Nimewaambieni mambo haya ili mpate kuwa na amani katika kuungana nami. Ulimwenguni mtapata masumbuko; lakini jipeni moyo! Mimi nimeushinda ulimwengu!”
Mwenyezi-Mungu ni mwema, yeye ni ngome ya usalama wakati wa taabu. Yeye huwalinda wote wanaokimbilia usalama kwake.
Katika taabu yangu nilimwita Mwenyezi-Mungu, nilimlilia Mungu wangu anisaidie. Aliisikia sauti yangu hekaluni mwake; kilio changu kilimfikia masikioni mwake.
“Nawaachieni amani; nawapeni amani yangu. Siwapi nyinyi kama vile ulimwengu ufanyavyo. Msiwe na wasiwasi, wala msifadhaike.
Ee Mungu Mkuu, hofu inaponishika, mimi nakutumainia wewe.
Namtumainia Mungu na kusifu neno lake; namtumainia Mungu, wala siogopi. Binadamu dhaifu atanifanya nini?
Mbona nasononeka hivyo moyoni? Kwa nini nahangaika hivyo? Nitamtumainia Mungu, maana nitamsifu tena Mungu, aliye msaada wangu na Mungu wangu.
Mwenyezi-Mungu ni mwanga wangu na wokovu wangu, ni nani nitakayemwogopa? Mwenyezi-Mungu ni ngome ya maisha yangu, sitamwogopa mtu yeyote.
“Tazama, mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa watu wote. Hakuna lolote linaloweza kunishinda.
Mungu ni kimbilio letu na nguvu yetu; yeye ni msaada wetu daima wakati wa taabu.
Asema: “Nyamazeni na kujua kuwa mimi ni Mungu! Mimi natukuka katika mataifa yote; mimi natukuzwa ulimwenguni kote!”
Mwenyezi-Mungu wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni kimbilio letu.
Kwa hiyo hatutaogopa chochote, dunia ijapoyeyuka na milima kutikisika kutoka baharini;
Maana ninajua hakika kwamba hakuna kitu kiwezacho kututenganisha na upendo wake: Wala kifo, wala uhai; wala malaika au nguvu nyingine za mbinguni; wala yanayotokea sasa, wala yatakayotokea baadaye; wala mamlaka;
wala ulimwengu wa juu, wala wa chini kabisa. Hakuna kiumbe chochote kitakachoweza kututenga na upendo wa Mungu katika Kristo Yesu Bwana wetu.
Lakini mimi namlilia Mungu, naye Mwenyezi-Mungu ataniokoa.
Jioni, asubuhi na adhuhuri, nalalama na kulia, naye ataisikia sauti yangu.
Atanikomboa salama katika vita ninayoikabili, kwa maana maadui zangu ni wengi.
Basi, usiogope, mimi nipo pamoja nawe. Usifadhaike, mimi ni Mungu wako. Nitakuimarisha na kukusaidia; nitakulinda kwa mkono wangu wa ushindi.
Namngojea Mungu peke yake kwa utulivu; kwake naliweka tumaini langu.
Yeye peke yake ndiye mwamba na wokovu wangu, yeye ni ngome yangu, sitatikisika.
Kwa maana Roho tuliyepewa na Mungu si wa kutufanya tuwe waoga; sivyo, ila ni Roho wa kutujalia upendo na nidhamu.
Mwenyezi-Mungu ndiye anayewaongoza; yeye atakuwa pamoja nanyi; yeye hataacha kuwasaidia na hatawatupa. Hivyo, msiogope wala msifadhaike.”
Enyi wafungwa wenye tumaini; rudini kwenye ngome yenu. Sasa mimi ninawatangazieni: Nitawarudishieni mema maradufu.
Nagaagaa chini mavumbini; unipe tena uhai kama ulivyoahidi.
Nimeungama niliyotenda, nawe ukanijibu; unifundishe masharti yako.
Namsifu Mwenyezi-Mungu kwa kuniongoza, usiku dhamiri yangu yanionya.
Namweka Mwenyezi-Mungu mbele yangu daima; yuko pamoja nami, wala sitatikisika.
Wanaopanda kwa machozi, watavuna kwa shangwe.
Wanaokwenda kupanda mbegu wakilia, watarudi kwa furaha wakichukua mavuno.
Tuzingatie kabisa tumaini letu tunalokiri, maana Mungu aliyefanya ahadi zake ni mwaminifu.
Enyi watu, mtumainieni Mungu daima; mfungulieni Bwana yaliyo moyoni mwenu. Mungu ndiye kimbilio la usalama wetu.
Furahini kuhusu jambo hilo, ijapokuwa sasa, kwa kitambo kidogo, itawabidi kuhuzunika kwa sababu ya majaribio mbalimbali mnayoteseka,
Lakini wote wanaomtumainia Mwenyezi-Mungu, watapata nguvu mpya. Watapanda juu kwa mabawa kama tai; watakimbia bila kuchoka; watatembea bila kulegea.
Mkipita katika mafuriko, mimi nitakuwa pamoja nanyi; mkipita katika mito, haitawashinda nguvu. Mkitembea katika moto, hamtaunguzwa; mwali wa moto hautawaunguza.
Maana, mimi Mwenyezi-Mungu ninajua mambo niliyowapangia. Nimewapangieni mema na si mabaya, ili mpate kuwa na tumaini la baadaye.
Naam, si hayo tu, bali tunafurahi pia katika taabu tukijua kwamba taabu huleta saburi,
nayo saburi huleta uthabiti, na uthabiti huleta tumaini.
Tumaini hilo haliwezi kutuhadaa, maana Mungu amekwisha mimina mioyoni mwetu upendo wake kwa njia ya Roho Mtakatifu aliyetujalia.
Basi, Mungu aliye msingi wa matumaini, awajazeni furaha yote na amani kutokana na imani yenu; tumaini lenu lipate kuongezeka kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.
Kwa sababu hiyo hatufi moyo; na hata kama maumbile yetu ya nje yataoza, lakini kwa ndani tunafanywa wapya siku kwa siku.
Taabu tunayopata ni kidogo, tena ya muda tu; lakini itatupatia utukufu upitao matazamio yote, utukufu ambao hauna mwisho.
Hivyo tunatazamia kwa makini si vitu vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Maana vinavyoonekana ni vya muda tu; lakini vile visivyoonekana ni vya milele.
Tunalo tumaini hilo kama nanga ya maisha yetu. Tumaini hilo lapenya mpaka mahali patakatifu mbinguni.
Lakini nakumbuka jambo hili moja, nami ninalo tumaini:
Kwamba fadhili za Mwenyezi-Mungu hazikomi, huruma zake hazina mwisho.
Kila kunapokucha ni mpya kabisa, uaminifu wake ni mkuu mno.
Njoni kwangu nyinyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
Jifungeni nira yangu, mkajifunze kwangu, maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtatulizwa rohoni mwenu.
wamwulize: “Je, wewe ni yule anayekuja, au tumngoje mwingine?”
Maana, nira niwapayo mimi ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”
Asifiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa huruma yake kuu alitufanya tuzaliwe upya kwa kumfufua Yesu kutoka kwa wafu. Ametujalia tumaini lenye uhai,
Heri mtu anayesaidiwa na Mungu wa Yakobo, mtu aliyeweka tumaini lake kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wake,
Ndivyo ilivyo hekima nafsini mwako; ukiipata utakuwa na matazamio mema, wala tumaini lako halitakuwa la bure.
Natazama juu milimani; msaada wangu utatoka wapi?
Msaada wangu watoka kwa Mwenyezi-Mungu, aliyeumba mbingu na dunia.
Msiwe na wasiwasi juu ya kitu chochote, ila kwa kila hali, mwombeni Mungu katika sala juu ya mahitaji yenu, kwa shukrani.
Nayo amani ya Mungu ipitayo akili zote za watu italinda salama mioyo na akili zenu katika kuungana na Kristo Yesu.
Mungu ametaka kuwajulisha hao jinsi siri hiyo ilivyo kuu na tukufu ambayo imeenea kwa watu wa mataifa, nayo ndiyo hii: Kristo yuko ndani yenu, na jambo hilo lamaanisha kwamba nyinyi mtaushiriki utukufu wa Mungu.
Kwake yeye ambaye kwa nguvu yake ifanyayo kazi ndani yetu aweza kufanya mambo makuu zaidi ya yale tuwezayo kuomba au kufikiria;
kwake Mungu uwe utukufu katika kanisa na katika Kristo Yesu, nyakati zote, milele na milele! Amina.
Tunajua kwamba, katika mambo yote, Mungu hufanya kazi na kuifanikisha pamoja na wote wampendao, yaani wale aliowaita kadiri ya kusudi lake.
Naamini nitauona wema wake Mwenyezi-Mungu katika makao ya walio hai.
Mtegemee Mwenyezi-Mungu! Uwe na moyo, usikate tamaa! Naam, mtegemee Mwenyezi-Mungu!
Basi, nina hakika kwamba Mungu aliyeanza kazi hii njema ndani yenu, ataiendeleza mpaka ikamilike katika siku ile ya Kristo Yesu.