Rafiki, Mungu ametupa ahadi kwa kila hali. Yeye yuko nasi kila wakati, na ndiyo maana ametupa ahadi nzuri, ili tuamini kwamba yuko kazini na tupumzike kwake. Hakuna ahadi ya Mungu ambayo imewahi kufeli. Zote zimetimia.
Kila ahadi tunayoweza kuomba katika jina la Kristo imehakikishwa na itatimizwa na Mungu kwa faida yetu na kwa utukufu wake. Ahadi huwa na sehemu mbili: sharti na matokeo, ambayo yanategemea kutimizwa kwa sharti hilo. Ahadi ya Mungu ni tamko kutoka kwake lenye uwezo wa kutimia, mradi tu masharti yatimizwe.
Ukisoma Biblia, ni rahisi kupata ahadi nyingi sana kutoka kwa Mungu. Mfano mzuri ni ahadi ya wokovu iliyopo chini ya Agano Jipya. Mungu anasema kupitia Paulo, "Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka" (Warumi 10:9).
Katika ahadi ya wokovu ambayo tumeona, inategemea wewe kama utaamini na kukiri kwamba Yesu ni Bwana. Ukiamini na kukiri, ahadi hiyo inaamilishwa na inatimia. Lakini inakutegemea wewe. Mungu anataka kuokoa kila mtu, lakini si kila mtu anayefungua uwezo wa ahadi hiyo.
Kutoka 20:12 inasema, "Waheshimu baba yako na mama yako, ili siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako." Hii ni ahadi ya Mungu itakayotimia tu ikiwa unawaheshimu baba yako na mama yako. Kwa hivyo, ili kuona ahadi hiyo ya Mungu ikitimia katika maisha yako, lazima kwanza utimize sharti, na matokeo ya ahadi hiyo yatafuata.
Mungu akubariki.
Maana Mungu aliupenda ulimwengu hivi hata akamtoa Mwana wake wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uhai wa milele.
Na, ushahidi wenyewe ndio huu: Mungu alitupatia uhai wa milele, na uhai huo uko kwa Bwana. Yeyote aliye na Mwana wa Mungu anao uhai huo; asiye na Mwana wa Mungu, hana uhai.
Kwa maana mshahara wa dhambi ni kifo; lakini zawadi anayotoa Mungu ni uhai wa milele katika kuungana na Kristo Yesu, Bwana wetu.
Mimi nawapa uhai wa milele; nao hawatapotea milele, wala hakuna mtu atakayeweza kuwatoa mkononi mwangu. Baba yangu ambaye ndiye aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote, wala hakuna awezaye kuwatoa mikononi mwake Baba.
Yesu akamwambia, “Mimi ndimi ufufuo na uhai. Anayeniamini mimi hata kama anakufa, ataishi; na kila anayeishi na kuniamini, hatakufa kamwe. Je, waamini hayo?”
“Kweli nawaambieni, anayesikia neno langu, na kumwamini yule aliyenituma, anao uhai wa milele. Hatahukumiwa kamwe, bali amekwisha pita kutoka kifoni na kuingia katika uhai.
Maana anachotaka Baba yangu ndicho hiki: Kila amwonaye Mwana na kumwamini awe na uhai wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.”
Asifiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa huruma yake kuu alitufanya tuzaliwe upya kwa kumfufua Yesu kutoka kwa wafu. Ametujalia tumaini lenye uhai, na hivyo tunatazamia kupata baraka zile ambazo Mungu aliwawekea watu wake. Mungu amewawekeeni baraka hizo mbinguni ambako haziwezi kuoza, au kuharibika, au kufifia.
ambayo msingi wake ni tumaini la kupata uhai wa milele. Mungu ambaye hasemi uongo, alituahidia uhai huo kabla ya mwanzo wa nyakati,
Na uhai wa milele ndio huu: Kukujua wewe uliye peke yako Mungu wa kweli, na kumjua Yesu Kristo uliyemtuma.
Sikilizeni, nawaambieni siri: Sisi hatutakufa sote, ila sote tutageuzwa, wakati wa mbiu ya mwisho, kwa nukta moja, kufumba na kufumbua. Maana tarumbeta ya mwisho itakapolia, wafu watafufuliwa katika hali ya kutoweza kufa tena, na sisi tutageuzwa.
Na sasa imebakia tu kupewa tuzo la ushindi kwa maisha ya uadilifu, tuzo ambalo Bwana, Hakimu wa haki, atanipa mimi siku ile, na wala si mimi tu, ila na wale wote wanaotazamia kwa upendo kutokea kwake.
Lakini sisi ni raia wa mbinguni, na twatazamia kwa hamu kubwa Mwokozi aje kutoka mbinguni, Bwana Yesu Kristo. Yeye ataibadili miili yetu dhaifu na kuifanya ifanane na mwili wake mtukufu, kwa nguvu ile ambayo kwayo anaweza kuviweka vitu vyote chini ya utawala wake.
Maana patatolewa amri, sauti ya malaika mkuu, sauti ya tarumbeta ya Mungu, naye Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni. Ndipo wale waliokufa wakiwa wanamwamini Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai wakati huo tutakusanywa pamoja nao katika mawingu kumlaki Bwana hewani. Na hivyo tutakuwa daima pamoja na Bwana.
Yesu aliwaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu. Mwaminini Mungu, niaminini na mimi pia. Je, huamini kwamba mimi niko ndani ya Baba, naye Baba yuko ndani yangu? Maneno ninayowaambieni siyasemi kwa mamlaka yangu; Baba aliye ndani yangu anafanya kazi yake. Mnapaswa kuniamini ninaposema kwamba mimi niko ndani ya Baba naye Baba yuko ndani yangu. Ama sivyo, aminini kwa sababu ya mambo ninayofanya. Kweli nawaambieni, anayeniamini atafanya mambo ninayofanya mimi; naam, atafanya hata makuu zaidi, kwani ninakwenda kwa Baba. Na chochote mtakachoomba kwa jina langu nitafanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba chochote kwa jina langu, nitawafanyieni. “Mkinipenda mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba naye atawapeni Msaidizi mwingine, atakayekaa nanyi milele. Yeye ni Roho wa ukweli. Ulimwengu hauwezi kumpokea kwa sababu hauwezi kumwona wala kumjua. Lakini nyinyi mnamjua kwa sababu anabaki nanyi na yu ndani yenu. “Sitawaacha nyinyi yatima; nitakuja tena kwenu. Bado kidogo nao ulimwengu hautaniona tena, lakini nyinyi mtaniona; na kwa kuwa mimi ni hai, nanyi pia mtakuwa hai. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama isingekuwa hivyo, ningalikwisha waambieni. Sasa nakwenda kuwatayarishieni nafasi. Siku ile itakapofika mtajua kwamba mimi niko ndani ya Baba, nanyi mko ndani yangu, nami ndani yenu. Azipokeaye amri zangu na kuzishika, yeye ndiye anipendaye. Naye anipendaye mimi atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.” Yuda (si yule Iskarioti) akamwambia, “Bwana, itawezekanaje wewe kujidhihirisha kwetu na si kwa ulimwengu?” Yesu akamjibu, “Mtu akinipenda atashika neno langu, na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kukaa naye. Asiyenipenda hashiki maneno yangu. Na neno mlilosikia si langu, bali ni lake Baba aliyenituma. “Nimewaambieni mambo haya nikiwa bado pamoja nanyi, lakini Msaidizi, Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwa jina langu, atawafundisheni kila kitu na kuwakumbusheni yote niliyowaambieni. “Nawaachieni amani; nawapeni amani yangu. Siwapi nyinyi kama vile ulimwengu ufanyavyo. Msiwe na wasiwasi, wala msifadhaike. Mlikwisha sikia nikiwaambieni: ‘Ninakwenda zangu, kisha nitarudi tena kwenu.’ Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu ninakwenda kwa Baba, maana yeye ni mkuu kuliko mimi. Nimewaambieni haya sasa kabla hayajatokea, ili yatakapotokea mpate kuamini. Na nikienda na kuwatayarishieni nafasi, nitarudi na kuwachukueni kwangu, ili nanyi muwe pale nilipo mimi.
Yeye atayafuta machozi yao yote; maana kifo hakitakuwako tena, wala uchungu, wala kilio, wala maumivu; maana ile hali ya kale imepita!”
Maana tunajua kwamba hema hii ambamo tunaishi sasa hapa duniani yaani mwili wetu, itakapongolewa, Mungu atatupa makao mengine mbinguni, nyumba ya milele isiyotengenezwa kwa mikono.
Usiku hautakuwako tena, wala hawatahitaji mwanga wa taa au wa jua, maana Bwana Mungu atawaangazia, nao watatawala milele na milele.
Nawaandikieni mpate kujua kwamba mnao uhai wa milele nyinyi mnaoamini kwa jina la Mwana wa Mungu.
Maana ninajua hakika kwamba hakuna kitu kiwezacho kututenganisha na upendo wake: Wala kifo, wala uhai; wala malaika au nguvu nyingine za mbinguni; wala yanayotokea sasa, wala yatakayotokea baadaye; wala mamlaka; wala ulimwengu wa juu, wala wa chini kabisa. Hakuna kiumbe chochote kitakachoweza kututenga na upendo wa Mungu katika Kristo Yesu Bwana wetu.
Basi, hawa watakwenda kwenye adhabu ya milele, lakini wale waadilifu watakwenda kwenye uhai wa milele.”
Basi, mwili huu wenye kuharibika utakapojivalia hali ya kutoharibika, na kile chenye kufa kitakapojivalia hali ya kutokufa, hapo ndipo litakapotimia lile neno lililoandikwa: “Kifo kimeangamizwa; ushindi umekamilika!” “Kifo, ushindi wako uko wapi? Uwezo wako wa kuumiza uko wapi?”
lakini Mungu alinionea huruma, ili Kristo aoneshe uvumilivu wake wote kwangu mimi, kama mfano kwa wale wote ambao baadaye watamwamini na kupokea uhai wa milele.
Lakini sisi, kufuatana na ahadi yake, twangojea mbingu mpya na dunia mpya ambayo imejaa uadilifu.
Maana, kwa neema ya Mungu mmekombolewa kwa njia ya imani. Jambo hili si matokeo ya juhudi zenu, bali ni zawadi ya Mungu. Wala halitokani na matendo yenu wenyewe, asije mtu akajivunia kitu.
“Mshindi atavikwa hivyo kwa mavazi meupe. Nami sitalifuta jina lake kutoka katika kitabu cha uhai; tena nitamkiri kwamba ni wangu mbele ya Baba yangu na mbele ya malaika wake.
Hivyo yeye ni mpatanishi wa agano jipya ambamo wale walioitwa na Mungu wanaweza kupokea baraka za milele walizoahidiwa. Kifo chake huwakomboa watu kutoka yale makosa waliyofanya wakati wa lile agano la kale.
kwa sababu Mwanakondoo aliye katikati ya kiti cha enzi atakuwa mchungaji wao, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji ya uhai. Naye Mungu atayafuta machozi yote machoni mwao.”
Msikishughulikie chakula kiharibikacho; kishughulikieni chakula kidumucho kwa ajili ya uhai wa milele. Mwana wa Mtu ambaye Baba amemthibitisha atawapeni chakula hicho.”
Na kila aliyeacha nyumba, au ndugu, au dada, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, atapokea mara mia zaidi, na kupata uhai wa milele.
Wanionesha njia ya kufikia uhai; kuwako kwako kwanijaza furaha kamili, katika mkono wako wa nguvu mna mema ya milele.
Lakini, ni kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Mambo ambayo jicho halijapata kuyaona, wala sikio kuyasikia, mambo ambayo binadamu hajapata kuyafikiria moyoni, hayo ndiyo Mungu aliyowatayarishia wale wampendao.”
Kama vile dhambi ilivyotawala kwa kifo, kadhalika neema inatawala kwa uadilifu na kuleta uhai wa milele kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.
Wapenzi wangu, sisi ni watoto wa Mungu sasa, lakini bado haijaonekana wazi jinsi tutakavyokuwa. Lakini tunajua kwamba, wakati Kristo atakapotokea, tutafanana naye kwani tutamwona vile alivyo.
Bwana Mungu atakiangamiza kifo milele! Atayafuta machozi katika nyuso za watu wote na kuwaondolea watu wake aibu duniani kote. Bwana Mwenyezi-Mungu ametamka.
Hata hivyo, msifurahi kwa sababu pepo wamewatii, bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.”
Anayependa maisha yake, atayapoteza; anayeyachukia maisha yake katika ulimwengu huu, atayaweka kwa ajili ya uhai wa milele.
Lakini mkisha teseka muda mfupi, Mungu aliye asili ya neema yote na ambaye anawaiteni kuushiriki utukufu wake wa milele katika kuungana na Kristo, yeye mwenyewe atawakamilisheni na kuwapeni uthabiti, nguvu na msingi imara.
Tuzingatie kabisa tumaini letu tunalokiri, maana Mungu aliyefanya ahadi zake ni mwaminifu.
Lakini wote wanaomtumainia Mwenyezi-Mungu, watapata nguvu mpya. Watapanda juu kwa mabawa kama tai; watakimbia bila kuchoka; watatembea bila kulegea.
Mwizi huja kwa shabaha ya kuiba, kuua na kuharibu. Mimi nimekuja mpate kuwa na uhai – uhai kamili.
Ndivyo ilivyo kuhusu ufufuo wa wafu. Kama vile mbegu, mwili huzikwa ardhini ukiwa katika hali ya kuharibika, lakini hufufuliwa katika hali ya kutoharibika. Huzikwa katika hali duni, hufufuliwa katika hali tukufu; huzikwa katika hali dhaifu, hufufuliwa ukiwa wenye nguvu. Unapozikwa ni mwili wa kawaida, unapofufuliwa ni mwili wa kiroho. Kuna mwili wa kawaida na kutakuwa na mwili wa kiroho.
Naye Roho mwenyewe anathibitisha na roho zetu kwamba sisi ni watoto wa Mungu. Basi, kwa vile sisi ni watoto wa Mungu, tutapokea baraka zote Mungu alizowawekea watu wake, na tutashiriki urithi huo pamoja na Kristo; maana, tukiyashiriki mateso yake Kristo, tutaushiriki pia utukufu wake.
“Aliye na masikio, basi, na asikie yale Roho anayoyaambia makanisa! “Mshindi nitamjalia kula matunda ya mti wa uhai ulioko ndani ya bustani ya Mungu.
Na Mungu alionesha upendo wake kwetu kwa kumtuma Mwanae wa pekee ulimwenguni, ili tuwe na uhai kwa njia yake.
Taabu tunayopata ni kidogo, tena ya muda tu; lakini itatupatia utukufu upitao matazamio yote, utukufu ambao hauna mwisho. Hivyo tunatazamia kwa makini si vitu vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Maana vinavyoonekana ni vya muda tu; lakini vile visivyoonekana ni vya milele.
Yeye alituokoa katika nguvu ya giza, akatuleta salama katika ufalme wa Mwanae mpenzi. Kwake yeye tunakombolewa, yaani dhambi zetu zinaondolewa.
lakini imefunuliwa kwetu sasa kwa kuja kwake Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Yeye amekomesha nguvu za kifo, na kwa njia ya Habari Njema akadhihirisha uhai usio na kifo.
Nanyi pia watu wa mataifa mengine, mliusikia ujumbe wa kweli yaani Habari Njema iliyowaletea wokovu, mkamwamini Kristo; naye Mungu, ili kuonesha kuwa nyinyi ni wake, akawapiga mhuri kwa kuwapeni yule Roho Mtakatifu aliyetuahidia. Huyu Roho ni dhamana ya kupata yote yale Mungu aliyowaahidia watu wake, na jambo hili latuhakikishia kwamba Mungu atawakomboa kabisa wote walio wake. Tuusifu utukufu wake!
Wameneemeka sana, tena heri yao wote wanaoshiriki ufufuo huu wa kwanza. Kifo cha pili hakitakuwa na nguvu juu yao; watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, na watatawala pamoja naye kwa miaka 1,000.
Tunalo tumaini hilo kama nanga ya maisha yetu. Tumaini hilo lapenya mpaka mahali patakatifu mbinguni.
Lakini atakayekunywa maji nitakayompa mimi, hataona kiu milele. Maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji ya uhai na kumpatia uhai wa milele.”
Uhai huo ulipotokea sisi tuliuona na sasa tunasema habari zake na kuwaambieni juu ya uhai huo wa milele uliokuwa kwa Baba na uliodhihirishwa kwetu.
Maana kwa njia ya neno hai la Mungu, nyinyi mmezaliwa upya, si kama watoto wa baba awezaye kufa, bali baba asiyekufa milele.
Kwa namna hiyo ametujalia zawadi kuu na za thamani ambazo alituahidia, ili kwa zawadi hizo mpate kuziepa kabisa tamaa mbaya zilizomo duniani, na kuishiriki hali yake ya kimungu.
“Mimi ni mzabibu, nanyi ni matawi. Akaaye ndani yangu, nami nikiwa ndani yake, huyo huzaa matunda mengi, maana bila mimi hamwezi kufanya chochote.
Roho na Bibi arusi waseme, “Njoo!” Kila mtu asikiaye hili, na aseme, “Njoo!” Aliye na kiu na aje; anayependa, na achukue maji ya uhai bila malipo.
Yesu akamjibu, “Mimi ni njia, na ukweli na uhai. Hakuna awezaye kwenda kwa Baba ila kwa kupitia kwangu.
Basi, kila mtu aliye na tumaini hili katika Kristo, hujiweka safi kama vile Kristo alivyo safi kabisa.
Kweli wema wako na fadhili zako zitakuwa pamoja nami, siku zote za maisha yangu; nami nitakaa nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu milele.
Kisha, nikaona mbingu mpya na dunia mpya. Mbingu ile ya kwanza na dunia ile ya kwanza vilikuwa vimetoweka, nayo bahari pia haikuwako tena.
Lakini Mungu amethibitisha kwamba anatupenda, maana wakati tulipokuwa bado wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu.
Wafu wako wataishi tena, miili yao itafufuka. Wanaolala mavumbini wataamka na kuimba kwa furaha! Mungu atapeleka umande wake wa uhai, nao walio kwa wafu watatoka hai.
Furahini na kushangilia maana tuzo lenu ni kubwa mbinguni. Hivyo ndivyo walivyowadhulumu manabii waliokuwako kabla yenu.
Wala si hivyo viumbe peke yake, bali hata sisi tulio na huyo Roho, aliye wa kwanza wa zawadi za Mungu; sisi pia tunalalamika ndani yetu, tukingojea tufanywe watoto wa Mungu, nazo nafsi zenu zikombolewe.
Lakini sasa wanataka nchi iliyo bora zaidi, yaani nchi ya mbinguni. Ndio maana Mungu haoni haya wakimwita yeye Mungu wao, kwa sababu yeye mwenyewe amekwisha watayarishia mji.
Kisha, nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Andika! Heri watu ambao tangu sasa wanakufa wakiwa wameungana na Bwana.” Naye Roho asema, “Naam! Watapumzika kutoka taabu zao; maana matunda ya jasho lao yatawafuata.”
Nawe ndugu yangu mwaminifu, nakutaka uwasaidie akina mama hao, kwani wamefanya kazi ya kueneza Injili kwa bidii pamoja nami na Klementi na wafanyakazi wenzangu wengine wote ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uhai.
Kwa maana Kristo mwenyewe alikufa kwa ajili ya dhambi zenu; alikufa mara moja tu na ikatosha, mtu mwema kwa ajili ya waovu, ili awapeleke nyinyi kwa Mungu. Aliuawa kimwili lakini akafanywa hai kiroho;
Mungu mwenyewe anayetupatia amani awatakase nyinyi kabisa kwa kila namna na kuzilinda nafsi zenu – roho, mioyo na miili yenu – mbali na hatia yoyote wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye anayewaita nyinyi atafanya hivyo kwani ni mwaminifu.
Mimi ni mlango. Anayeingia kwa kupitia kwangu ataokolewa; ataingia na kutoka, na kupata malisho.
Bado kidogo nao ulimwengu hautaniona tena, lakini nyinyi mtaniona; na kwa kuwa mimi ni hai, nanyi pia mtakuwa hai.
Tunachoona sasa ni kama tu sura hafifu katika kioo, lakini hapo baadaye tutaona uso kwa uso. Sasa ninajua kiasi fulani tu, lakini hapo baadaye nitajua yote kikamilifu, kama vile Mungu anavyonijua mimi.
Bwana hakawii kutimiza yale aliyoahidi kama watu wengine wanavyofikiri kuwa atakawia. Yeye ana saburi kwa ajili yenu, maana hapendi hata mmoja wenu apotee, bali huwavuta wote wapate kutubu.
Piga mbio kadiri uwezavyo katika shindano la mbio za imani, ukajipatie tuzo la uhai wa milele uliloitiwa wakati ulipokiri imani yako mbele ya mashahidi wengi.
Simoni Petro akamjibu, “Bwana, tutakwenda kwa nani? Wewe unayo maneno ya uhai wa milele.
Mtu yeyote akiungana na Kristo huwa kiumbe kipya, mambo ya kale yamepita, hali mpya imefika.
Lakini njia inayoongoza kwenye uhai ni nyembamba, na mlango wa kuingilia humo ni mwembamba; ni watu wachache tu wanaoweza kuigundua njia hiyo.
Anayemwamini Mwana anao uhai wa milele; asiyemwamini Mwana hatakuwa na uhai wa milele, bali ghadhabu ya Mungu hubaki juu yake.
maana Mwenyezi-Mungu hupenda uadilifu, wala hawaachi waaminifu wake. Huwalinda hao milele; lakini wazawa wa waovu wataangamizwa.
Basi, wale ambao Mungu aliwateua ndio hao aliowaita; na hao aliowaita ndio hao aliowafanya kuwa waadilifu na hao aliowafanya waadilifu ndio hao aliowashirikisha pia utukufu wake.
Sisi tunaamini kwamba Yesu alikufa, akafufuka; na hivyo sisi tunaamini kwamba Mungu atawaleta pamoja na Yesu wale wote waliofariki wakiwa wanamwamini.
“Mshindi nitamfanya awe nguzo katika hekalu la Mungu wangu, na hatatoka humo kamwe. Pia nitaandika juu yake jina la Mungu wangu na jina la mji wa Mungu wangu, yaani Yerusalemu mpya, mji ambao utashuka kutoka juu mbinguni kwa Mungu wangu. Tena nitaandika juu yake jina langu jipya.
Yesu alipozungumza nao tena, aliwaambia, “Mimi ndimi mwanga wa ulimwengu. Anayenifuata mimi hatembei kamwe gizani, bali atakuwa na mwanga wa uhai.”
Sioni aibu kutangaza Habari Njema; yenyewe ni nguvu ya Mungu inayowaokoa wote wanaoamini: Wayahudi kwanza na wasio Wayahudi pia.
Msimhuzunishe Roho Mtakatifu wa Mungu, maana Roho huyo ni alama ya Mungu kwenu kwamba nyinyi ni watu wake, na thibitisho kwamba siku itakuja ambapo Mungu atawakomboeni.
“Baba! Nataka hao ulionipa wawe pamoja nami pale nilipo, ili wauone utukufu wangu ulionipa; kwa kuwa ulinipenda kabla ya kuumbwa ulimwengu.
Lakini hakuna chochote kilicho najisi kitakachoingia humo; wala mtu yeyote atendaye mambo ya kuchukiza au ya uongo hataingia humo. Ni wale tu walioandikwa katika kitabu cha uhai cha Mwanakondoo ndio watakaoingia ndani.
Ama hakika, hawawezi kufa tena, kwa sababu watakuwa kama malaika, na ni watoto wa Mungu kwa vile wamefufuliwa katika wafu.
Sisi basi, na tushukuru, kwani tunapokea ufalme usiotikisika. Tuwe na shukrani na kumwabudu Mungu kwa namna itakayompendeza, kwa ibada na hofu;
Watu wako uliowakomboa, ee Mwenyezi-Mungu, watarudi, watakuja Siyoni wakiimba; watajaa furaha ya milele, watapata furaha na shangwe. Huzuni na maombolezo vitatoweka kabisa.
“Kama mkono au mguu wako ukikukosesha, ukate na kuutupa mbali nawe. Afadhali kwako kuingia katika uhai bila mkono au mguu, kuliko kutupwa katika moto wa milele ukiwa na mikono miwili na miguu yako miwili. Na jicho lako likikukosesha, lingoe na kulitupa mbali nawe. Afadhali kwako kuingia katika uhai ukiwa chongo, kuliko kutupwa katika moto wa Jehanamu ukiwa na macho yako yote mawili.
Lakini fadhili za Mwenyezi-Mungu hudumu milele, kwa wale wote wanaomheshimu; na wema wake wadumu vizazi vyote,
Ulimwengu pamoja na vitu vyake vyote vyenye kutamanika unapita; lakini mtu atendaye atakalo Mungu, anaishi milele.
ndiye aliyetutia mhuri wa kuwa mali yake yeye na kutujalia Roho mioyoni mwetu kama dhamana ya mambo yote ambayo ametuwekea.
Wale wanaozingatia kutenda mema, kutafuta utukufu na heshima ya Mungu na kutokufa, watapata uhai wa milele.
naye Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani. Namwomba mpate kuwa na mzizi na msingi katika mapendo kusudi muweze kufahamu pamoja na watu wote wa Mungu jinsi upendo wa Kristo ueneavyo kwa mapana na marefu, kwa kimo na kina. Naam, mpate kujua upendo wa Kristo upitao elimu yote, mjazwe kabisa utimilifu wote wa Mungu.
Msistaajabie jambo hili; maana wakati unakuja ambapo wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake, nao watafufuka: Wale waliotenda mema watafufuka na kuishi, na wale waliotenda maovu watafufuka na kuhukumiwa.
“Hutahitaji tena jua kukuangazia mchana, wala mwezi kukumulikia usiku; maana mimi Mwenyezi-Mungu ni mwanga wako milele; mimi Mungu wako nitakuwa fahari yako. Tazama, giza litaifunika dunia, giza nene litayafunika mataifa; lakini wewe, Mwenyezi-Mungu atakuangazia, utukufu wake utaonekana kwako. Mwanga wako mchana hautatua kama jua, wala mwangaza wako usiku kufifia kama mbalamwezi; maana Mwenyezi-Mungu ni mwanga wako milele, nazo siku zako za kuomboleza zitakoma.
Maana tunajua kwamba hema hii ambamo tunaishi sasa hapa duniani yaani mwili wetu, itakapongolewa, Mungu atatupa makao mengine mbinguni, nyumba ya milele isiyotengenezwa kwa mikono. Maana sote ni lazima tusimame mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mmoja apokee anayostahili kwa matendo aliyoyafanya wakati alipokuwa anaishi duniani, mema au mabaya. Basi, sisi tunajua umuhimu wa kumcha Bwana, na hivyo tunajitahidi kuwavuta watu. Mungu anatujua waziwazi, nami natumaini kwamba nanyi pia mnatujua kinaganaga. Si kwamba tunajaribu tena kujipendekeza kwenu, ila tunataka kuwapa nyinyi sababu zetu za kuona fahari juu yenu, ili mpate kuwajibu wale wanaojivunia hali yao ya nje zaidi kuliko jinsi walivyo moyoni. Ikiwa tumeonekana kuwa wendawazimu, hiyo ni kwa ajili ya Mungu; na ikiwa tunazo akili zetu timamu, hiyo ni kwa faida yenu. Maana mapendo ya Kristo yanatumiliki sisi ambao tunatambua ya kwamba mtu mmoja tu amekufa kwa ajili ya wote, na hiyo ina maana kwamba wote wanashiriki kifo chake. Alikufa kwa ajili ya watu wote, ili wanaoishi wasiishi kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa, akafufuliwa kwa ajili yao. Basi, tangu sasa, sisi hatumpimi mtu yeyote kibinadamu. Hata kama kwa wakati mmoja tulimpima Kristo kibinadamu, sasa si hivyo tena. Mtu yeyote akiungana na Kristo huwa kiumbe kipya, mambo ya kale yamepita, hali mpya imefika. Yote ni kazi ya Mungu mwenye kutupatanisha sisi naye kwa njia ya Kristo, na kutupa jukumu la kuwapatanisha watu naye. Ndiyo kusema: Mungu, amekuwa akiupatanisha ulimwengu naye kwa njia ya Kristo, bila kutia maanani dhambi zao binadamu. Yeye ametupa ujumbe kuhusu kuwapatanisha watu naye. Na sasa, katika hali hii, tunaugua tukitazamia kwa hamu kubwa kuvikwa makao yetu yaliyo mbinguni.
Mnahitaji kuwa na uvumilivu ili muweze kutimiza matakwa ya Mungu na kupokea kile alichoahidi.
Namwomba Mungu aifunue mioyo yenu iweze kuuona mwanga wake, mpate kutambua lile tumaini alilowaitieni na utukufu mkuu wa zawadi alizowawekea watu wake,
Tunajua kwamba yule aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua sisi pia pamoja na Yesu na kutuweka mbele yake pamoja nanyi.
Hizo zitakuwa zenu nyinyi ambao kwa imani mnalindwa salama kwa nguvu ya Mungu kwa ajili ya wokovu ambao uko tayari kufunuliwa mwishoni mwa nyakati.
Waliokombolewa na Mwenyezi-Mungu watarudi, watakuja Siyoni wakipiga vigelegele. Watakuwa wenye furaha ya milele, watajaliwa furaha na shangwe; huzuni na kilio vitatoweka kabisa.
Maana ujumbe kuhusu kifo cha Kristo msalabani ni jambo la kipumbavu kwa wale walio katika mkumbo wa kupotea, lakini kwetu sisi tulio katika njia ya wokovu, ujumbe huo ni nguvu ya Mungu.
Wapenzi wangu, tupendane, maana upendo hutoka kwa Mungu. Kila mtu aliye na upendo ni mtoto wa Mungu, na anamjua Mungu.
Yesu akawaambia, “Mimi ndimi mkate wa uhai. Anayekuja kwangu hataona njaa; anayeniamini hataona kiu kamwe.
Siku moja tu katika maskani yako, ni bora kuliko siku elfu mahali pengine; afadhali kusimama mlangoni pa nyumba yako, kuliko kuishi nyumbani kwa watu waovu. Mwenyezi-Mungu ni jua letu na ngao yetu; yeye hutuneemesha na kutujalia fahari. Hawanyimi chochote kilicho chema, wale waishio kwa unyofu.
Bwana wake akamwambia, ‘Vema, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu katika mambo madogo, nitakukabidhi makubwa. Njoo ufurahi pamoja na bwana wako.’
Usiogope hata kidogo yale ambayo itakulazimu kuteseka. Sikiliza! Ibilisi anataka kuwajaribu kwa kuwatia baadhi yenu gerezani; nanyi mtapata dhiki kwa muda wa siku kumi. Muwe waaminifu hata mpaka kufa, nami nitawapeni taji ya uhai.
Kwa kuungana na Kristo Yesu, Mungu alitufufua pamoja naye, tukatawale pamoja naye mbinguni. Ndivyo alivyopenda kuonesha kwa watu wa nyakati za baadaye ukuu wa neema yake aliyotujalia kwa ukarimu katika kuungana kwetu na Kristo Yesu.
Kwa hiyo, basi, muwe tayari kabisa, na kukesha. Wekeni tumaini lenu lote katika neema ile mtakayopewa wakati Yesu Kristo atakapoonekana!
Twajua pia kwamba Mwana wa Mungu amekuja, akatupa elimu ili tumjue Mungu wa kweli; tuishi katika muungano na Mungu wa kweli – katika muungano na Mwanae, Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na huu ndio uhai wa milele.
Kwangu, kuishi ni Kristo, na kufa ni faida zaidi. Lakini, kama kwa kuishi nitaweza kufanya kazi yenye faida zaidi, basi, sijui nichague lipi! Nakabiliwa na haya mawili yaliyo sawa. Natamani kuyaacha maisha haya nikakae pamoja na Kristo, jambo ambalo ni bora zaidi;
Lakini sasa mmekwisha kombolewa kutoka utumwa wa dhambi na mmekuwa watumishi wa Mungu; faida mliyo nayo sasa ni utakatifu, na matokeo yake ni uhai wa milele.
Heri yao wale wanaoosha mavazi yao, wapate kuwa na haki ya kula tunda la mti wa uhai, na haki ya kuingia mjini kwa kupitia milango yake.
Lakini ukweli ni kwamba Kristo amefufuliwa kutoka kwa wafu, wa kwanza wa wale waliolala katika kifo. Maana kama vile kifo kilivyoletwa duniani na mtu mmoja, vivyo hivyo nako kufufuka kutoka kwa wafu kumesababishwa na mtu mmoja. Kama vile watu wote wanavyokufa kwa kujiunga na Adamu, vivyo hivyo wote watafufuliwa kwa kuungana na Kristo.
Ikiwa Roho wa Mungu aliyemfufua Kristo kutoka wafu anaishi ndani yenu, basi huyo aliyemfufua Kristo kutoka kwa wafu ataipa uhai miili yenu yenye hali ya kufa; atafanya hivyo kwa njia ya Roho wake akaaye ndani yenu.
Mungu mwenyewe alitutayarishia mabadiliko hayo, naye ametupa Roho wake awe dhamana ya yote aliyotuwekea.
Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: ‘Anayeniamini mimi, mito ya maji ya uhai itatiririka kutoka moyoni mwake!’”
na hivyo tunatazamia kupata baraka zile ambazo Mungu aliwawekea watu wake. Mungu amewawekeeni baraka hizo mbinguni ambako haziwezi kuoza, au kuharibika, au kufifia.
Kama vile Baba huwafufua wafu na kuwapa uhai, vivyo hivyo naye Mwana huwapa uhai wale anaopenda.
Anayeyashikilia maisha yake, atayapoteza; lakini anayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu, atayapata.
Basi, kama vile kila mtu hufa mara moja tu, kisha husimama mbele ya hukumu ya Mungu, vivyo hivyo Kristo naye alijitoa tambiko mara moja tu kwa ajili ya kuziondoa dhambi za wengi. Atakapotokea mara ya pili, si kwa ajili ya kupambana na dhambi, bali ni kwa ajili ya kuwaokoa wale wanaomngojea.
ili kwa neema yake tupate kukubaliwa kuwa waadilifu na kuupokea uhai wa milele tunaotumainia.
Mimi ni yeye aliye hai! Nilikuwa nimekufa, lakini, tazama, sasa ni hai milele na milele. Ninazo funguo za kifo na kuzimu.