Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Mwanzo 42 - Swahili Revised Union Version


Ndugu zake Yusufu waenda Misri

1 Basi Yakobo akaona ya kuwa kuna nafaka katika Misri, Yakobo akawaambia wanawe, Kwa nini mnatazamana?

2 Akasema, Angalia, nimesikia ya kuwa kuna nafaka Misri; shukeni huko mkatununulie chakula, tupate kuishi wala tusife.

3 Basi ndugu kumi wa Yusufu wakashuka Misri ili wanunue nafaka.

4 Lakini Benyamini, ndugu wa Yusufu, Yakobo hakumpeleka pamoja na ndugu zake, maana alisema, Mabaya yasimpate.

5 Wana wa Israeli wakaja wanunue chakula miongoni mwao waliokuja, kwa kuwa kulikuwa na njaa katika nchi ya Kanaani.

6 Naye Yusufu alikuwa ni mkuu juu ya nchi, ndiye aliyewauzia watu wote wa nchi. Nao ndugu zake Yusufu wakaja, wakainama kifudifudi mbele yake.

7 Yusufu akawaona nduguze, akawatambua, lakini alijifanya kama mgeni kwao. Akasema nao kwa maneno makali, akawaambia, Mmetoka wapi ninyi? Wakasema. Tumetoka nchi ya Kanaani, ili tununue chakula.

8 Yusufu akawatambua nduguze, bali wao hawakumtambua yeye.

9 Yusufu akazikumbuka zile ndoto alizowaotea. Akawaambia, Wapelelezi ninyi, mmekuja ili mwuone utupu wa nchi.

10 Wakamwambia, Hasha, bwana, watumwa wako tumekuja ili tununue chakula.

11 Sisi sote ni wana wa mtu mmoja tu watu wa kweli sisi; watumwa wako si wapelelezi.

12 Akawaambia, Sivyo, mmekuja ili mwuone utupu wa nchi.

13 Wakamwambia, Sisi watumwa wako tu ndugu kumi na wawili, wana wa mtu mmoja katika nchi ya Kanaani; na mdogo wetu yuko pamoja na baba yetu leo, na mmoja hayuko.

14 Yusufu akawaambia, Ndivyo nilivyowaambia, nikisema, Wapelelezi ninyi.

15 Mtabainika kwa njia hii; aishivyo Farao, hamtoki hapa, asipokuja huku huyo ndugu yenu mdogo.

16 Mtumeni mmoja wenu, aende akamlete ndugu yenu, na ninyi mtafungwa jela, hadi maneno yenu yahakikishwe kama mna kweli ninyi; ikiwa sivyo, aishivyo Farao hakika ninyi ni wapelelezi.

17 Akawatia wote gerezani siku tatu.

18 Siku ya tatu, Yusufu akawaambia, Fanyeni hivi, mkaishi, maana mimi namcha Mungu.

19 Kama ninyi ni wa kweli, mmoja wenu na afungwe gerezani, nanyi mwende mkachukue nafaka kwa ajili ya njaa ya nyumba zenu,

20 mkamlete ndugu yenu mdogo kwangu; hivyo maneno yenu yatahakikishwa, wala hamtakufa. Ndivyo walivyofanya.

21 Wakaambiana, Kweli sisi tulimkosea ndugu yetu, kwa kuwa tuliona shida ya roho yake, alipotusihi, wala hatukusikia, kwa hiyo shida hii imetupata.

22 Reubeni akajibu, akawaambia, Sikuwaambia, nikisema, Msimkosee kijana? Wala hamkusikia; kwa hiyo tunadaiwa damu yake.

23 Wala hawakujua ya kwamba Yusufu anawasikia, kwa sababu alizungumza nao kupitia kwa mkalimani.

24 Akaenda kando, akalia. Kisha akawarudia, na kusema nao, akamtwaa Simeoni miongoni mwao, akamfunga mbele ya macho yao.

25 Yusufu akaamuru kuvijaza vyombo vyao nafaka, na kumrudishia kila mtu fedha yake katika gunia lake, na kuwapa chakula cha njiani. Na hivyo ndivyo walivyofanyiwa.


Ndugu zake Yusufu warudi Kanaani

26 Wakawatwika punda wao nafaka yao, wakatoka huko.

27 Mmoja wao alipofungua gunia lake ili ampe punda wake chakula katika nyumba ya wageni, aliiona fedha yake; kumbe! Iko kinywani mwa gunia lake.

28 Akawaambia nduguze, Fedha yangu imerudishwa, angalia, imo humo guniani mwangu. Mioyo yao ikazimia, wakageukiana wakitetemeka, wakasema, Ni nini hii Mungu aliyotutendea?

29 Wakaja kwa Yakobo, baba yao, katika nchi ya Kanaani, wakampasha habari za yote yaliyowapata, wakisema,

30 Mtu yule aliye bwana wa nchi alisema nasi kwa maneno makali, akatufanya tu wapelelezi wa nchi.

31 Tukamwambia, Tu watu wa kweli sisi, wala si wapelelezi.

32 Sisi tu ndugu kumi na wawili, wana wa baba yetu. Mmoja hayuko, na mdogo wetu yuko pamoja na baba yetu leo katika nchi ya Kanaani.

33 Yule mtu, bwana wa nchi, akatuambia, Kwa njia hii nitawajua kama ninyi ni watu wa kweli; ndugu yenu mmoja mwacheni huku kwangu, kachukueni nafaka kwa njaa ya nyumba zenu, mwende zenu.

34 Mkaniletee ndugu yenu mdogo; ndipo nitakapojua kama ninyi si wapelelezi, bali ni watu wa kweli; basi nitawarudishia ndugu yenu, nanyi mtafanya biashara katika nchi hii.

35 Ikawa walipomimina magunia yao, kumbe! Bahasha ya fedha ya kila mtu imo katika gunia lake. Nao walipoziona bahasha za fedha zao, wao na baba yao waliogopa.

36 Yakobo baba yao akawaambia, Mmeniondolea watoto wangu; Yusufu hayuko, wala Simeoni hayuko, na Benyamini mnataka kumchukua naye; mambo hayo yote yamenipata mimi.

37 Reubeni akamwambia baba yake, akasema, Uwaue wanangu wawili nisipomrudisha kwako; mtie katika mikono yangu, nami nitamrudisha kwako.

38 Akasema, Mwanangu hatashuka pamoja nanyi, maana nduguye amekufa, naye amesalia peke yake; mabaya yakimpata katika njia mtakayoiendea ndipo mtakaposhusha mvi zangu kwa sikitiko mpaka kaburini.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo