Ni ngumu sana kujua ya kwamba hutamwona tena yule umpendaye, aliyetangulia mbele ya haki. Yule ambaye mlikuwa mkishiriki mambo mengi, mkicheka, mkihusiana… Moyo unauma sana. Sote hupitia wakati wa huzuni, majonzi. Wakati kama huu ni sawa kulia, kuhisi uchungu. Hakuna ubaya wowote. Hata Yesu alilia aliposikia kwamba rafiki yake Lazaro amefariki (Yohana 11:35). Ni muhimu sana kuonyesha hisia zako wakati wa huzuni. Lakini licha ya yote haya, tusikubali majonzi yatutawale. Mungu yuko nawe, atafuta machozi yako, atakutia moyo, na atarudisha tabasamu kwenye uso wako. Mruhusu tu Mungu afanye kazi yake. (2 Wakorintho 1:3) Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa faraja yote.
Nimewaambieni mambo haya ili mpate kuwa na amani katika kuungana nami. Ulimwenguni mtapata masumbuko; lakini jipeni moyo! Mimi nimeushinda ulimwengu!”
Mwenyezi-Mungu ni mwema, yeye ni ngome ya usalama wakati wa taabu. Yeye huwalinda wote wanaokimbilia usalama kwake.
Asema: “Nyamazeni na kujua kuwa mimi ni Mungu! Mimi natukuka katika mataifa yote; mimi natukuzwa ulimwenguni kote!”
Muwe imara na hodari, wala msiwaogope au kutishwa nao, maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu ndiye anayekwenda pamoja nanyi. Yeye hataacha kuwasaidia na hatawatupa.”
Mkipita katika mafuriko, mimi nitakuwa pamoja nanyi; mkipita katika mito, haitawashinda nguvu. Mkitembea katika moto, hamtaunguzwa; mwali wa moto hautawaunguza.
Maana wewe umekuwa ngome kwa maskini, ngome kwa fukara katika taabu zao. Wewe ni kimbilio wakati wa tufani, kivuli wakati wa joto kali. Kweli pigo la watu wakatili ni kali kama tufani inayopiga ukuta;
Basi, akaamka, akaukemea ule upepo na kuyaamrisha mawimbi ya ziwa, “Kimya! Tulia!” Hapo upepo ukakoma, kukawa shwari kabisa.
Yesu akawaambia, “Mimi ndimi mkate wa uhai. Anayekuja kwangu hataona njaa; anayeniamini hataona kiu kamwe.
Kumbuka kuwa mimi nimekuamuru uwe imara na hodari. Usiogope wala usifadhaike kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, niko pamoja nawe popote uendapo.”
Waadilifu wakimlilia Mwenyezi-Mungu yeye huwasikia, na kuwaokoa katika taabu zao zote. Mwenyezi-Mungu yu karibu na waliokufa moyo; huwaokoa wote waliokata tamaa kabisa. Mateso ya mwadilifu ni mengi, lakini Mwenyezi-Mungu humwokoa kutoka yote. Mimi nitaona fahari juu ya Mwenyezi-Mungu, wanyonge wasikie na kufurahi. Huvilinda viungo vya mwili wake wote, hakuna hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa.
Yesu akawaambia, “Enyi watu wenye imani haba; mbona mnaogopa?” Basi, akainuka, akaukemea upepo na lile ziwa; kukawa shwari kabisa.
Mungu ni kimbilio letu na nguvu yetu; yeye ni msaada wetu daima wakati wa taabu. Asema: “Nyamazeni na kujua kuwa mimi ni Mungu! Mimi natukuka katika mataifa yote; mimi natukuzwa ulimwenguni kote!” Mwenyezi-Mungu wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni kimbilio letu. Kwa hiyo hatutaogopa chochote, dunia ijapoyeyuka na milima kutikisika kutoka baharini; hata kama bahari ikichafuka na kutisha, na milima ikatetemeka kwa machafuko yake.
Basi, Mungu wangu, kwa utajiri wake mkuu kwa njia ya Kristo, atawapeni mahitaji yenu yote.
Daima twapata taabu, lakini hatugandamizwi; twapata mashaka, lakini hatukati tamaa; twateseka, lakini hatuachwi bila msaada; na ingawa tumeangushwa chini, hatukuangamizwa.
Tunajua kwamba, katika mambo yote, Mungu hufanya kazi na kuifanikisha pamoja na wote wampendao, yaani wale aliowaita kadiri ya kusudi lake.
Ninakulilia kutoka miisho ya dunia, nikiwa nimevunjika moyo. Uniongoze juu kwenye mwamba mkubwa
Mtumaini Mwenyezi-Mungu kwa moyo wako wote, wala usitegemee akili zako mwenyewe. Umtambue Mungu katika kila ufanyalo, naye atazinyosha njia zako.
Basi, usiogope, mimi nipo pamoja nawe. Usifadhaike, mimi ni Mungu wako. Nitakuimarisha na kukusaidia; nitakulinda kwa mkono wangu wa ushindi.
Ndugu zangu, muwe na furaha mnapopatwa na majaribu mbalimbali, Mwenye hasira hawezi kutimiza matakwa ya Mungu yaliyo ya haki. Kwa hiyo, tupilieni mbali mwenendo mchafu na tabia zote mbovu; jiwekeni chini ya Mungu na kupokea lile neno lililopandwa mioyoni mwenu, ambalo laweza kuziokoa nafsi zenu. Msijidanganye wenyewe kwa kusikiliza tu neno lake, bali litekelezeni kwa vitendo. Yeyote anayesikiliza hilo neno lakini halitekelezi, huyo ni kama mtu anayejiangalia sura yake mwenyewe katika kioo. Hujiangalia mwenyewe, kisha huenda zake, na mara husahau jinsi alivyo. Lakini mtu anayeangalia kwa makini sheria kamilifu ambayo huwapa watu uhuru, mtu anayeendelea kuizingatia, na si kuisikia tu na kuisahau baadaye, bali anaitekeleza, mtu huyo atabarikiwa katika kila kitu anachofanya. Kama mtu akijiona kuwa ni mtu mwenye dini, lakini hawezi kuutawala ulimi wake, dini yake haifai kitu, na anajidanganya mwenyewe. Dini iliyo safi na isiyo na hitilafu mbele ya Mungu Baba ni hii: Kuwasaidia yatima na wajane katika shida zao, na kujilinda mwenyewe usichafuliwe na ulimwengu huu. kwani mwajua kwamba imani yenu ikisha stahimili, itawapatieni uvumilivu. Muwe na hakika kwamba uvumilivu wenu utawategemeza mpaka mwisho, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu, bila kupungukiwa chochote.
Lakini alipouona ule upepo, aliogopa, akaanza kuzama; akalia kwa sauti, “Bwana, niokoe!”
Unielekee, ee Mungu, unionee huruma, maana mimi ni mpweke na mnyonge. Uniondolee mahangaiko ya moyoni mwangu; unitoe katika mashaka yangu.
Anayekaa chini ya ulinzi wa Mungu Mkuu, anayeishi chini ya kivuli cha Mungu Mwenye Nguvu, Kwa hiyo, hutapatwa na maafa yoyote; nyumba yako haitakaribiwa na baa lolote. Maana Mungu atawaamuru malaika zake, wakulinde popote uendapo. Watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa kwenye jiwe. Utakanyaga simba na nyoka, utawaponda wana simba na majoka. Mungu asema: “Nitamwokoa yule anipendaye; nitamlinda anayenitambua! Akiniita, mimi nitamwitikia; akiwa taabuni nitakuwa naye; nitamwokoa na kumpa heshima. Nitamridhisha kwa maisha marefu, nitamjalia wokovu wangu.” ataweza kumwambia Mwenyezi-Mungu: “Wewe ni kimbilio langu na ngome yangu; Mungu wangu, ninayekutumainia!”
Sisi tunalo kundi hili kubwa la mashahidi mbele yetu. Kwa hiyo tuondoe kila kizuizi kinachotuzuia, na dhambi ile inayotungangania. Tupige mbio kwa uvumilivu katika mashindano yaliyowekwa mbele yetu. Wazazi wetu hapa duniani walituadhibu kwa muda, kama wao wenyewe walivyoona kuwa vema; lakini Mungu anatuadhibu kwa ajili ya faida yetu wenyewe, tupate kuushiriki utakatifu wake. Kuadhibiwa si jambo la kufurahisha bali la kuhuzunisha. Lakini wale waliofunzwa kuwa na nidhamu mwishowe watavuna tuzo la amani kutoka katika maisha adili. Basi, inueni mikono yenu inayolegea na kuimarisha magoti yenu yaliyo dhaifu. Endeleeni kutembea katika njia iliyonyoka, ili kile kilicholemaa kisiumizwe, bali kiponywe. Jitahidini kuishi kwa amani na watu wote. Ishini maisha ya utakatifu, kwa sababu hakuna mtu atakayemwona Bwana bila ya maisha kama hayo. Jitahidini sana mtu yeyote asije akapoteza neema ya Mungu. Muwe waangalifu ili mti mchungu usizuke kati yenu na kuwaua wengi kwa sumu yake. Jihadharini ili miongoni mwenu pasiwe na mtu mwasherati au mtu asiyemcha Mungu kama Esau, aliyeuza haki yake ya mzaliwa wa kwanza kwa mlo mmoja. Nyinyi mnafahamu kwamba hata alipotaka kuipata tena ile baraka iliyokuwa yake, alikataliwa, maana hakupata tena nafasi ya kutubu, ingawa aliitafuta kwa machozi. Nyinyi hamkuwasili mlimani Sinai, ambao unaweza kushikika kama walivyofanya watu wa Israeli; hamkufika kwenye moto uwakao, penye giza, tufani, mvumo wa tarumbeta na sauti ya maneno. Wale waliosikia sauti hiyo waliomba wasisikie tena neno lingine, Tumwelekee Yesu ambaye ndiye aliyeianzisha imani yetu na ambaye ataikamilisha. Kwa ajili ya furaha iliyokuwa inamngojea, yeye alivumilia kifo msalabani, bila kuijali aibu yake, na sasa anaketi upande wa kulia wa kiti cha enzi cha Mungu.
Katika taabu yangu nilimwomba Mwenyezi-Mungu, naye akanisikia na kuniweka huru. Mwenyezi-Mungu yuko nami, siogopi kitu; binadamu ataweza kunifanya nini?
Ee Mungu, wawaweka katika amani walio thabiti, wawaweka katika amani kwa kuwa wanakutegemea.
Naam, si hayo tu, bali tunafurahi pia katika taabu tukijua kwamba taabu huleta saburi, nayo saburi huleta uthabiti, na uthabiti huleta tumaini. Tumaini hilo haliwezi kutuhadaa, maana Mungu amekwisha mimina mioyoni mwetu upendo wake kwa njia ya Roho Mtakatifu aliyetujalia.
Kwa maana Roho tuliyepewa na Mungu si wa kutufanya tuwe waoga; sivyo, ila ni Roho wa kutujalia upendo na nidhamu.
Natazama juu milimani; msaada wangu utatoka wapi? Msaada wangu watoka kwa Mwenyezi-Mungu, aliyeumba mbingu na dunia.
Majaribu mliyokwisha pata ni ya kawaida kwa binadamu. Mungu ni mwaminifu, naye hataruhusu mjaribiwe kupita nguvu zenu, ila pamoja na majaribu, yeye atawapeni pia nguvu ya kustahimili na njia ya kutoka humo salama.
Hasira yake hudumu kitambo kidogo, wema wake hudumu milele. Kilio chaweza kuwapo hata usiku, lakini asubuhi huja furaha.
Hata nikikumbana na taabu, wewe wanilinda; waunyosha mkono wako dhidi ya hasira ya maadui zangu wakali; kwa nguvu yako kuu wanisalimisha.
Milima yaweza kutoweka, vilima vyaweza kuondolewa, lakini fadhili zangu hazitakuondoka, agano langu la amani halitaondolewa. Mimi Mwenyezi-Mungu nikuhurumiaye nimesema.
Mwenyezi-Mungu ni mwanga wangu na wokovu wangu, ni nani nitakayemwogopa? Mwenyezi-Mungu ni ngome ya maisha yangu, sitamwogopa mtu yeyote.
Njoni kwangu nyinyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jifungeni nira yangu, mkajifunze kwangu, maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtatulizwa rohoni mwenu. wamwulize: “Je, wewe ni yule anayekuja, au tumngoje mwingine?” Maana, nira niwapayo mimi ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”
Tumaini lenu liwaweke daima wenye furaha; muwe na saburi katika shida, na kusali daima.
Lakini akaniambia: “Neema yangu inatosha kwa ajili yako; maana uwezo wangu hukamilishwa zaidi katika udhaifu.” Basi, ni radhi kabisa kujivunia udhaifu wangu ili uwezo wake Kristo ukae juu yangu.
maana mtu mwema huanguka mara nyingi lakini huinuka, lakini mtu mwovu huangamizwa na janga.
Nijapopita katika bonde la giza kuu la kifo, sitaogopa hatari yoyote, maana wewe ee Mwenyezi-Mungu u pamoja nami; gongo lako na fimbo yako vyanilinda.
Msiwe watu wa kupenda fedha; toshekeni na vile vitu mlivyo navyo. Mungu mwenyewe amesema: “Sitakuacha kamwe, wala sitakutupa.”
Yesu akawajibu, “Kwa sababu ya imani yenu haba. Nawaambieni kweli, kama tu mkiwa na imani, iwe ndogo hata kama mbegu ya haradali, mtaweza kuuambia mlima huu: ‘Toka hapa uende pale,’ nao utakwenda. Hakuna chochote ambacho hakingewezekana kwenu. [
Hatimaye, nawatakeni muwe imara katika kuungana na Bwana na kwa msaada wa nguvu yake kuu. Vaeni silaha anazowapeni Mungu mpate kuzipinga mbinu mbaya za Ibilisi.
Maana yeye hapuuzi au kudharau unyonge wa mnyonge; wala hajifichi mbali naye, ila humsikia anapomwomba msaada.
Umetupima, ee Mungu, umetujaribu kama madini motoni. Umetuacha tunaswe wavuni; umetubebesha taabu nzito. Umewaacha watu watukanyage; tumepitia motoni na majini. Lakini sasa umetuleta kwenye usalama.
Furahini kuhusu jambo hilo, ijapokuwa sasa, kwa kitambo kidogo, itawabidi kuhuzunika kwa sababu ya majaribio mbalimbali mnayoteseka, majaribio ambayo shabaha yake ni kuthibitisha imani yenu. Hata dhahabu yenyewe, ambayo huharibika, hujaribiwa kwa moto; hali kadhalika na imani yenu, ambayo ni ya thamani kuliko dhahabu, ni lazima ijaribiwe ipate kuwa thabiti. Hapo mtapokea sifa na utukufu na heshima siku ile Yesu Kristo atakapofunuliwa.
Msiogope maana mimi nipo pamoja nanyi. “Nitawarudisha wazawa wenu toka mashariki, nitawakusanyeni kutoka magharibi.
Atukuzwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba mwenye huruma na Mungu mwenye kuleta faraja yote. Yeye hutufariji sisi katika taabu zetu zote, ili nasi tupate kuwafariji wengine katika kila taabu kwa faraja hiyohiyo tunayopokea kutoka kwa Mungu.
Msiwe na wasiwasi juu ya kitu chochote, ila kwa kila hali, mwombeni Mungu katika sala juu ya mahitaji yenu, kwa shukrani. Nayo amani ya Mungu ipitayo akili zote za watu italinda salama mioyo na akili zenu katika kuungana na Kristo Yesu.
Nilimngojea Mwenyezi-Mungu kwa uvumilivu, akanielekea na kukisikia kilio changu. Sikuuficha moyoni mwangu ukombozi ulionijalia, nimetangaza daima kuwa wewe ni mwokozi mwaminifu; sikulificha kusanyiko kubwa la watu fadhili zako na uaminifu wako. Ee Mwenyezi-Mungu, usininyime huruma yako! Fadhili zako na uaminifu wako vinihifadhi daima. Maafa yasiyohesabika yanizunguka, maovu yangu yanikaba hata siwezi kuona; ni mengi kuliko nywele kichwani mwangu, nami nimevunjika moyo. Upende ee Mwenyezi-Mungu kuniokoa; ee Mwenyezi-Mungu, uje haraka kunisaidia. Wanaonuia kuniangamiza, na waaibike na kufedheheka! Hao wanaotamani niumie, na warudi nyuma na kuaibika! Hao wanaonisimanga, na wapumbazike kwa kushindwa kwao! Lakini wote wale wanaokutafuta wafurahi na kushangilia kwa sababu yako. Wapendao wokovu wako, waseme daima: “Mwenyezi-Mungu ni Mkuu!” Mimi ni maskini na fukara, ee Bwana; lakini ee Bwana wewe wanikumbuka. Ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu; uje, ee Mungu wangu, usikawie! Aliniondoa katika shimo la hatari, alinitoa katika matope ya dimbwi, akanisimamisha salama juu ya mwamba, na kuziimarisha hatua zangu. Alinifundisha wimbo mpya, wimbo wa sifa kwa Mungu wetu. Wengi wataona na kuogopa, na kumtumainia Mwenyezi-Mungu.
“Kwa hiyo, kila mtu anayeyasikia maneno yangu na kuyazingatia, anafanana na mtu mwenye busara, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba. Mvua ikanyesha, mito ikafurika, pepo kali zikavuma na kuipiga nyumba hiyo. Lakini haikuanguka kwa sababu ilikuwa imejengwa juu ya mwamba.
Njoni watu wangu, ingieni majumbani mwenu, mkajifungie humo ndani. Jificheni kwa muda mfupi, mpaka ifike ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu.
Ee Mungu Mkuu, hofu inaponishika, mimi nakutumainia wewe. Namtumainia Mungu na kusifu neno lake; namtumainia Mungu, wala siogopi. Binadamu dhaifu atanifanya nini?
Kutokana na hayo, tuseme nini zaidi? Ikiwa Mungu yuko upande wetu, nani awezaye kutupinga?
Mwenyezi-Mungu ni nguvu yangu kuu; yeye mwenyewe ndiye wokovu wangu. Sauti za furaha ya ushindi zasikika hemani mwao waadilifu: “Mkono wa Mwenyezi-Mungu umetenda mambo makuu! Mkono wa nguvu wa Mwenyezi-Mungu umeleta ushindi! Mkono wa Mwenyezi-Mungu umetenda mambo makuu!”
Hatakuacha uanguke; mlinzi wako hasinzii. Kweli mlinzi wa Israeli hasinzii wala halali.
Kwake Mwenyezi-Mungu nakimbilia usalama; mnawezaje basi kuniambia: “Ruka kama ndege, mpaka milimani,
Lakini Mwenyezi-Mungu asema: “Kwa sababu maskini wanadhulumiwa, na wahitaji wanapiga kite, sasa naja, nami nitawapa usalama wanaoutazamia.”
Toka upeo wa unyonge wangu, nakulilia, ee Mwenyezi-Mungu. Ee Bwana, sikia sauti yangu, uitegee sikio sauti ya ombi langu.
Mwenyezi-Mungu ni mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu. Hunipumzisha kwenye malisho mabichi; huniongoza kando ya maji matulivu, na kuirudishia nafsi yangu nguvu mpya. Huniongoza katika njia sawa kwa hisani yake.
Mwenyezi-Mungu yuko karibu na wote wanaomwomba, wote wanaomwomba kwa moyo mnyofu. Huwapatia mahitaji yao wote wanaomcha; husikia kilio chao na kuwaokoa.
Waambieni waliokufa moyo: “Jipeni moyo, msiogope! Tazameni Mungu wenu atakuja kulipiza kisasi, atakuja kuwaadhibu maadui zenu; atakuja yeye mwenyewe kuwaokoeni.”
Lakini wote wanaomtumainia Mwenyezi-Mungu, watapata nguvu mpya. Watapanda juu kwa mabawa kama tai; watakimbia bila kuchoka; watatembea bila kulegea.
Mwenyezi-Mungu asifiwe siku kwa siku! Yeye hutubebea mizigo yetu; yeye ndiye Mungu wa wokovu wetu.
Wale wanafunzi wakamwendea Yesu, wakamwamsha wakisema, “Bwana, Bwana! Tunaangamia!” Yesu akaamka, akaukemea upepo na mawimbi ya maji, navyo vikatulia, kukawa shwari.
Wapenzi wangu, msishangae kuhusu majaribio makali mnayopata kana kwamba mnapatwa na kitu kisicho cha kawaida. Ila furahini kwamba mnashiriki mateso ya Kristo ili muweze kuwa na furaha tele wakati utukufu wake utakapofunuliwa.
Mwenyezi-Mungu huwaokoa waadilifu, na kuwalinda wakati wa taabu. Uitafute furaha yako kwa Mwenyezi-Mungu, naye atakujalia unayotamani moyoni. Mwenyezi-Mungu huwasaidia na kuwaokoa; huwatoa makuchani mwa waovu na kuwaokoa, maana wanakimbilia usalama kwake.
Basi, na tukikaribie bila hofu kiti cha enzi cha Mungu mwenye neema, tupokee huruma na neema ya kutusaidia wakati wa shida.
Maana Mungu atawaamuru malaika zake, wakulinde popote uendapo. Watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa kwenye jiwe.
Katika siku za fanaka uwe na furaha; katika siku za maafa utafakari jambo hili: Fanaka, pia maafa, Mungu amefanya hiyo ya kwanza iambatane na ya pili ili binadamu asiweze kujua yatakayotukia baada yake.
Wewe ee Mwenyezi-Mungu, waniangazia; walifukuza giza langu, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu. Kwa msaada wako nakishambulia kikosi; wewe wanipa nguvu ya kuruka ukuta.
Mungu aliye msingi wa saburi na faraja yote, awajalieni nyinyi kuwa na msimamo mmoja kufuatana na mfano wake Kristo Yesu, ili nyinyi nyote, kwa nia moja na sauti moja, mumtukuze Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo.
Kila mtu anayetaka kuishi maisha ya kumcha Mungu katika kuungana na Kristo Yesu lazima adhulumiwe.
Bwana Mungu hunisaidia, kwa hiyo siwezi kufadhaika. Uso wangu nimeukaza kama jiwe; najua kwamba sitaaibishwa.
Hata nikikosa nguvu mwilini na rohoni, wewe, ee Mungu, u mwamba wangu; riziki yangu kuu ni wewe milele.
Tuzingatie kabisa tumaini letu tunalokiri, maana Mungu aliyefanya ahadi zake ni mwaminifu.
Lakini mimi ni kama mzeituni mbichi, unaostawi katika nyumba ya Mungu. Nazitegemea fadhili zake milele na milele. Ee Mungu, nitakushukuru daima, kwa ajili ya mambo uliyofanya. Nitatangaza kwamba wewe ni mwema, mbele ya watu wako waaminifu.
Watu wote watawachukieni nyinyi kwa sababu ya jina langu. Lakini, hata unywele mmoja wa vichwa vyenu hautapotea. Kwa uvumilivu wenu, mtayaokoa maisha yenu.
Heri wanaoteswa kwa sababu ya kufanya atakavyo Mungu, maana ufalme wa mbinguni ni wao. “Heri yenu nyinyi watu wakiwatukana, wakiwadhulumu na kuwasingizia kila aina ya uovu kwa ajili yangu. Furahini na kushangilia maana tuzo lenu ni kubwa mbinguni. Hivyo ndivyo walivyowadhulumu manabii waliokuwako kabla yenu.
Msiwaogope wale wauao mwili, lakini hawawezi kuiua roho. Afadhali zaidi kumwogopa yule awezaye kuuangamiza mwili pamoja na roho katika moto wa Jehanamu.
Mwenyezi-Mungu alipoturekebisha na kuturudisha Siyoni, tulikuwa kama watu wanaoota ndoto! Hapo tuliangua kicheko; tulishangilia kwa furaha. Nao watu wa mataifa mengine walisema: “Mwenyezi-Mungu amewatendea mambo makubwa!” Kweli Mwenyezi-Mungu alitutendea mambo makubwa, tulifurahi kwelikweli!
Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ndimi ninayetegemeza mkono wako. Mimi ndimi ninayekuambia: ‘Usiogope, nitakusaidia.’”
Basi, nina hakika kwamba Mungu aliyeanza kazi hii njema ndani yenu, ataiendeleza mpaka ikamilike katika siku ile ya Kristo Yesu.
Mwenyezi-Mungu ndiye nguvu yangu na ngao yangu; tegemeo la moyo wangu limo kwake. Amenisaidia nami nikashangilia kwa moyo; kwa wimbo wangu ninamshukuru.
Fanya haraka, ee Mwenyezi-Mungu! Watu wema wamekwisha; waaminifu wametoweka miongoni mwa watu. Kila mmoja humdanganya mwenzake, husema kwa kudanganya na kwa moyo wa unafiki.
Lakini wafurahi wote wanaokimbilia usalama kwako, waimbe kwa shangwe daima. Uwalinde wanaolipenda jina lako, wapate kushangilia kwa sababu yako.
Ee Mwenyezi-Mungu, wewe umenichunguza; wewe wanijua mpaka ndani. hata huko upo kuniongoza; mkono wako wa kulia utanitegemeza. Kama ningeliomba giza linifunike, giza linizunguke badala ya mwanga, kwako giza si giza hata kidogo, na usiku wangaa kama mchana; kwako giza na mwanga ni mamoja. Wewe umeniumba, mwili wangu wote; ulinitengeneza tumboni mwa mama yangu. Nakusifu maana nimefanywa kwa namna ya ajabu, matendo yako ni ya ajabu; wewe wanijua kabisakabisa. Umbo langu halikufichika kwako nilipotungwa kwa siri na ustadi ndani ya dunia. Wewe uliniona hata kabla sijazaliwa, uliandika kila kitu kitabuni mwako; siku zangu zote ulizipanga, hata kabla ya kuweko ile ya kwanza. Ee Mungu, mawazo yako ni makuu mno; hayawezi kabisa kuhesabika. Ningeyahesabu yangekuwa mengi kuliko mchanga. Niamkapo, bado nipo pamoja nawe. Laiti, ee Mungu, ungewaua watu waovu! Laiti watu wauaji wangeondoka kwangu! Nikiketi au nikisimama, wewe wajua; wajua kutoka mbali kila kitu ninachofikiria. Wanasema vibaya juu yako; wanasema maovu juu ya jina lako! Ee Mwenyezi-Mungu, nawachukia wanaokuchukia; nawadharau sana wale wanaokuasi! Maadui zako ni maadui zangu; ninawachukia kabisakabisa. Unichunguze, ee Mungu, unijue moyo wangu, unipime, uyajue mawazo yangu. Uangalie kama mwenendo wangu ni mbaya, uniongoze katika njia ya milele. Watambua nikienda au nikipumzika; wewe wazijua shughuli zangu zote.
Lakini mkisha teseka muda mfupi, Mungu aliye asili ya neema yote na ambaye anawaiteni kuushiriki utukufu wake wa milele katika kuungana na Kristo, yeye mwenyewe atawakamilisheni na kuwapeni uthabiti, nguvu na msingi imara.
Sisi basi, na tushukuru, kwani tunapokea ufalme usiotikisika. Tuwe na shukrani na kumwabudu Mungu kwa namna itakayompendeza, kwa ibada na hofu;
Basi, chochote mfanyacho iwe ni kula au kunywa, fanyeni yote kwa ajili ya utukufu wa Mungu.
Lakini, katika mambo haya yote, tumepata ushindi mkubwa kwa msaada wake yeye aliyetupenda.
Bwana Mungu, Mtakatifu wa Israeli, asema: “Mkinirudia na kutulia mtaokolewa; kwa utulivu na kunitumainia mtapata nguvu.” Lakini nyinyi hamkutaka.
Kila mara ninapokuomba msaada wako, maadui zangu wanarudishwa nyuma. Najua kweli Mungu yuko upande wangu.
Nani kati yenu amchaye Mwenyezi-Mungu? Nani anayetii maneno ya mtumishi wake? Kama yupo atembeaye gizani bila taa, amtumainie Mwenyezi-Mungu, na kumtegemea Mungu wake.
Taabu tunayopata ni kidogo, tena ya muda tu; lakini itatupatia utukufu upitao matazamio yote, utukufu ambao hauna mwisho.
Basi, nimo mbioni kuelekea lengo langu, ili nipate lile tuzo, ambalo ni mwito wa Mungu kwa maisha ya juu kwa njia ya Kristo Yesu.
Basi, msiwe na wasiwasi juu ya kesho; kesho inayo yake. Matatizo ya siku moja yanawatosheni kwa siku hiyo.
Msiwe watu wa kupenda fedha; toshekeni na vile vitu mlivyo navyo. Mungu mwenyewe amesema: “Sitakuacha kamwe, wala sitakutupa.” Ndiyo maana tunathubutu kusema: “Bwana ndiye msaada wangu, sitaogopa. Binadamu atanifanya nini?”
Naye Mungu aliye chanzo cha amani hatakawia kumponda Shetani chini ya miguu yenu. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi.
Watu waovu watapata mateso mengi, bali wanaomtumainia Mwenyezi-Mungu wazungukwa na fadhili zake. Furahini na kushangilia kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu enyi waadilifu; pigeni vigelegele vya shangwe enyi wanyofu wa moyo.
Ee Mwenyezi-Mungu, alfajiri waisikia sauti yangu, asubuhi nakutolea tambiko yangu, kisha nangojea unijibu.
Namlilia Mungu kwa sauti, kwa sauti namlilia Mungu anisikie. Kisha nikasema, “Kinachonichoma zaidi ni kwamba, Mungu Mkuu hatendi tena kitu kwa ajili yetu!” Nitayakumbuka matendo yako, ee Mwenyezi-Mungu, naam, nitayafikiria maajabu yako ya hapo kale. Nitatafakari juu ya kazi zako, na kuwaza juu ya matendo yako makuu. Kila ufanyacho ee Mungu, ni kitakatifu. Ni mungu gani aliye mkuu kama Mungu wetu? Wewe ni Mungu unayetenda maajabu; wewe umeyaonesha mataifa uwezo wako. Kwa mkono wako wa nguvu uliwakomboa watu wako; uliwakomboa wazawa wa Yakobo na Yosefu. Maji yalipokuona, ee Mungu, maji yalipokuona, yaliogopa mno; naam, bahari ilitetemeka hata vilindini. Mawingu yalichuruzika maji, ngurumo zikavuma angani, mishale ya umeme ikaangaza kila upande. Kishindo cha ngurumo yako kilitokea katika kimbunga, umeme wako ukauangaza ulimwengu; dunia ikatikisika na kutetemeka. Wewe uliweka njia yako juu ya bahari; ulitembea juu ya maji yale mengi, lakini nyayo zako hazikuonekana. Wakati wa taabu namwomba Bwana; namnyoshea mikono yangu usiku bila kuchoka, lakini sipati faraja yoyote kwa mtu.
Na sisi tuko thabiti mbele ya Mungu kwani tuna hakika kwamba tukimwomba chochote kadiri ya matakwa yake, yeye hutusikiliza. Yeye hutusikiliza kila tunapomwomba; na kwa vile tunajua kwamba yeye hutusikiliza kila tunapomwomba, twajua pia kwamba hutupatia yote tunayomwomba.
Wapenzi wangu, msilipize kisasi, bali mwachieni Mungu jambo hilo; maana Maandiko Matakatifu yasema: “Kulipiza kisasi ni shauri langu; mimi nitalipiza, asema Bwana.”
Mwenyezi-Mungu atakukinga na baya lolote; atayalinda salama maisha yako. Mwenyezi-Mungu atakulinda katika shughuli zako zote tangu sasa na hata milele.
Msiwe na wasiwasi juu ya kitu chochote, ila kwa kila hali, mwombeni Mungu katika sala juu ya mahitaji yenu, kwa shukrani.
Mimi nilipofanikiwa, nilisema: “Kamwe sitashindwa!” Kwa wema wako, ee Mwenyezi-Mungu, umeniimarisha kama mlima mkubwa. Lakini ukajificha mbali nami, nami nikafadhaika.
Lakini Bwana ni mwaminifu. Yeye atawaimarisheni na kuwalinda salama na yule Mwovu.
Tunalo tumaini hilo kama nanga ya maisha yetu. Tumaini hilo lapenya mpaka mahali patakatifu mbinguni.