Luka 14 - Swahili Revised Union VersionYesu amponya mtu mwenye ugonjwa wa safura 1 Ikawa alipoingia ndani ya nyumba ya mtu mmoja miongoni mwa wakuu wa Mafarisayo siku ya sabato, ale chakula, walikuwa wakimvizia. 2 Na tazama, mbele yake palikuwa na mtu mwenye ugonjwa wa safura. 3 Yesu akajibu, akawaambia wanasheria na Mafarisayo, Je! Ni halali kuponya siku ya sabato, ama sivyo? 4 Wao wakanyamaza. Akamshika, akamponya, akamruhusu aende zake. 5 Akawaambia, Ni nani miongoni mwenu, ikiwa ng'ombe wake au punda wake ametumbukia kisimani, asiyemwopoa mara hiyo siku ya sabato? 6 Nao hawakuweza kujibu maneno haya. Unyenyekevu na ukarimu 7 Akawaambia mfano wale walioalikwa, alipoona jinsi walivyochagua viti vya mbele; akisema, 8 Ukialikwa na mtu arusini, usiketi katika kiti cha mbele; isiwe kwamba amealikwa mtu mwenye kustahiwa kuliko wewe, 9 akaja yule aliyewaalika wewe na yeye, na kukuambia, Mpishe huyu! Ndipo utakapoanza kwa haya kushika mahali pa nyuma. 10 Bali ukialikwa, nenda ukaketi mahali pa nyuma, ili ajapo yule aliyekualika akuambie, Rafiki yangu, njoo huku mbele zaidi; ndipo utakapokuwa na utukufu mbele ya wote walioketi pamoja nawe. 11 Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa. 12 Akamwambia na yule aliyemwalika, Ufanyapo chakula cha mchana au cha jioni, usiwaite rafiki zako, wala ndugu zako, wala jamaa zako, wala jirani zako wenye mali; wao wasije wakakualika nawe ukapata malipo. 13 Bali ufanyapo karamu waite maskini, vilema, viwete, vipofu, 14 nawe utakuwa heri, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa; kwa maana utalipwa katika ufufuo wa wenye haki. Mfano wa karamu kuu 15 Basi aliposikia hayo mmojawapo wa wale walioketi chakulani pamoja naye alimwambia, Heri yule atakayekula mkate katika ufalme wa Mungu. 16 Akamwambia, Mtu mmoja alifanya karamu kubwa akaalika watu wengi, 17 akamtuma mtumwa wake saa ya chakula awaambie wale walioalikwa, Njooni, kwa kuwa vitu vyote vimekwisha kuwekwa tayari. 18 Wakaanza wote kutoa udhuru kwa nia moja. Wa kwanza alimwambia, Nimenunua shamba, sharti niende nikalitazame; tafadhali unisamehe. 19 Mwingine akasema, Nimenunua ng'ombe jozi tano, ninakwenda kuwajaribu; tafadhali unisamehe. 20 Mwingine akasema, Nimeoa mke, na kwa sababu hiyo siwezi kuja. 21 Yule mtumwa akaenda, akamwambia Bwana wake kuhusu mambo hayo. Basi, yule mwenye nyumba akakasirika, akamwambia mtumwa wake, Toka upesi, uende katika njia kuu na vichochoro vya mji, ukawalete hapa maskini, na vilema, na vipofu, na viwete. 22 Mtumwa akasema, Bwana, hayo uliyoagiza yamekwisha tendeka, na hata sasa ingaliko nafasi. 23 Bwana akamwambia mtumwa, Toka nje uende barabarani na mipakani, ukawashurutishe kuingia ndani, nyumba yangu ipate kujaa. 24 Maana nawaambia ya kwamba katika wale walioalikwa, hakuna hata mmoja atakayeionja karamu yangu. Gharama ya uanafunzi 25 Makutano mengi walipokuwa wakifuatana naye, aligeuka, akawaambia, 26 Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake wa kiume na wa kike; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. 27 Mtu yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. 28 Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, haketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia? 29 Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, 30 wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza. 31 Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, haketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini? 32 Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule akiwa bado mbali. 33 Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Kuhusu chumvi 34 Chumvi ni kitu chema; lakini chumvi ikiwa imeharibika, itiwe nini ikolee? 35 Haiifai nchi wala jaa; watu huitupa nje. Mwenye masikio ya kusikia, na asikie. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya