Miungu yao ni ya fedha na dhahabu; imetengenezwa kwa mikono ya wanadamu.
Ina vinywa, lakini haisemi. Ina macho, lakini haioni.
Ina masikio, lakini haisikii. Ina pua, lakini hainusi.
Ina mikono, lakini haipapasi. Ina miguu, lakini haitembei. Haiwezi kamwe kutoa sauti.
Wote wanaoitengeneza wanafanana nayo, kadhalika na wote wanaoitumainia.
Enyi watu, mtumainieni Mungu daima; mfungulieni Bwana yaliyo moyoni mwenu. Mungu ndiye kimbilio la usalama wetu.
Hujitwisha sanamu hiyo mabegani, wakaibeba, kisha huiweka mahali pake, ikakaa papo hapo; kamwe haiwezi hata kusogea kutoka hapo ilipo. Mtu akiililia, haiwezi kumwitikia, wala haiwezi kumwokoa mtu katika taabu zake.
Lakini Mwenyezi-Mungu ni Mungu wa kweli; Mungu aliye hai, mfalme wa milele. Akikasirika, dunia hutetemeka, mataifa hayawezi kustahimili hasira yake.
Mtumaini Mwenyezi-Mungu kwa moyo wako wote, wala usitegemee akili zako mwenyewe.
Umtambue Mungu katika kila ufanyalo, naye atazinyosha njia zako.
Jina langu mimi ni Mwenyezi-Mungu; utukufu wangu sitampa mwingine, wala sifa zangu sanamu za miungu.
Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Alaaniwe mtu anayemtegemea binadamu, mtu ambaye anategemea nguvu za binadamu, mtu ambaye moyo wake umeniacha mimi Mwenyezi-Mungu.
Vinyago vyao ni kama vinyago vya kutishia ndege katika shamba la matango, havina uwezo wa kuongea; ni lazima vibebwe maana haviwezi kutembea. Msiviogope vinyago hivyo, maana haviwezi kudhuru, wala haviwezi kutenda lolote jema.”
Heri mtu anayesaidiwa na Mungu wa Yakobo, mtu aliyeweka tumaini lake kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wake,
aliyeumba mbingu na dunia, bahari na vyote vilivyomo. Yeye hushika ahadi yake milele.
“Chafaa nini kinyago alichotengeneza mtu? Sanamu ni madini yaliyoyeyushwa, ni kitu cha kueneza udanganyifu! Mtengeneza sanamu hutumaini alichotengeneza mwenyewe, kinyago ambacho hakiwezi hata kusema!
Heri mtu anayemtumainia Mwenyezi-Mungu; mtu asiyejiunga na watu wenye majivuno, watu waliopotoka kwa kuabudu miungu ya uongo.
Basi, na tukikaribie bila hofu kiti cha enzi cha Mungu mwenye neema, tupokee huruma na neema ya kutusaidia wakati wa shida.
Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ndimi ninayetegemeza mkono wako. Mimi ndimi ninayekuambia: ‘Usiogope, nitakusaidia.’”
Kutokana na hayo, tuseme nini zaidi? Ikiwa Mungu yuko upande wetu, nani awezaye kutupinga?
Maana, kweli nitakuokoa na hutauawa vitani; utapata faida ya kuokoa maisha yako kwa sababu umeniamini mimi. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Ee Mwenyezi-Mungu, kwako naielekeza nafsi yangu!
Mwenyezi-Mungu hutenda kwa fadhili na uaminifu, kwa wale wanaoshika agano lake na maamuzi yake.
Kwa ajili ya jina lako, ee Mwenyezi-Mungu, unisamehe kosa langu kwani ni kubwa.
Kila mtu anayemcha Mwenyezi-Mungu, Mwenyezi-Mungu atamfunza njia ya kufuata.
Mtu wa namna hiyo atafanikiwa daima, na wazawa wake watamiliki nchi.
Mwenyezi-Mungu ni rafiki ya wale wamchao; yeye huwajulisha hao agano lake.
Namwangalia Mwenyezi-Mungu daima; yeye atainasua miguu yangu mtegoni.
Unielekee, ee Mungu, unionee huruma, maana mimi ni mpweke na mnyonge.
Uniondolee mahangaiko ya moyoni mwangu; unitoe katika mashaka yangu.
Uangalie mateso yangu na dhiki yangu; unisamehe dhambi zangu zote.
Angalia jinsi walivyo wengi maadui zangu; ona jinsi wanavyonichukia kwa ukatili.
Nakutumainia wewe, ee Mungu wangu, usiniache niaibike; adui zangu wasifurahie kushindwa kwangu.
Basi, Mungu aliye msingi wa matumaini, awajazeni furaha yote na amani kutokana na imani yenu; tumaini lenu lipate kuongezeka kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.
Mtakapolia kuomba msaada, rundo la vinyago vyenu na liwaokoe! Upepo utavipeperushia mbali; naam, pumzi itavitupilia mbali. Lakini watakaokimbilia usalama kwangu, wataimiliki nchi, mlima wangu mtakatifu utakuwa mali yao.”
Wamisri ni binadamu tu wala si Mungu; farasi wao nao ni wanyama tu, si roho. Mwenyezi-Mungu akiunyosha mkono wake, taifa linalotoa msaada litajikwaa, na lile linalosaidiwa litaanguka; yote mawili yataangamia pamoja.
Lakini wote wanaomtumainia Mwenyezi-Mungu, watapata nguvu mpya. Watapanda juu kwa mabawa kama tai; watakimbia bila kuchoka; watatembea bila kulegea.
Nani kati yenu amchaye Mwenyezi-Mungu? Nani anayetii maneno ya mtumishi wake? Kama yupo atembeaye gizani bila taa, amtumainie Mwenyezi-Mungu, na kumtegemea Mungu wake.
Tunaweza kusema hayo kwa sababu ya tumaini letu tulilo nalo kwa Mungu kwa njia ya Kristo.
Si kwamba sisi tunaweza kufanya chochote kwa nguvu zetu wenyewe, ila uwezo wetu wote hutoka kwa Mungu:
Najua Mwenyezi-Mungu atamsaidia mfalme aliyemteua, atamjibu kutoka patakatifu pake mbinguni; kwa mkono wake wa kulia atamjalia ushindi mkubwa.
Wengine hujigamba kwa magari ya vita; wengine hujigamba kwa farasi wao. Lakini sisi twajivunia Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.
Mwenyezi-Mungu ni jua letu na ngao yetu; yeye hutuneemesha na kutujalia fahari. Hawanyimi chochote kilicho chema, wale waishio kwa unyofu.
Mtafuteni Mwenyezi-Mungu wakati bado anapatikana, mwombeni msaada wakati yupo bado karibu.
Maana ninajua hakika kwamba hakuna kitu kiwezacho kututenganisha na upendo wake: Wala kifo, wala uhai; wala malaika au nguvu nyingine za mbinguni; wala yanayotokea sasa, wala yatakayotokea baadaye; wala mamlaka;
wala ulimwengu wa juu, wala wa chini kabisa. Hakuna kiumbe chochote kitakachoweza kututenga na upendo wa Mungu katika Kristo Yesu Bwana wetu.
Nimeyafagilia mbali makosa yako kama wingu, nimezifanya dhambi zako zitoweke kama ukungu. Rudi kwangu maana mimi nimekukomboa.”
Palipo na upendo hapana woga; naam, upendo kamili hufukuza woga wote. Basi, mtu mwenye woga hajakamilika bado katika upendo, kwani woga huhusikana na adhabu.
nami nateseka kwa mambo haya kwa sababu hiyo. Lakini niko bado timamu kabisa kwani namjua yule niliyemwamini, tena nina hakika kwamba yeye atakilinda salama kile alichonikabidhi, mpaka siku ile.
Hata nikikosa nguvu mwilini na rohoni, wewe, ee Mungu, u mwamba wangu; riziki yangu kuu ni wewe milele.
Mwenyezi-Mungu huwasaidia na kuwaokoa; huwatoa makuchani mwa waovu na kuwaokoa, maana wanakimbilia usalama kwake.
Ee Mungu, wawaweka katika amani walio thabiti, wawaweka katika amani kwa kuwa wanakutegemea.
Na sisi tuko thabiti mbele ya Mungu kwani tuna hakika kwamba tukimwomba chochote kadiri ya matakwa yake, yeye hutusikiliza.
Basi, nina hakika kwamba Mungu aliyeanza kazi hii njema ndani yenu, ataiendeleza mpaka ikamilike katika siku ile ya Kristo Yesu.
Basi, usiogope, mimi nipo pamoja nawe. Usifadhaike, mimi ni Mungu wako. Nitakuimarisha na kukusaidia; nitakulinda kwa mkono wangu wa ushindi.
Mungu ndiye mwenye kuniokoa, nitamtegemea yeye, wala sitaogopa; Mwenyezi-Mungu hunijalia nguvu; yeye mwenyewe ndiye aniokoaye.”
Mwenyezi-Mungu ni mwema, yeye ni ngome ya usalama wakati wa taabu. Yeye huwalinda wote wanaokimbilia usalama kwake.
Bwana Mungu, Mtakatifu wa Israeli, asema: “Mkinirudia na kutulia mtaokolewa; kwa utulivu na kunitumainia mtapata nguvu.” Lakini nyinyi hamkutaka.
Wanaomtegemea Mwenyezi-Mungu, wako kama mlima Siyoni, ambao hautikisiki bali wabaki imara daima.
Ole wao wale waendao Misri kuomba msaada, ole wao wanaotegemea farasi, wanaotegemea wingi wa magari yao ya vita, na nguvu za askari wao wapandafarasi, nao hawamtegemei Mtakatifu wa Israeli, wala hawamwombi Mwenyezi-Mungu shauri!
Anachofanya Mungu hakina dosari! Ahadi ya Mwenyezi-Mungu ni ya kuaminika; yeye ni ngao kwa wote wanaomkimbilia.
“Mimi ni Mwenyezi-Mungu, wala hakuna mwingine; hakuna Mungu mwingine ila mimi. Ninakuimarisha ingawa wewe hunijui,
Namtumainia Mungu na kusifu neno lake; namtumainia Mungu, wala siogopi. Binadamu dhaifu atanifanya nini?
Mwenyezi-Mungu ni mwanga wangu na wokovu wangu, ni nani nitakayemwogopa? Mwenyezi-Mungu ni ngome ya maisha yangu, sitamwogopa mtu yeyote.
Mwenyezi-Mungu, Mfalme na Mkombozi wa Israeli, naam, Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Mimi ni wa kwanza na wa mwisho; hakuna Mungu mwingine ila mimi.
ataweza kumwambia Mwenyezi-Mungu: “Wewe ni kimbilio langu na ngome yangu; Mungu wangu, ninayekutumainia!”
Nyinyi mlijaliwa kuyaona mambo hayo, ili mpate kutambua kwamba Mwenyezi-Mungu, ndiye peke yake Mungu na wala hakuna mwingine.
Waamuru watu walio matajiri katika mambo ya maisha ya sasa, wasijivune, wasiweke tumaini lao katika mali isiyoweza kutegemewa; bali wamtegemee Mungu, ambaye kwa ukarimu hutupatia vitu vyote tuvifurahie.
Mkipita katika mafuriko, mimi nitakuwa pamoja nanyi; mkipita katika mito, haitawashinda nguvu. Mkitembea katika moto, hamtaunguzwa; mwali wa moto hautawaunguza.
Hata jeshi likinizunguka, moyo wangu hautaogopa kitu; hata nikikabiliwa na vita, bado nitakuwa na tumaini.
Naam, tulikuwa kama watu waliohukumiwa kuuawa, ili tufundishwe kumtegemea Mungu mwenye kuwafufua wafu, badala ya kutegemea nguvu zetu sisi wenyewe.
Hana haja ya kuogopa akipata habari mbaya; ana moyo thabiti na humtegemea Mwenyezi-Mungu.
Nijapopita katika bonde la giza kuu la kifo, sitaogopa hatari yoyote, maana wewe ee Mwenyezi-Mungu u pamoja nami; gongo lako na fimbo yako vyanilinda.
Ndiyo maana tunathubutu kusema: “Bwana ndiye msaada wangu, sitaogopa. Binadamu atanifanya nini?”
Yeye ni rafiki yangu amini na ngome yangu, kinga yangu na mkombozi wangu; yeye ni ngao yangu, kwake napata usalama; huyashinda mataifa na kuyaweka chini yangu.
Nigeukieni mimi mpate kuokolewa, popote mlipo duniani. Maana mimi ni Mungu, wala hakuna mwingine.
Mwenyezi-Mungu ndiye nguvu yangu na ngao yangu; tegemeo la moyo wangu limo kwake. Amenisaidia nami nikashangilia kwa moyo; kwa wimbo wangu ninamshukuru.
“Usiwe na miungu mingine ila mimi.
“Usijifanyie sanamu ya miungu wa uongo, au kinyago cha chochote kilicho mbinguni, katika nchi au majini chini ya dunia.