Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Walawi 13 - Swahili Revised Union Version


Aina za ukoma na dalili zake

1 Kisha BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,

2 Mtu atakapokuwa na uvimbe katika ngozi ya mwili wake, au upele, au kipaku king'aacho, nao ukawa ni ugonjwa wa ukoma katika ngozi ya mwili wake, ndipo atakapoletwa kwa Haruni kuhani, au kwa mmojawapo wa wanawe makuhani;

3 na huyo kuhani ataliangalia hilo pigo lililo katika ngozi ya mwili; na nywele zilizoko katika hilo pigo zimegeuka kuwa nyeupe, na hilo pigo kuonekana kwake limeingia ndani kuliko ile ngozi ya mwili wake, ni pigo la ukoma hilo; na ikiwa nywele zilizoko katika sehemu zilizougua zimegeuka rangi na kuwa nyeupe, na hilo pigo kuonekana limeingia ndani kuliko ile ngozi ya mwili, hilo ni pigo la ukoma,

4 Lakini ikiwa kipaku king'aacho katika ngozi ya mwili wake ni cheupe, na kuonekana si shimo la kuingia ndani kuliko ngozi wala nywele hazikugeuka kuwa nyeupe, ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba huyo aliye na hilo pigo;

5 kisha kuhani atamwangalia siku ya saba; naye akiona ya kuwa pigo limezuilika, na halikuenea katika ngozi yake, ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba tena;

6 kisha siku ya saba kuhani atamwangalia tena; ikiwa hilo pigo limeanza kufifia, wala pigo halikuwa katika ngozi yake ndipo kuhani atasema kuwa ni mzima, ni kipele tu; naye atazifua nguo zake, kisha atakuwa ni safi.

7 Lakini ikiwa kipele kimeenea katika ngozi yake baada ya kujionesha kwa kuhani ili kutakaswa, atamwendea kuhani tena;

8 naye kuhani ataangalia, ikiwa huo upele umeenea katika ngozi, ndipo kuhani atasema kuwa ni najisi; ni ukoma.

9 Mtu atakapopatwa na ugonjwa wa ukoma, ndipo ataletwa kwa kuhani;

10 naye kuhani ataangalia, ikiwa pana uvimbe mweupe katika ngozi yake, na mnywele zimegeuzwa kuwa nyeupe, tena ikiwa panafanyika kidonda katika ule uvimbe,

11 ni ukoma usiopona ulio katika ngozi ya mwili wake, na kuhani atasema kuwa ni najisi; hatamweka mahali, kwa kuwa yeye ana unajisi.

12 Huo ukoma ukitokeza katika ngozi ya mgonjwa, na ukaenea katika ngozi yake yote, kutoka kichwani hadi miguuni, kama kuhani atakavyoweza kuona,

13 ndipo huyo kuhani ataangalia; ikiwa ukoma umemwenea mwili wake wote, atasema kuwa ni safi huyo aliye na hilo pigo, ikiwa ngozi yake yote imegeuka kuwa nyeupe, naye akawa safi.

14 Lakini popote kitakapoonekana kidonda kibichi kwake mtu huyo, atakuwa yu najisi.

15 Kuhani atakiangalia hicho kidonda kibichi, naye atasema kuwa ni najisi; kile kidonda kibichi ni najisi; ni ukoma.

16 Au kama hicho kidonda kibichi kinageuka tena na kuwa cheupe, ndipo atamwendea kuhani,

17 na huyo kuhani atamwangalia; ikiwa hilo pigo limegeuzwa kuwa jeupe, ndipo huyo kuhani atasema kuwa huyo aliyekuwa na pigo ni safi.

18 Tena mwili wa mtu utakapokuwa na jipu katika ngozi yake, nalo limepoa,

19 na mahali palipokuwa na lile jipu pana uvimbe mweupe, au kipaku king'aacho, cheupe lakini chekundu kidogo, ndipo atamwonesha kuhani mahali hapo;

20 na kuhani ataangalia, kama kutaonekana kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe, na malaika yakiwa yamegeuka kuwa meupe, ndipo kuhani atasema kwamba ni najisi; ni pigo la ukoma limetokea katika hilo jipu.

21 Lakini kuhani akipaangalia, na iwe hamna nywele nyeupe ndani yake, wala hapakuingia ndani kuliko ile ngozi, lakini paanza kufifia, ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba;

22 na kwamba pameenea katika ngozi, ndipo kuhani atasema kwamba ni najisi; hili ni pigo.

23 Lakini ikiwa kipaku hicho king'aacho kimekaa pale pale, wala hakienei, ni kovu ya jipu; na kuhani atasema kwamba yu safi.

24 Au mwili wa mtu ukiwa una mahali palipoungua katika ngozi yake, kisha pakawa kidonda, kikawa kipaku chekundu kidogo, au cheupe;

25 ndipo kuhani atapaangalia; ikiwa nywele iliyo katika kile kipaku imegeuka kuwa nyeupe, na kwamba kumeonekana kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe; ni ukoma, umetokea katika mahali palipoungua; na kuhani atasema kuwa ni najisi; hili ni pigo la ukoma.

26 Lakini kuhani akipaangalia, nywele nyeupe hamna katika hicho kipaku king'aacho, nacho hakikuingia ndani kuliko ngozi, lakini chafifia; ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba;

27 na kuhani atamwangalia siku ya saba; kama kimeenea katika ngozi, ndipo huyo kuhani atasema kuwa ni najisi; hili ni pigo la ukoma.

28 Na kama hicho kipaku kikibaki pale pale, wala hakikuenea katika ngozi, lakini kimefifia; ni kufura kwake pale penye moto, na kuhani atasema kuwa ni safi; kwa kuwa ni kovu la kuwasha hili.

29 Mwanamume au mwanamke atakapopatwa na maradhi kichani au kidevuni,

30 ndipo kuhani ataliangalia hilo pigo; ikiwa pigo limeingia ndani kuliko ngozi yenyewe, na nywele zilizomo kuwa za rangi ya manjano na nyembamba, ndipo kuhani atasema kwamba ni najisi, maana ni kipwepwe, ni ukoma wa kichwa au wa kindevu.

31 Tena kuhani akiliangalia lile pigo la kipwepwe, ikiwa kumeonekana si kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe, wala hamna nywele nyeusi ndani yake, ndipo kuhani atamweka mahali huyo aliye na pigo la kipwepwe muda wa siku saba;

32 na siku ya saba kuhani ataliangalia hilo pigo; na ikiwa hicho kipwepwe hakikuenea, wala hamna nywele za rangi ya manjano ndani yake, na kwamba kipwepwe hakionekani kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe,

33 ndipo huyo mtu atanyolewa, lakini hicho kipwepwe hatakinyoa; na kuhani atamweka mahali huyo aliye na kipwepwe muda wa siku saba tena;

34 na siku ya saba kuhani atakiangalia hicho kipwepwe, ikiwa kipwepwe hakikuenea katika ngozi yake, wala hakionekani kuingia ndani kuliko ngozi; ndipo huyo kuhani atasema kwamba ni safi; naye atazifua nguo zake, naye atakuwa ni safi.

35 Lakini hicho kipwepwe kama kikienea katika ngozi yake baada ya kutakasika kwake;

36 ndipo kuhani atamwangalia; na ikiwa hicho kipwepwe kimeenea katika ngozi yake, kuhani hatatafuta hizo nywele za rangi ya manjano; yeye ni najisi.

37 Lakini akiona ya kuwa hicho kipwepwe kimepungua, na nywele nyeusi zimemea humo; hicho kipwepwe kimepoa, naye yu safi, na huyo kuhani atasema kwamba yu safi.

38 Mwanamume au mwanamke, atakapokuwa na vipaku ving'aavyo katika ngozi ya mwili, vipaku ving'aavyo vyeupe;

39 ndipo kuhani ataangalia; ikiwa vile vipaku ving'aavyo vilivyo katika ngozi ya mwili wake ni vyeupe kidogo; ni mba iliyotokeza katika ngozi; yeye ni safi.

40 Kwamba nywele za mtu zimemtoka kichwani mwake, yeye ni mwenye upara, ni safi.

41 Tena kwamba nywele za mtu zimemtoka kichwani upande wa mbele, yeye ni mwenye upara wa kipaji; ni safi.

42 Lakini kwamba katika kile kichwa kilicho na upara, au kile kipaji kilicho na upara, laonekana pigo jeupe kisha jekundu kidogo; ni ukoma, unatokea katika kichwa chake cha upara, au katika kipaji chake cha upara.

43 Ndipo kuhani atamwangalia; kivimbe cha pigo kikiwa cheupe na chekundu chekundu, katika kichwa chake chenye upara, au katika kipaji chake cha upara, kama vile kuonekana kwa ukoma katika ngozi ya mwili;

44 yeye ni mtu mwenye ukoma, ni najisi; na kuhani hana budi atasema kuwa ni najisi; pigo lake liko katika kichwa chake.

45 Mtu mwenye ukoma aliye na pigo ndani yake, atavaa nguo zilizoraruka, na nywele timutimu; na ataufunika mdomo wake wa juu na kusema, “Ni najisi, ni najisi”.

46 Kwa siku zote ambazo pigo litakuwa ndani yake atakuwa najisi, ataishi kwa upweke katika makazi yake, nje ya kambi.

47 Kuhusu mavazi; vazi ambalo pigo la ukoma limo ndani yake, liwe ni vazi la sufu au la katani;

48 likiwa limefumwa, au kusokotwa; likiwa ni la kitani au la sufu; liwe katika ngozi, au kitu chochote kilichofanywa cha ngozi;

49 hilo pigo likiwa la rangi ya kijani au jekundu, katika vazi, au katika ngozi, au katika lililofumwa, au katika lililosokotwa, au katika kitu chochote cha ngozi; ni pigo la ukoma, nalo ataoneshwa kuhani;

50 na kuhani ataliangalia hilo pigo, naye atakiweka mahali kile kilicho na pigo muda wa siku saba;

51 kisha siku ya saba ataliangalia hilo pigo; kama pigo limeenea katika hilo lililofumwa, au katika hilo lililosokotwa, au katika ngozi, ijapokuwa hiyo ngozi ina matumizi yoyote; hilo pigo ni ukoma unaona; vazi hilo ni najisi.

52 Naye ataliteketeza vazi hilo, liwe ni la kufumwa au ni la kusokotwa, kama ni la sufu, au la kitani, au kitu chochote cha ngozi, ambacho kina hilo pigo ndani yake; kwa maana, ni ukoma unaona; vazi hilo litateketezwa;

53 Na kama kuhani akitazama, ikiwa hilo pigo halikuenea katika hilo vazi, wala katika hilo lililofumwa, wala katika hilo lililosokotwa, wala katika kitu chochote cha ngozi;

54 ndipo kuhani ataamuru kwamba wakifue kitu kile kilicho na hilo pigo, naye atakiweka mahali muda wa siku saba tena;

55 kisha kuhani ataangalia, baada ya kuoshwa hilo pigo; ikiwa hilo pigo halikugeuka rangi yake, wala halikuenea, ni najisi; utaliteketeza; ni uharibifu likiwa lina doa ndani au nje.

56 Huyo kuhani ataangalia, ikiwa hilo pigo limeanza kufifia, baada ya kufuliwa kwake, ndipo atalirarua hilo pigo litoke katika vazi, au katika ngozi, au katika lililofumwa, au katika lililosokotwa;

57 kisha, likionekana liko vile vile katika hilo vazi, katika lililofumwa, au katika lililosokotwa, au katika kitu chochote cha ngozi, ni pigo lenye kuenea; nawe vazi hilo lenye pigo utaliteketeza.

58 Na hilo vazi, lililofumwa, au lililosokotwa, au kitu chochote cha ngozi, utakalolifua, kama hilo pigo limetoka na kuliacha, ndipo litafuliwa mara ya pili, nalo litakuwa safi.

59 Na katika pigo la ukoma katika vazi la sufu, au la kitani, kama ni katika lililofumwa, au lililosokotwa, au katika kitu chochote cha ngozi, sheria yake ni hiyo, kusema kwamba ni safi, au kusema kwamba ni najisi.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo