Mwanzo 18 - Swahili Revised Union VersionAbrahamu na Sara waahidiwa mtoto 1 BWANA akamtokea Abrahamu karibu na mialoni ya Mamre, alipokuwa ameketi mlangoni pa hema yake mchana wakati wa joto. 2 Akainua macho yake akaona, na tazama, watu watatu wamesimama mbele yake. Naye alipowaona alipiga mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema, akainama mpaka chini, 3 akasema, Bwana wangu, kama nimeona fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa mimi mtumwa wako. 4 Na yaletwe basi maji kidogo mkanawe miguu, mkapumzike chini ya mti huu. 5 Nami nitaleta chakula kidogo, mkaburudishe moyo, baadaye mwendelee, kwa maana mmemjia mtumwa wenu. Wakasema, Haya, fanya kama ulivyosema. 6 Basi Abrahamu akaenda hima hemani kwa Sara, akasema, Tayarisha haraka vipimo vitatu vya unga safi, uukande, ufanye mikate. 7 Abrahamu akapiga mbio kwenda kundini, akaleta ndama wa ng'ombe aliye laini, mzuri, akampa mtumishi, naye akaharakisha kuiandaa. 8 Akatwaa siagi na maziwa, na ndama aliyoiandaa, akawaandalia mbele yao, akasimama karibu nao chini ya mti, nao wakala. 9 Wakamwambia, Yu wapi Sara mkeo? Akasema, Yumo hemani. 10 Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume. Sara akasikia mlangoni pa hema iliyokuwapo nyuma yake. 11 Basi Abrahamu na Sara walikuwa wazee wenye umri mkubwa, na Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake. 12 Kwa hiyo Sara akacheka moyoni mwake, akisema, Niwapo mkongwe, nitapata furaha, na bwana wangu mzee? 13 BWANA akamwambia Abrahamu, Mbona Sara amecheka akisema, Mimi kweli nitazaa mwana, nami ni mzee? 14 Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda BWANA? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati huu huu mwakani, na Sara atapata mwana wa kiume. 15 Akakana Sara, akisema, Sikucheka, maana aliogopa. Naye akasema, Sivyo! Umecheka. Abrahamu aombea Sodoma 16 Kisha watu hao wakaondoka huko wakaelekeza nyuso zao Sodoma. Abrahamu akaenda pamoja nao awasindikize. 17 BWANA akasema, Je! Nimfiche Abrahamu jambo ambalo ninataka kulifanya, 18 ikiwa Abrahamu atakuwa taifa kuu, hodari, na katika yeye mataifa yote ya dunia watabarikiwa? 19 Kwa maana nimemchagua ili awaamuru wanawe na vizazi vyake baada yake wadumishe njia ya BWANA, kwa kuwa wenye haki na kweli, ili BWANA naye akamtimizie Abrahamu ahadi zake. 20 BWANA akasema, Kwa kuwa kilio cha Sodoma na Gomora kimezidi, na dhambi zao zimeongezeka sana, 21 basi, nitashuka sasa nione kama wanayotenda ni kiasi cha kilio kilichonijia; na kama sivyo, nitajua. 22 Basi wale watu wakatoka huko wakaelekea Sodoma; lakini Abrahamu alibaki amesimama mbele za BWANA. 23 Abrahamu akakaribia, akasema, Je! Utaharibu mwenye haki pamoja na mwovu? 24 Huenda wakawapo wenye haki hamsini katika mji, utaharibu, wala hutauacha mji kwa ajili ya hao hamsini wenye haki waliomo? 25 La hasha! Usifanye hivyo, ukamwue mwenye haki pamoja na mwovu, mwenye haki awe kama mwovu. Hasha! Mhukumu ulimwengu wote asitende haki? 26 BWANA akasema, Nikiona katika Sodoma wenye haki hamsini mjini, nitapaacha mahali pote kwa ajili yao. 27 Abrahamu akajibu, akasema, Basi, nimeshika kusema na Bwana, nami ni mavumbi na majivu tu. 28 Huenda wakapunguka watano katika wale hamsini wenye haki, je! Utaharibu mji wote kwa kupungua watano? Akasema, Sitauharibu, nikiona humo arubaini na watano. 29 Akazidi tena kusema naye, akinena, Huenda wakaonekana humo arubaini? Akasema, Sitafanya kwa ajili ya hao arubaini. 30 Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema, Huenda wakaonekana huko thelathini? Akasema, Sitafanya, nikiona humo thelathini. 31 Akasema, Tazama, nimeshika kusema na Bwana, huenda wakaonekana huko ishirini? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao ishirini. 32 Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema mara hii tu, Huenda wakaonekana huko kumi? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao kumi. 33 Basi BWANA alipokwisha kuzungumza na Abrahamu, akaenda zake; Abrahamu naye akarudi mahali pake. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya