Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Marko 8 - Swahili Revised Union Version


Kuwalisha watu elfu nne

1 Katika siku zile, kwa vile ulivyokuwa mkuu tena ule mkutano, nao wamekosa kitu cha kula, akawaita wanafunzi wake, akawaambia,

2 Nawahurumia mkutano kwa sababu yapata siku tatu wamekaa nami, wala hawana kitu cha kula;

3 nami nikiwaaga waende zao nyumbani kwao wakiwa na njaa, watazimia njiani; na baadhi yao wametoka mbali.

4 Wanafunzi wake wakamjibu, Je! Ataweza wapi mtu kuwashibisha hawa mikate hapa nyikani?

5 Akawauliza, Mnayo mikate mingapi? Wakasema, Saba,

6 Akawaagiza mkutano waketi chini; akaitwaa ile mikate saba, akashukuru, akaimega, akawapa wanafunzi wake wawaandalie; wakawaandalia mkutano.

7 Walikuwa na visamaki vichache; akavibariki, akasema wawagawie na hivyo pia.

8 Wakala, wakashiba, wakakusanya mabaki ya vipande vya mikate vikapu saba.

9 Na watu waliokula walikuwa elfu nne. Akawaaga.

10 Mara akapanda katika mashua pamoja na wanafunzi wake, akaenda pande za Dalmanutha.


Dai la ishara

11 Wakatokea Mafarisayo, wakaanza kuhojiana naye; wakitafuta kwake ishara itokayo mbinguni; wakimjaribu.

12 Akapiga kite rohoni mwake, akasema, Mbona kizazi hiki chatafuta ishara? Amin, nawaambieni, Hakitapewa ishara kizazi hiki.

13 Akawaacha, akapanda tena katika mashua, akaenda zake hadi ng'ambo.


Chachu ya Mafarisayo na ya Herode

14 Wakasahau kuchukua mikate, wala katika mashua hawana ila mkate mmoja tu.

15 Akawaagiza, akasema, Angalieni, jihadharini na chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode.

16 Wakabishana wao kwa wao, kwa kuwa hawana mikate.

17 Naye Yesu akatambua, akawaambia, Mbona mnabishana kwa sababu hamna mikate? Hamfahamu bado, wala hamjaelewa? Je! Mioyo yenu ni mizito?

18 Mna macho, hamwoni; mna masikio, hamsikii? Wala hamkumbuki?

19 Nilipoivunja ile mikate mitano na kuwapa wale elfu tano, mlichukua vikapu vingapi vimejaa vipande? Wakamwambia, Kumi na viwili.

20 Na ile saba kuwapa wale elfu nne, mlichukua vikapu vingapi vimejaa vipande? Wakamwambia, Saba.

21 Akawaambia, Hamjafahamu bado?


Yesu amponya kipofu Bethsaida

22 Wakafika Bethsaida, wakamletea kipofu, wakamsihi amguse.

23 Akamshika mkono yule kipofu, akamchukua nje ya kijiji, akamtemea mate katika macho, akamwekea mikono yake, akamwuliza, Waona kitu?

24 Akatazama juu, akasema, Naona watu kama miti, inakwenda.

25 Ndipo akaweka tena mikono yake juu ya macho yake, naye akatazama sana; akawa mzima, akaona vyote waziwazi.

26 Akamwagiza aende nyumbani kwake, akisema, Hata kijijini usiingie. Petro Amkiri Yesu kuwa Kristo.

27 Akatoka Yesu na wanafunzi wake, wakaenda kwenye vijiji vya Kaisaria-Filipi; na njiani akawauliza wanafunzi wake, akasema, Watu huninena mimi kuwa ni nani?

28 Wakamjibu, Yohana Mbatizaji; wengine, Eliya; wengine, Mmojawapo wa manabii.

29 Naye akawauliza, Na ninyi mnasema ya kuwa mimi ni nani? Petro akamjibu, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo.

30 Akawaonya wasimwambie mtu habari zake.


Yesu asema juu ya kufa na kufufuka kwake

31 Akaanza kuwafundisha kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupatikana na mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na baada ya siku tatu kufufuka.

32 Naye alikuwa akinena neno hilo waziwazi. Petro akamchukua, akaanza kumkemea.

33 Akageuka, akawatazama wanafunzi wake, akamkemea Petro, akasema, Nenda nyuma yangu, Shetani; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.

34 Akawaita mkutano pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, Mtu yeyote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate.

35 Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha.

36 Kwa kuwa itamfaidi mtu nini kuupata ulimwengu wote, akiipoteza nafsi yake?

37 Ama mtu atoe nini badala ya nafsi yake?

38 Maana kila mtu atakayenionea haya mimi, na maneno yangu, katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo