Nahumu 3 - Swahili Revised Union VersionKuja kwa uharibifu usioepukika 1 Ole wake mji wa damu! Umejaa mambo ya uongo na unyang'anyi; mateka hayaondoki. 2 Kelele za mjeledi, kelele za magurudumu yafanyayo kishindo; na farasi wenye kuparapara, na magari ya vita yenye kurukaruka; 3 mpanda farasi akipanda, na upanga ukimetameta, na mkuki ukimeremeta; na wingi wa waliouawa, na rundo kubwa la mizoga; mizoga isiyo na mwisho; wanajikwaa juu ya mizoga yao. 4 Kwa sababu ya wingi wa ukahaba wa yule kahaba mzuri, yule bibi wa mambo ya uchawi, auzaye mataifa kwa ukahaba wake, na jamaa za watu kwa uchawi wake. 5 Tazama, mimi ni juu yako, asema BWANA wa majeshi; nami nitayainua marinda yako mbele ya uso wako; nami nitawaonesha mataifa uchi wako, na falme aibu yako. 6 Nami nitatupa uchafu uchukizao juu yako, kukufanya uwe mchafu, nami nitakufanya kuwa kitu cha kutazamwa kwa dharau. 7 Hata itakuwa, wote wakutazamao watakukimbia, wakisema, Ninawi umeharibika; ni nani atakayeuhurumia? Nikutafutie wapi wafariji? 8 Je! Wewe u mwema kuliko No-amoni, uliowekwa kati ya mito, uliozungukwa na maji; ambao boma lake lilikuwa bahari, na bahari ilikuwa ukuta wake. 9 Kushi na Misri walikuwa nguvu zake, nazo zilikuwa hazina mpaka; Puti na Walibya walikuwa wasaidizi wake. 10 Hata hivyo alichukuliwa mbali, alikwenda utumwani; watoto wake wachanga walisetwa kwenye maachano ya njia kuu zote; watu wake wenye heshima wakapigiwa kura, na wakuu wake wote wakafungwa kwa minyororo. 11 Tena utalewa, utafichwa; tena utatafuta ngome kwa sababu ya adui. 12 Ngome zako zote zitakuwa kama mitini yenye tini zilizoiva kwanza; ikitikisika zaanguka katika kinywa chake alaye. 13 Tazama, watu wako walio ndani yako ni wanawake; malango ya nchi yako yamekuwa wazi kabisa mbele ya adui zako; moto umeteketeza mapingo yako. 14 Teka maji yawe tayari kwa kuzingirwa kwako; Zitie nguvu ngome zako; Ingia katika udongo, yakanyage matope, Itie nguvu tanuri ya kuokea matofali. 15 Huko moto utakuteketeza; Upanga utakukatilia mbali; Utakumeza kama tunutu alavyo; Jifanye kuwa wengi kama tunutu! Jifanye kuwa wengi kama nzige! 16 Umeongeza wafanya biashara wako kuwa wengi kuliko nyota za mbinguni; tunutu huharibu; kisha huruka juu na kwenda zake. 17 Watu wako waliotiwa taji ni kama nzige, na majemadari wako ni kama makundi ya mapanzi, watuao katika vitalu siku ya baridi, lakini jua lipandapo huruka juu na kwenda zao, wala hapana ajuaye walikokwenda. 18 Wachungaji wako wanalala usingizi, Ee mfalme wa Ashuru; watu wako wenye heshima wamepumzika; watu wako wametawanyika juu ya milima, wala hapana mtu wa kuwakusanya. 19 Jeraha lako halipunguziki; donda lako haliponyeki; wote wasikiao habari zako wapiga makofi juu yako; kwa maana ni nani aliyewahi kuukwepa ukatili wako usio na mwisho? |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya