Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Hesabu 1 - Swahili Revised Union Version


Hesabu ya kwanza ya Waisraeli

1 BWANA akanena na Musa katika jangwa la Sinai, hemani mwa kukutania, siku ya kwanza ya mwezi wa pili, katika mwaka wa pili baada ya kutoka kwao nchi ya Misri, akamwambia,

2 Fanyeni hesabu ya watu wote wa Israeli, kwa kufuata jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina ilivyo, kila mwanamume mmoja mmoja;

3 kuanzia aliye na umri wa miaka ishirini na zaidi, wote wawezao kutoka kwenda vitani katika Israeli; wewe na Haruni mtawahesabu kwa kufuata majeshi yao.

4 Tena mwanamume mmoja wa kila kabila atakuwa pamoja nanyi; kila mmoja aliye kichwa cha nyumba ya baba zake.

5 Haya ndiyo majina ya wanaume watakaokusaidia; Wa Reubeni; Elisuri mwana wa Shedeuri.

6 Wa Simeoni; Shelumieli mwana wa Suri-shadai.

7 Wa Yuda; Nashoni mwana wa Aminadabu.

8 Wa Isakari; Nethaneli mwana wa Suari.

9 Wa Zabuloni; Eliabu mwana wa Heloni.

10 Katika wana wa Yusufu; wa Efraimu, Elishama mwana wa Amihudi; na wa Manase; Gamalieli mwana wa Pedasuri.

11 Wa Benyamini Abidani mwana wa Gideoni.

12 Wa Dani; Ahiezeri mwana wa Amishadai.

13 Wa Asheri; Pagieli mwana wa Okirani.

14 Wa Gadi; Eliasafu mwana wa Deueli.

15 Wa Naftali; Ahira mwana wa Enani.

16 Hao ndio waliochaguliwa na mkutano, wakuu wa makabila ya baba zao; nao ndio vichwa vya wa wale maelfu ya Israeli.

17 Basi Musa na Haruni wakawatwaa watu hao, wanaume waliotajwa majina yao;

18 nao waliwakutanisha watu wote, siku ya kwanza ya mwezi wa pili, nao wakaonesha ukoo wa vizazi vyao kwa kufuata jamaa zao, kwa nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, kuanzia umri wa miaka ishirini na zaidi, mmoja mmoja.

19 Kama BWANA alivyomwagiza Musa, ndivyo alivyowahesabu huko katika jangwa la Sinai.

20 Na wana wa Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Israeli, vizazi vyao, kwa kufuata jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, kichwa kwa kichwa, kila mwanamume kuanzia umri wa miaka ishirini na zaidi wote walioweza kwenda vitani;

21 wale waliohesabiwa katika kabila la Reubeni, walikuwa watu elfu arubaini na sita na mia tano (46,500) mmoja mmoja.

22 Katika wana wa Simeoni, vizazi vyao, kwa kufuata jamaa zao, na nyumba za baba zao, wale waliohesabiwa kama hesabu ya majina, kichwa kwa kichwa, kila mwanaume kuanzia umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani;

23 wale waliohesabiwa katika kabila la Simeoni, walikuwa watu elfu hamsini na tisa na mia tatu (59,300).

24 Katika wana wa Gadi, kwa kufuata vizazi vyao, jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, kuanzia umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani;

25 wale waliohesabiwa katika kabila la Gadi, walikuwa watu elfu arubaini na tano, mia sita na hamsini (45,650).

26 Katika wana wa Yuda, vizazi vyao, kwa kufuata jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, kuanzia umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani;

27 wale waliohesabiwa katika kabila la Yuda, walikuwa watu elfu sabini na nne na mia sita (74,600).

28 Katika wana wa Isakari, vizazi vyao, kwa kufuata jamaa zao, na nyumba za baba zao, kwa hesabu ya majina, kuanzia umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani;

29 wale waliohesabiwa katika kabila la Isakari, walikuwa watu elfu hamsini na nne na mia nne (54,400).

30 Katika wana wa Zabuloni, vizazi vyao, kwa kufuata jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, kuanzia umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani;

31 wale waliohesabiwa katika kabila la Zabuloni, walikuwa watu elfu hamsini na saba na mia nne (57,400).

32 Katika wana wa Yusufu, maana katika wana wa Efraimu, vizazi vyao kwa kufuata jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, kuanzia umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani,

33 wale waliohesabiwa katika kabila la Efraimu, walikuwa watu elfu arubaini na mia tano (40,500).

34 Katika wana wa Manase, vizazi vyao, kwa kufuata jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, kuanzia umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani;

35 wale waliohesabiwa katika kabila la Manase, walikuwa watu elfu thelathini na mbili na mia mbili (32,200).

36 Katika wana wa Benyamini, vizazi vyao, kwa kufuata jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, kuanzia umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani;

37 wale waliohesabiwa katika kabila la Benyamini, walikuwa watu elfu thelathini na tano na mia nne (35,400).

38 Katika wana wa Dani, vizazi vyao, kwa kufuata jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, kuanzia umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani;

39 wale waliohesabiwa katika kabila la Dani, walikuwa watu elfu sitini na mbili na mia saba (62,700).

40 Katika wana wa Asheri, vizazi vyao, kwa kufuata jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, kuanzia umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani;

41 wale waliohesabiwa katika kabila la Asheri, walikuwa watu elfu arubaini na moja na mia tano (41,500).

42 Katika wana wa Naftali, vizazi vyao, kwa kufuata jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, kuanzia umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani;

43 wale waliohesabiwa katika kabila la Naftali, walikuwa watu elfu hamsini na tatu na mia nne (53,400).

44 Hao ndio waliohesabiwa, ambao Musa na Haruni na wale wakuu wa Israeli watu kumi na wawili waliwahesabu; walikuwa kila mmoja kwa ajili ya nyumba ya baba zake.

45 Basi hao wote waliohesabiwa katika wana wa Israeli kwa kufuata nyumba za baba zao kuanzia umri wa miaka ishirini na zaidi; wote walioweza kwenda vitani katika Israeli;

46 hao wote waliohesabiwa walikuwa ni wanaume elfu mia sita na tatu, mia tano na hamsini (603,550).

47 Lakini Walawi kwa kulifuata kabila la baba zao hawakuhesabiwa katika watu hao.

48 Kwa kuwa BWANA alinena na Musa, na kumwambia,

49 Hilo kabila la Lawi tu usilihesabu, wala usiitie hesabu yao katika wana wa Israeli;

50 lakini uwaweke Walawi wawe juu ya maskani ya ushahidi, na juu ya vyombo vyake vyote, na juu ya vitu vyake vyote; wao wataichukua hiyo maskani, na vyombo vyake vyote; nao wataitumikia, na kupanga hema zao kwa kuizunguka maskani pande zote.

51 Tena hapo maskani itakapokwenda mbele, Walawi wataishusha; tena hapo maskani itakaposimamishwa, Walawi wataisimamisha; na mgeni atakayekaribia atauawa.

52 Na wana wa Israeli watazipanga hema zao, kila mtu katika kambi yake mwenyewe, kila mtu hapo ilipo bendera yake mwenyewe, kama majeshi yao yalivyo.

53 Lakini Walawi watapanga hema zao kuizunguka maskani ya ushahidi pande zote, ili zisiwe hasira juu ya mkutano wa wana wa Israeli; kisha Walawi wahudumu katika hiyo Hema Takatifu.

54 Ndivyo walivyofanya wana wa Israeli; kama yote BWANA aliyomwagiza Musa, ndivyo walivyofanya.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo