Mathayo 10 - Swahili Revised Union VersionWanafunzi kumi na wawili 1 Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. 2 Na majina ya hao mitume kumi na wawili ni haya; Wa kwanza Simoni aliyeitwa Petro, na Andrea nduguye; Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye; 3 Filipo, na Bartholomayo; Tomaso, na Mathayo mtoza ushuru; Yakobo wa Alfayo, na Thadayo; 4 Simoni Mkananayo, na Yuda Iskarioti, naye ndiye aliyemsaliti. Wajibu wa hao kumi na wawili 5 Hao Kumi na Wawili Yesu aliwatuma, akawaagiza, akisema, Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wowote wa Wasamaria msiingie. 6 Bali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. 7 Na katika kuenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia. 8 Ponyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure. 9 Msichukue dhahabu, wala fedha, wala pesa mishipini mwenu; 10 wala mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala viatu, wala fimbo; maana mfanyakazi astahili posho yake. 11 Na mji wowote au kijiji chochote mtakachoingia, tafuteni ni nani humo aliye mtu mwaminifu; mkae kwake hadi mtakapotoka. 12 Nanyi mkiingia katika nyumba isalimuni. 13 Na nyumba ile ikistahili, amani yenu na iifikie; la, kwamba haistahili, amani yenu na iwarudie ninyi. 14 Na mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo katika nyumba ile, au mji ule, kung'uteni mavumbi ya miguuni mwenu. 15 Amin, nawaambia, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma na Gomora kustahimili adhabu ya siku ya hukumu, kuliko mji ule. Mateso yajayo 16 Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwamwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua. 17 Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka mabarazani, na katika masinagogi yao watawapiga; 18 nanyi mtachukuliwa mbele ya watawala na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa. 19 Lakini hapo watakapowapeleka, msifikirifikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. 20 Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu. 21 Na ndugu atamsaliti nduguye ili auawe, na baba atamsaliti mwana, na wana watawainukia wazazi wao, na kuwaua. 22 Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. 23 Lakini watakapowafukuza katika mji huu, kimbilieni mwingine; kwa maana ni kweli nawaambia, Hamtaimaliza miji ya Israeli, hata ajapo Mwana wa Adamu. 24 Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, wala mtumwa hampiti bwana wake. 25 Yamtosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumwa kuwa kama bwana wake. Ikiwa wamemwita mwenye nyumba Beelzebuli, je! Si zaidi wale walio wa nyumbani mwake? Astahiliye kuogopewa 26 Basi, msiwaogope, kwa maana hakuna neno lililositirika, ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa, ambalo halitajulikana. 27 Niwaambialo ninyi katika giza, lisemeni katika nuru; na msikialo kwa siri, lihubirini juu ya nyumba. 28 Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika Jehanamu. 29 Je! Mashomoro wawili hawauzwi kwa senti moja? Wala hata mmoja haanguki chini asipojua Baba yenu; 30 lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. 31 Msiogope basi; bora ninyi kuliko mashomoro wengi. 32 Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni. 33 Bali mtu yeyote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Si Amani, bali upanga 34 Msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani; la! Sikuja kuleta amani, bali upanga. 35 Kwa maana nilikuja kumfitini mtu na babaye, na binti na mamaye, na mkwe na mkwe mtu; 36 na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake. 37 Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili. 38 Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili. 39 Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona. Thawabu 40 Awapokeaye ninyi, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi, ampokea yeye aliyenituma. 41 Ampokeaye nabii kwa kuwa ni nabii, atapata thawabu ya nabii; naye ampokeaye mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki, atapata thawabu ya mwenye haki. 42 Na mtu awaye yote atakayemnywesha mmojawapo wa wadogo hawa angaa kikombe cha maji baridi, kwa kuwa ni mwanafunzi, amin, nawaambia, haitampotea kamwe thawabu yake. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya