Mathayo 15 - Swahili Revised Union VersionMapokeo ya wazee 1 Ndipo Mafarisayo na waandishi toka Yerusalemu walipomwendea Yesu wakisema, 2 Mbona wanafunzi wako huyavunja mapokeo ya wazee, kwa maana hawanawi mikono walapo chakula. 3 Akajibu, akawaambia, Mbona ninyi nanyi huivunja amri ya Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu? 4 Kwa kuwa Mungu alisema, Mheshimu baba yako na mama yako, na Amtukanaye baba yake au mama yake kufa na afe. 5 Bali ninyi husema, Atakayemwambia babaye au mamaye, chochote kikupasacho nikusaidie kwacho nakitoa wakfu, 6 basi asimheshimu baba yake au mama yake. Mkalitangua neno la Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu. 7 Enyi wanafiki, ni vema alivyotabiri Isaya kwa habari zenu, akisema, 8 Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami. 9 Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu. Mambo yatiayo unajisi 10 Akawaita makutano akawaambia 11 Sikilizeni, mfahamu; Sicho kiingiacho kinywani kimtiacho mtu unajisi; bali kitokacho kinywani ndicho kimtiacho mtu unajisi. 12 Ndipo wanafunzi wake walipomwendea, wakamwambia, Wajua ya kuwa Mafarisayo walipolisikia neno lile walichukizwa? 13 Akajibu, akasema, Kila pando asilolipanda Baba yangu wa mbinguni litang'olewa. 14 Waacheni; hao ni viongozi vipofu wa vipofu. Na kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, watatumbukia shimoni wote wawili. 15 Basi Petro akajibu, akamwambia, Tueleze mfano huo. 16 Yesu akasema, Hata sasa ninyi nanyi mngali hamna akili? 17 Hamjafahamu bado ya kuwa kila kiingiacho kinywani hupita tumboni, kikatupwa chooni? 18 Bali vitokavyo kinywani vyatoka moyoni; navyo ndivyo vimtiavyo mtu unajisi. 19 Kwa maana moyoni hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati; wizi, ushuhuda wa uongo, na matukano; 20 hayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi; lakini kula kabla hajanawa mikono hakumtii mtu unajisi. Imani ya mwanamke Mkanaani 21 Yesu akaondoka huko, akaenda kando pande za Tiro na Sidoni. 22 Na tazama, mwanamke Mkanaani wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo. 23 Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa kuwa anaendelea kutupigia makelele nyuma yetu. 24 Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. 25 Naye akaja akamsujudia, akisema Bwana, unisaidie. 26 Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa. 27 Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao. 28 Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile. Yesu awaponya watu wengi 29 Yesu akaondoka huko, akafika kando ya bahari ya Galilaya; akapanda mlimani, akaketi huko. 30 Wakamwendea makutano mengi wakimletea viwete, vipofu, mabubu, vilema, na wengine wengi, wakawaweka miguuni pake; akawaponya; 31 hata ule mkutano wakastaajabu, walipowaona mabubu wanasema, vilema wanakuwa wazima, viwete wanakwenda, na vipofu wanaona; wakamtukuza Mungu wa Israeli. Kulishwa kwa watu elfu nne 32 Yesu akawaita wanafunzi wake, akasema, Nawahurumia mkutano, kwa kuwa yapata siku tatu wamekaa pamoja nami, wala hawana kitu cha kula, tena sitaki kuwaaga wakiwa na njaa, wasije wakazimia njiani. 33 Wanafunzi wake wakamwambia, Tupate wapi mikate mingi hapa nyikani, hata kushibisha mkutano mkuu namna hii? 34 Yesu akawaambia, Mnayo mikate mingapi? Wakasema, Saba, na visamaki vichache. 35 Akawaagiza mkutano waketi chini; 36 akaitwaa ile mikate saba na vile visamaki, akashukuru akavimega, akawapa wanafunzi wake, nao wanafunzi wakawapa makutano. 37 Wakala wote wakashiba; wakayaokota mabaki ya vipande vya mikate makanda saba, yamejaa. 38 Nao waliokula walikuwa wanaume elfu nne, bila kuhesabu wanawake na watoto. 39 Akawaaga makutano, akapanda katika mashua, akaenda pande za Magadani. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya