Marko 4 - Swahili Revised Union VersionMfano wa mpanzi 1 Akaanza kufundisha tena kando ya ziwa. Kundi kubwa sana la watu wakamkusanyikia, hata yeye akapanda katika mashua, akakaa ziwani, watu wote walikuwa katika nchi kavu kando ya ziwa. 2 Akawafundisha mambo mengi kwa mifano, akawaambia katika mafundisho yake, 3 Sikilizeni; Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda; 4 ikawa alipokuwa akipanda, mbegu nyingine ilianguka kando ya njia, wakaja ndege wakaila. 5 Nyingine ikaanguka penye mwamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara ikaota kwa kuwa na udongo haba; 6 hata jua lilipozuka iliungua, na kwa kuwa haina mizizi ikanyauka. 7 Nyingine ikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea ikaisonga, isizae matunda. 8 Nyingine zikaanguka penye udongo ulio mzuri, zikazaa matunda, zikimea na kukua, na kuzaa, moja thelathini, moja sitini, na moja mia. 9 Akasema, Aliye na masikio ya kusikilia, na asikie. Makusudi ya mifano 10 Naye alipokuwa peke yake, wale watu waliomzunguka, na wale Kumi na Wawili, walimwuliza kuhusu ile mifano. 11 Akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuijua siri ya ufalme wa Mungu, bali kwa wale walio nje, yote hufanywa kwa mifano, 12 ili wakitazama watazame, wasione; Na wakisikia wasikie, wasielewe; Wasije wakaongoka, na kusamehewa. 13 Akawaambia, Hamjui mfano huu? Basi mifano yote mtaitambuaje? 14 Mpanzi huyo hulipanda neno. 15 Hawa ndio walio kando ya njia lipandwapo neno; nao, wakiisha kusikia, mara huja Shetani, akaliondoa lile neno lililopandwa mioyoni mwao. 16 Kadhalika na hawa ndio wapandwao penye miamba, ambao kwamba wakiisha kulisikia lile neno, mara hulipokea kwa furaha; 17 ila hawana mizizi ndani yao, bali hudumu muda mchache; kisha ikitokea dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara hujikwaa. 18 Na hawa ndio wale wapandwao penye miiba; ni watu walisikiao lile neno, 19 na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali, na tamaa za mambo mengine zikiingia, hulisonga lile neno, likawa halizai. 20 Na hawa ndio waliopandwa penye udongo ulio mzuri; ni watu walisikiao lile neno na kulipokea, na kuzaa matunda, mmoja thelathini, mmoja sitini, na mmoja mia. Taa chini ya pishi 21 Akawaambia, Mwaonaje? Taa huja ili kuwekwa chini ya pishi, au mvunguni? Si kuwekwa juu ya kiango? 22 Kwa maana hakuna neno lililositirika, ila kusudi lije kudhihirika; wala hakuna lililofichwa, ila kusudi lije kutokea wazi. 23 Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie. 24 Akawaambia, Angalieni msikialo; kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa, na tena mtazidishiwa. 25 Kwa maana mwenye kitu atapewa, naye asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa. Mfano wa mbegu inayokua 26 Akasema, Ufalme wa Mungu, mfano wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi; 27 akawa akilala na kuondoka, usiku na mchana, nayo mbegu ikamea na kukua, asivyojua yeye. 28 Maana nchi huzaa yenyewe; kwanza jani, tena suke, kisha ngano pevu katika suke. 29 Hata matunda yakiiva, mara atapeleka mundu, kwa kuwa mavuno yamefika. Mfano wa punje ya haradali 30 Akasema, Tuulinganishe na nini ufalme wa Mungu? Au tuutie katika mfano gani? 31 Ni kama punje ya haradali, ambayo ipandwapo katika nchi, ingawa ni ndogo kuliko mbegu zote zilizo katika nchi, 32 lakini ikiisha kupandwa hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi makubwa; hata ndege wa angani waweza kukaa chini ya uvuli wake. Matumizi ya mifano 33 Kwa mifano mingi ya namna hii alikuwa akisema nao neno lake, kwa kadiri walivyoweza kulisikia; 34 wala pasipo mfano hakusema nao; lakini akawaeleza wanafunzi wake mwenyewe mambo yote kwa faragha. Yesu atuliza dhoruba 35 Siku hiyo kulipokuwa jioni, Yesu akawaambia, Na tuvuke mpaka ng'ambo. 36 Wakauacha mkutano, wakamchukua vile vile alivyokuwa katika mashua. Na mashua zingine zilikuwako pamoja naye. 37 Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakaipiga mashua hata ikaanza kujaa maji. 38 Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia? 39 Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu. 40 Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado? 41 Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii? |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya