Yobu 3 - Swahili Revised Union VersionAyubu ailaani siku aliyozaliwa 1 Baada ya hayo Ayubu akafunua kinywa chake, na kuilaani siku yake. 2 Ayubu akajibu, na kusema; 3 Na ipotelee mbali ile siku niliyozaliwa mimi, Na ule usiku uliosema, Mtoto wa kiume ametungishwa mimba. 4 Siku hiyo na iwe giza; Mungu asiiangalie toka juu, Wala mwanga usiiangazie. 5 Ishikwe na giza, giza tupu, kuwa yake; Wingu na likae juu yake; Chote kiifanyacho siku kuwa giza na kiitishe. 6 Tena usiku huo, na ushikwe na giza kuu; Usihesabiwe katika siku za mwaka; Wala kutiwa katika hesabu ya miezi. 7 Tazama, usiku huo na uwe tasa; Wala isiwe ndani yake sauti ya shangwe. 8 Na waulaani hao waulaanio mchana, Hao walio tayari kumwamsha huyo Lewiathani. 9 Nyota za mapambazuko yake na ziwe giza; Na utafute mwanga lakini usiupate; Wala usiyaone mapambazuko; 10 Kwa sababu haukuifunga milango ya tumbo la mamangu. Wala kunifichia taabu machoni. 11 Mbona mimi sikufa wakati nikizaliwa? Mbona nisitoe roho hapo nilipotoka tumboni? 12 Mbona pawe na magoti ya kunipokea? Au hayo maziwa, hata nikanyonya? 13 Maana hapo ningelala na kutulia; Ningelala usingizi; na kupata kupumzika; 14 Pamoja na wafalme na washauri wa dunia, Hao waliojijengea maganjoni; 15 Au pamoja na wakuu wenye dhahabu, Waliozijaza nyumba zao fedha; 16 Au, mbona kuzikwa kama mimba iliyoharibika, nisingekuwako; Kama wachanga wasiouona mwanga kabisa. 17 Huko waovu huacha kusumbua; Huko nako hao waliochoka wanapumzika. 18 Huko wafungwa wanastarehe pamoja; Hawaisikii sauti yake msimamizi. 19 Wakuu na wadogo wako huko; Mtumishi yuko huru kwa bwana wake. 20 Mbona yeye aliye mashakani kupewa mwanga, Na hao wenye uchungu rohoni kupewa uhai; 21 Ambao wangojea mauti, lakini hawayapati; Na kuyachimbulia kuliko watafutavyo hazina iliyostirika; 22 Ambao wafurahi mno, Na kushangilia watakapoliona kaburi? 23 Kwa nini mtu aliyezibiwa njia kupewa mwanga, Ambaye Mungu amemzingira kwa ukigo? 24 Kwani kuugua kwangu kwaja kana kwamba ni chakula, Na kunguruma kwangu kumemiminika kama maji. 25 Maana jambo hilo nichalo hunipata, Nalo linitialo hofu hunijia. 26 Mimi sioni raha, wala situlii, wala kupumzika; Lakini taabu huja. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya