Yesu.

30 Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe.

31 Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka?

32 Nao walipopanda katika mashua, upepo ulikoma.

33 Nao waliokuwamo ndani ya mashua wakamsujudia, wakisema, Hakika wewe u Mwana wa Mungu.


Yesu awaponya wagonjwa katika Genesareti

34 Na walipokwisha kuvuka, walifika nchi ya Genesareti.

35 Na watu wa mahali pale walipomtambua, walituma watu kwenda nchi zile zilizo kandokando, wakamletea wote waliokuwa wagonjwa;

36 nao wakamsihi waguse hata pindo la vazi lake tu; na wote waliogusa wakaponywa kabisa.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo