Neno la Mungu lina nguvu na linatubadilisha. Kuna mistari mingi ambayo tunasikia mara kwa mara na yenye uwezo wa kutubadilisha. Inaweza kubadilisha mawazo yetu, jinsi tunavyoishi. Ni mistari ambayo tunajifunza ili tuitendee kazi katika kila hali.
"Ninaweza kufanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu." (Wafilipi 4:13). Huu ni mmoja wa mistari ambao tunajifunza mara kwa mara, na tunautumia wakati tunahisi tumekata tamaa. Unatupa nguvu ya kusonga mbele.
"Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele." (Yohana 3:16). Huu ni moja wapo wa mistari muhimu sana, na ni miongoni mwa mistari ya kwanza unayosikia unapojua kumhusu Bwana wetu Yesu. Ni msitari unaotuonyesha upendo mkubwa wa Mungu kwetu.
Kuna mistari mingine mingi sana ambayo inasemwa mara kwa mara, na hapa utaipata.
Mtumaini Mwenyezi-Mungu kwa moyo wako wote, wala usitegemee akili zako mwenyewe. Umtambue Mungu katika kila ufanyalo, naye atazinyosha njia zako.
Lakini kama mmoja wenu ametindikiwa hekima, basi, anapaswa kumwomba Mungu ambaye atampatia; kwani Mungu huwapa wote kwa wingi na kwa ukarimu.
Kumcha Mwenyezi-Mungu ni shule ya hekima; kabla ya kuheshimika ni lazima kuwa mnyenyekevu.
Mtu asiye mwepesi wa hasira ana busara kubwa, lakini akasirikaye upesi hukuza upumbavu.
Heri mtu anayegundua hekima, mtu yule anayepata ufahamu. Hekima ni bora kuliko fedha, ina faida kuliko dhahabu.
“Mimi Hekima nina thamani kuliko johari; chochote unachotamani hakiwezi kulingana nami.
Nyumba hujengwa kwa hekima, na kuimarishwa kwa busara. Nilipitia karibu na shamba la mvivu; shamba la mzabibu la mtu mpumbavu. Nilishangaa kuona limemea miiba, magugu yamefunika eneo lake lote, na ukuta wake wa mawe umebomoka. Nilitazama, nikawaza, mwishowe nikapata funzo: Lala tu kidogo; sinzia tu kidogo! Kunja mikono yako tu upumzike! Lakini kumbuka kwamba uwapo usingizini, umaskini utakuvamia kama mnyanganyi, ufukara kama mtu mwenye silaha. Kwa maarifa vyumba vyake hujazwa vitu vya thamani na vya kupendeza.
Kulindwa na hekima ni kama kulindwa na fedha. Faida ya maarifa ni kwamba hekima hulinda maisha ya mtu aliye nayo.
Mwenye hekima ni mwangalifu na huepa uovu, lakini mpumbavu hajizuii wala hana uangalifu.
Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa wazee wake, lakini mke mwenye busara hutoka kwa Mwenyezi-Mungu.
Kuna dhahabu na wingi wa mawe ya thamani kubwa; lakini cha thamani kubwa zaidi ni maneno ya busara!
Mipango ya mtu wa bidii huleta mali kwa wingi, lakini kila aliye na pupa huishia patupu.
Hakuna hekima, maarifa, wala mawaidha yoyote ya mtu, yawezayo kumshinda Mwenyezi-Mungu.
Mwanangu, usiyasahau mafundisho yangu, bali kwa moyo wako uzishike amri zangu. Hapo ghala zako zitajaa nafaka, na mapipa yako yatafurika divai mpya. Mwanangu, usidharau adhabu ya Mwenyezi-Mungu, wala usiudhike kwa maonyo yake; maana Mwenyezi-Mungu humwonya yule ampendaye, kama baba amwonyavyo mwanawe mpenzi. Heri mtu anayegundua hekima, mtu yule anayepata ufahamu. Hekima ni bora kuliko fedha, ina faida kuliko dhahabu. Hekima ina thamani kuliko johari, hamna unachotamani kiwezacho kulingana nayo. Kwa mkono wake wa kulia Hekima atakupa maisha marefu; kwa mkono wake wa kushoto atakupa mali na heshima. Njia zake ni za kupendeza, zote zaelekea kwenye amani. Hekima ni mti wa uhai kwa wote wampatao; wana heri wote wanaoshikamana naye. Kwa hekima Mwenyezi-Mungu aliweka misingi ya dunia, kwa akili aliziimarisha mbingu. Maana yatakupa wingi wa siku, maisha marefu na fanaka kwa wingi.
Mfunze mwenye hekima naye atazidi kuwa na hekima; mfundishe mwadilifu naye atazidi kuelimika.
Hizi ni methali za Solomoni: Mtoto mwenye hekima ni furaha ya baba yake; lakini mtoto mpumbavu ni huzuni ya mama yake.
Anayeandamana na wenye hekima hupata hekima, lakini anayejiunga na wapumbavu atapata madhara.
Mwanamke mwenye hekima huijenga nyumba yake, lakini mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe.
Hekima ya mwenye busara humwonesha njia yake, lakini upumbavu wa wapumbavu huwadanganya wenyewe.
Maneno yaweza kuwa chemchemi ya hekima; yenye kilindi kama bahari, kama kijito kinachobubujika.
Maneno ya mpumbavu huleta ugomvi; kila anachosema husababisha adhabu. Kinywa cha mpumbavu humwangamiza mwenyewe; mdomo wake ni mtego wa kumnasa yeye mwenyewe.
Maana kwa mwongozo mzuri waweza kupigana vita, na kwa washauri wengi ushindi hupatikana.
Anayetegemea akili yake mwenyewe ni mpumbavu; lakini anayeishi kwa hekima atakuwa salama.
Afadhali kuwa na kidogo na kumcha Mwenyezi-Mungu, kuliko kuwa na mali nyingi pamoja na taabu.
Jipatie hekima, jipatie ufahamu; usisahau wala kupuuza maneno yangu. Usimwache Hekima, naye atakutunza; umpende, naye atakulinda.
Mwanangu, zingatia hekima safi na busara; usiviache vitoweke machoni pako, navyo vitakuwa uhai nafsini mwako, na pambo zuri shingoni mwako.
Asiye mwepesi wa hasira ni bora kuliko mwenye nguvu; aitawalaye nafsi yake ni bora kuliko autekaye mji.
Mipango mizuri hufanyika kwa kushauriana; ukitaka kuanza vita lazima kutafakari kwanza.
Mke mwema ni taji ya fahari kwa mumewe; amwaibishaye mumewe ni kama kidonda mifupani mwake.
Mungu humjalia mtu apendezwaye naye hekima, akili na furaha; lakini humpa mwenye dhambi kazi ya kuvuna na kurundika, kisha akampa anayempendeza yeye Mungu. Yote hayo pia ni bure kabisa; ni sawa na kufukuza upepo.
Zingatia mafundisho ya Hekima na usimwache aponyoke, mshike kwa makini maana yeye ni uhai wako.
Usifanye urafiki na mtu wa hasira, wala usiandamane na mwenye ghadhabu, usije ukajifunza mwenendo wake, ukajinasa kabisa katika mtego.
Mwanangu, moyo wako ukiwa wenye busara, moyo wangu pia utakuwa wenye furaha. Moyo wangu utashangilia, mdomo wako utakaposema maneno yaliyo sawa.
Amchimbiaye mwenzake shimo, hutumbukia mwenyewe; abingirishaye jiwe litamrudia mwenyewe.
Nguvu nyingi zaidi zahitajika kwa mtumiaji shoka butu lisilonolewa, lakini kutumia hekima humfanya mtu afanikiwe.
Kumcha Mwenyezi-Mungu kunaleta uhai; amchaye hujaliwa pumziko la kutosheleza, wala hatapatwa na baa lolote.
Mizani ya udanganyifu ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu, lakini matumizi ya kipimo halali ni furaha kwake.
Kuna vitu sita anavyochukia Mwenyezi-Mungu; naam, vitu saba ambavyo ni chukizo kwake: Macho ya kiburi, ulimi mdanganyifu, mikono inayoua wasio na hatia, moyo unaopanga mipango miovu, miguu iliyo mbioni kutenda maovu, shahidi wa uongo abubujikaye uongo, na mtu achocheaye fitina kati ya ndugu.
Dhamiri ya mtu ni taa ya Mwenyezi-Mungu; huchunguza nafsi yake mtu mpaka ndani kabisa.
Je, yuko mtu mwenye maarifa kazini mwake? Huyo atawatumikia wafalme; hatawapa huduma yake watu wasiofaa.
Anayemsaidia maskini anamkopesha Mwenyezi-Mungu; Mwenyezi-Mungu atamlipa kwa tendo lake jema.
Baraka za Mwenyezi-Mungu ndizo ziletazo fanaka, juhudi za mtu haziongezi hapo chochote.
Usimnyime mtu anayehitaji msaada, ikiwa unao uwezo wa kufanya hivyo. Usimwambie jirani yako aende zake hadi kesho, hali wewe waweza kumpa anachohitaji leo.
Njia ya watu wema ni kama nuru ya alfajiri, ambayo hungaa zaidi na zaidi hata mchana kamili. Lakini njia ya waovu ni kama giza nene, hawajui kinachowafanya wajikwae.
Moyo wako usiwaonee wivu wenye dhambi, ila endelea kumcha Mwenyezi-Mungu siku zote. Hakika kuna kesho ya milele, na tumaini lako halitakuwa bure.
Mwenyezi-Mungu hutaka kipimo na mizani halali; mawe yote mfukoni ya kupimia ni kazi yake.
Kwa hekima Mwenyezi-Mungu aliweka misingi ya dunia, kwa akili aliziimarisha mbingu. Maana yatakupa wingi wa siku, maisha marefu na fanaka kwa wingi. Kwa maarifa yake vilindi vilipasuka, na mawingu yakadondosha umande.
Utii na uaminifu visitengane nawe. Vifunge shingoni mwako; viandike moyoni mwako. Usigombane na mtu bila sababu ikiwa hajakudhuru kwa lolote. Usimwonee wivu mtu mkatili, wala usiige mwenendo wake. Maana waovu ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu; lakini yeye huwafanya marafiki zake wale walio wanyofu. Mwenyezi-Mungu huapiza nyumba za waovu, lakini huyabariki makao ya waadilifu. Yeye huwadharau wenye dharau, lakini huwafadhili wanyenyekevu. Wenye hekima watavuna heshima, lakini wapumbavu watapata fedheha. Hivyo utakubalika na kusifika, mbele ya Mungu na mbele ya wanadamu.