Mwanzo 39 - Swahili Revised Union VersionYusufu na mke wa Potifa 1 Basi Yusufu akaletwa mpaka Misri, naye Potifa, ofisa wa Farao, mkuu wa askari walinzi, mtu wa Misri, akamnunua mkononi mwa hao Waishmaeli waliomleta huko. 2 BWANA akawa pamoja na Yusufu, naye akasitawi; naye alikuwa katika nyumba ya bwana wake, yule Mmisri. 3 Bwana wake akaona ya kwamba BWANA yu pamoja naye, na ya kuwa BWANA anafanikisha mambo yote mkononi mwake. 4 Yusufu akaona neema machoni pake, akamtumikia. Naye akamweka kuwa msimamizi wa nyumba yake, na yote yaliyomo akayaweka mkononi mwake. 5 Ikawa tokea wakati alipomweka kuwa msimamizi wa nyumba yake, na vyote vilivyomo, BWANA akabariki nyumba ya yule Mmisri kwa ajili ya Yusufu. Baraka za BWANA zikawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba, na katika shamba. 6 Akayaacha yote aliyokuwa nayo mkononi mwa Yusufu; wala hakujua habari za kitu chochote chake, ila hicho chakula alichokula tu. Naye Yusufu alikuwa mtu mzuri, na mwenye uso mzuri. 7 Ikawa baada ya mambo hayo, mke wa bwana wake akamtamani Yusufu, akamwambia, Lala nami. 8 Lakini akakataa, akamwambia mke wa bwana wake, Tazama, bwana wangu hajui kitu kilichowekwa kwangu nyumbani, na vyote alivyo navyo amevitia mkononi mwangu. 9 Hakuna mkuu katika nyumba hii kuliko mimi, wala hakunizuilia kitu chochote ila wewe, kwa kuwa wewe u mkewe. Nifanyeje ubaya huu mkubwa nimkosee Mungu? 10 Akawa akizidi kusema na Yusufu siku baada ya siku, lakini hakumsikia alale naye, wala kuwa naye. 11 Ikawa, siku moja, akaingia nyumbani afanye kazi yake, na hapakuwa na mtu yeyote kati ya wale wa nyumbani karibu; 12 huyo mwanamke akamshika nguo zake, akisema, Lala nami. Yusufu akaiacha nguo yake mkononi mwake, akakimbia, akatoka nje. 13 Ikawa alipoona ya kwamba amemwachilia nguo yake mkononi mwake, naye amekimbia nje, 14 akawaita watu wa nyumbani mwake, akasema nao, akinena, Angalieni, ametuletea mtu Mwebrania atufanyie dhihaka. Ameingia kwangu ili alale nami, nikalia kwa sauti kuu. 15 Ikawa, aliposikia ya kuwa nimepaza sauti yangu na kulia, aliiacha nguo yake kwangu, akakimbia, akatoka nje. 16 Basi akaiweka ile nguo kwake hata bwana wake aje nyumbani. 17 Naye akamwambia maneno yayo hayo, akisema, Yule mtumwa Mwebrania uliyemleta kwetu, aliingia kwangu anidhihaki. 18 Ikawa nilipopaza sauti yangu, nikalia, akaacha nguo yake kwangu akakimbia nje. 19 Ikawa bwana wake aliposikia maneno aliyoambia na mkewe, akisema, Mtumwa wako amenitendea mambo kama haya, hasira yake ikawaka. 20 Bwana wake akamtwaa Yusufu, akamtia gerezani, mahali wafungwa wa mfalme walimokuwa wamefungiwa, naye akawa humo gerezani. 21 Lakini BWANA akawa pamoja na Yusufu, akamfadhili, akampa kibali machoni pa mkuu wa gereza. 22 Mkuu wa gereza akawatia mkononi mwa Yusufu watu wote waliofungwa, waliokuwemo gerezani; na yote yaliyofanywa humo, yeye ndiye aliyeyafanya. 23 Wala mkuu wa gereza hakufuatilia kazi liliyokuwa mikononi mwa Yusufu; kwa kuwa BWANA alikuwa pamoja naye. BWANA akayafanikisha yote aliyoyafanya. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya