Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Yoshua 22 - Swahili Revised Union Version


Makabila ya mashariki warudi katika nchi zao

1 Wakati huo Yoshua akawaita Wareubeni, na Wagadi, na hiyo nusu ya kabila la Manase,

2 naye akawaambia, Ninyi mmeyafuata hayo yote mliyoamriwa na Musa, mtumishi wa BWANA, nanyi mmeisikia sauti yangu katika yote niliyowaamuru mimi;

3 hamkuwaacha hao ndugu zenu siku hizi nyingi hata hivi leo, lakini mmeyashika maagizo ya amri ya BWANA, Mungu wenu.

4 Na sasa yeye BWANA, Mungu wenu, amewapa ndugu zenu kustarehe, kama alivyowaambia; basi sasa rudini ninyi mwende mahemani kwenu, hata nchi ya milki yenu, ambayo huyo Musa, mtumishi wa BWANA, aliwapa ng'ambo ya pili ya Yordani.

5 Lakini mjibidiishe sana kuzifanya amri na sheria, ambazo Musa, mtumishi wa BWANA, aliwaamuru, kumpenda BWANA, Mungu wenu, na kwenenda katika njia zake zote, na kuzishika amri zake, na kushikamana na yeye, na kumtumikia kwa moyo wenu wote na nafsi yenu yote.

6 Basi Yoshua akawabariki, na kuwapa ruhusa waende zao; nao wakaenda mahemani kwao.

7 Basi Musa alikuwa amewapa hiyo nusu moja ya kabila la Manase urithi katika Bashani; lakini hiyo nusu ya pili Yoshua aliwapa urithi kati ya ndugu zao, ng'ambo ya Yordani upande wa kuelekea magharibi. Zaidi ya hayo Yoshua, hapo alipowaruhusu waende zao mahemani kwao, akawabariki,

8 kisha akanena nao, na kuwaambia, Rudini na mali mengi mahemani kwenu, na ng'ombe wengi sana, na fedha, na dhahabu, na shaba, na chuma, na mavazi mengi sana; mgawane na ndugu zenu hizo nyara za adui zenu.

9 Basi wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila la Manase wakarudi, wakatoka kwa wana wa Israeli katika Shilo, ulioko nchi ya Kanaani, ili waende nchi ya Gileadi, hiyo nchi ya milki yao, waliyokuwa wanaimiliki, sawasawa na amri ya BWANA kwa mkono wa Musa.


Madhabahu ya ukumbusho

10 Nao walipofika pande za Yordani zilizo katika nchi ya Kanaani, hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na nusu ya kabila la Manase, wakajenga madhabahu huko karibu na Yordani, iliyoonekana kuwa ni madhabahu kubwa.

11 Wana wa Israeli walisikia ikinenwa, Tazama, wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila la Manase, wamejenga madhabahu huko upande wa mbele wa nchi ya Kanaani, katika nchi iliyo karibu na Yordani, kwa upande huo ulio milki ya wana wa Israeli.

12 Basi, wana wa Israeli waliposikia habari hiyo, mkutano wote wa wana wa Israeli wakakutanika pamoja huko Shilo, ili waende kupigana nao.

13 Kisha wana wa Israeli wakatuma wajumbe waende kwa wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila la Manase, hadi nchi ya Gileadi; nao ni hawa, Finehasi mwana wa Eleazari kuhani;

14 na pamoja naye wakuu kumi, mkuu mmoja wa nyumba ya mababa kutoka kwa kila kabila la Israeli; nao kila mmoja alikuwa ni kichwa cha nyumba ya mababa katika maelfu ya Israeli.

15 Nao wakawafikia hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila la Manase, katika nchi ya Gileadi, na wakasema nao, wakinena,

16 Mkutano wote wa BWANA wanena, Ni kosa gani hili mlilolikosa juu ya Mungu wa Israeli, hata mkakengeuka hivi leo na kuacha kumfuata BWANA, katika kujijengea madhabahu, na kuasi hivi leo juu ya BWANA?

17 Je! Ule uovu wa Peori haututoshi, ambao hamjajitakasa nafsi zenu katika huo hata hivi leo, ijapokuwa ilikuja tauni juu ya mkutano wa BWANA,

18 hata ikawa hamna budi hivi leo kugeuka na kuacha kumfuata BWANA? Kisha itakuwa, kwa kuwa ninyi mnamwasi BWANA hivi leo, kwamba kesho yeye atakasirika na mkutano wote wa Israeli.

19 Basi ikiwa hiyo inchi yenu ni najisi, vukeni na kuingia katika nchi ya milki yake BWANA, ambamo maskani ya BWANA inakaa ndani yake, nanyi twaeni milki kati yetu; lakini msimwasi BWANA, wala msituasi sisi, kwa kujijengea madhabahu zaidi ya hiyo madhabahu ya BWANA, Mungu wetu.

20 Je! Huyo Akani mwana wa Zera hakukosa katika vile vitu vilivyowekwa wakfu, na hasira ikauangukia mkutano wote wa Israeli? Kisha mtu huyo hakuangamia peke yake katika uovu wake?

21 Ndipo hapo wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila la Manase, wakajibu, na kuwaambia hao waliokuwa ni vichwa vya maelfu ya Israeli, wakasema,

22 Mungu, Mungu BWANA, naam, Mungu, Mungu BWANA, yeye anajua, na Israeli naye atajua; kama ni katika uasi, au kama ni katika kosa juu ya BWANA, usituokoe hivi leo;

23 kama tumejijengea madhabahu ili kukengeuka na kuacha kumfuata BWANA; au kama ni kusongeza juu yake sadaka ya kuteketezwa, au sadaka ya unga, au kama ni kusongeza sadaka za amani juu yake, yeye BWANA mwenyewe na atulipize kisasi;

24 au kama sisi tumefanya jambo hili kwa hofu kuwa, katika siku zijazo wana wenu huenda wakanena na wana wetu na kusema, Ninyi mna uhusiano gani na BWANA, Mungu wa Israeli?

25 Kwa kuwa yeye BWANA ameufanya huu mto wa Yordani uwe mpaka katikati yetu nanyi, enyi wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, hamna fungu katika BWANA; basi hivyo wana wenu wangeweza kuwafanya wana wetu waache kumwabudu BWANA.

26 Kwa ajili ya hayo tulisema, Natujijengee madhabahu, si kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, wala kwa sadaka yoyote;

27 bali iwe ushahidi kati yetu nanyi, tena kati ya vizazi vyetu baada yetu, kwamba sisi tunamhudumia BWANA kwa njia ya sadaka zetu za kuteketezwa, na kwa dhabihu zetu, na kwa sadaka zetu za amani; ili kwamba wana wenu wasiwaambie wana wetu katika siku zijazo, Ninyi hamna fungu katika BWANA.

28 Kwa hiyo tulisema, Itakuwa, hapo watakapotuambia neno kama hilo, au kuwaambia watu wa vizazi vyetu katika siku zijazo neno kama hilo, ndipo sisi tutawaambia, Angalieni huu mfano wa madhabahu ya BWANA, walioufanya baba zetu, si kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, wala kwa ajili ya dhabihu; lakini ni ushahidi kati yetu nanyi.

29 Mungu na atuzuie tusimwasi BWANA, na kukengeuka hivi leo na kuacha kumfuata BWANA, hata mkajenga madhabahu kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, au sadaka za unga, au dhabihu, mbali na ile madhabahu ya BWANA, Mungu wetu, iliyo huko mbele ya maskani yake.

30 Basi Finehasi kuhani, na wakuu wa mkutano, na hao vichwa vya maelfu ya Israeli waliokuwa pamoja naye, hapo walipoyasikia hayo maneno waliyoyasema hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na wana wa Manase, maneno hayo yaliwaridhisha sana.

31 Naye Finehasi, mwana wa Eleazari, kuhani, akawaambia wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na wana wa Manase, akasema, Siku hii ya leo tumejua ya kwamba BWANA yu kati yetu, kwa sababu hamkukosa katika jambo hili mbele ya BWANA; sasa ninyi mmewaokoa wana wa Israeli na mkono wa BWANA.

32 Kisha Finehasi, mwana wa Eleazari, kuhani, na hao wakuu, wakarudi na kuwaacha wana wa Reubeni na wana wa Gadi, wakatoka katika nchi ya Gileadi, na kuingia nchi ya Kanaani; wakawarudia wana wa Israeli, wakawapa habari.

33 Ripoti hiyo ikawaridhisha Waisraeli; nao Waisraeli wakamhimidi Mungu, wala hawakusema tena habari ya kuwaendea ili kupigana nao, wala kuiharibu nchi waliyoikaa wana wa Reubeni, na wana wa Gadi.

34 Basi hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, wakaiita madhabahu hiyo Edi; wakasema, Kwa kuwa ni ushahidi kati yetu ya kwamba yeye BWANA ndiye Mungu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo