Maombolezo 5 - Swahili Revised Union VersionOmbi la kuhurumiwa 1 Ee BWANA, kumbuka yaliyotupata; Utazame na kuiona aibu yetu. 2 Urithi wetu umegeuka kuwa mali ya wageni; Na nyumba zetu kuwa mali ya mataifa. 3 Tumekuwa yatima waliofiwa na baba; Mama zetu wamekuwa kama wajane. 4 Tumekunywa maji yetu kwa fedha; Kuni zetu twauziwa. 5 Watufuatiao wako juu ya shingo zetu; Tumechoka, tusipate pumziko lolote. 6 Tumewapa hao Wamisri mkono; Na Waashuri nao, ili tushibe chakula. 7 Baba zetu walitenda dhambi hata hawako; Na sisi tumeyachukua maovu yao. 8 Watumwa wanatutawala; Hakuna mtu wa kutuokoa na mikono yao. 9 Twapata chakula kwa kujihatarisha nafsi zetu; Kwa sababu ya upanga wa nyikani. 10 Ngozi yetu ni nyeusi kama tanuri; Kwa sababu ya joto ya njaa ituteketezayo. 11 Wanawake katika Sayuni wanashikwa kwa nguvu; Na mabikira katika miji ya Yuda. 12 Wakuu hutundikwa kwa mikono yao; Nyuso za wazee hazipewi heshima. 13 Vijana huyachukua mawe ya kusagia; Na watoto hujikwaa chini ya kuni. 14 Wazee wameacha kwenda langoni; Na vijana kwenda ngomani. 15 Furaha ya mioyo yetu imekoma; Machezo yetu yamegeuka maombolezo. 16 Taji ya kichwa chetu imeanguka; Ole wetu! Kwa kuwa tumetenda dhambi. 17 Kwa sababu hiyo mioyo yetu imezimia; Kwa ajili ya hayo macho yetu hayaoni vema. 18 Kwa ajili ya mlima Sayuni ulio ukiwa, Mbweha hutembea juu yake. 19 Wewe, BWANA, unadumu milele; Kiti chako cha enzi ni tangu kizazi hata kizazi. 20 Mbona watusahau sikuzote; Na kutuacha muda huu mwingi? 21 Ee BWANA, utugeuze kwako, nasi tutageuka; Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale. 22 Ingawa wewe umetukataa kabisa; Nawe una hasira nyingi sana juu yetu. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya