Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Mwanzo 43 - Swahili Revised Union Version


Ndugu zake Yusufu warudi, wakimleta Benyamini

1 Njaa ikawa kali katika nchi.

2 Ikawa walipokwisha kula nafaka waliyoileta kutoka Misri, baba yao akawaambia, Rudini huko, mkatununulie chakula kidogo.

3 Yuda akamwambia akisema, Yule mtu alituagizia sana akisema, Hamtaniona uso wangu, ndugu yenu asipokuwa pamoja nanyi.

4 Ukimtuma ndugu yetu pamoja nasi, tutashuka na kukununulia chakula.

5 Ila usipomtuma, hatushuki, maana mtu yule alituambia, Hamtaniona uso wangu, ndugu yenu asipokuwa pamoja nanyi.

6 Israeli akasema, Mbona mmenitendea vibaya hata mkamwarifu mtu yule ya kwamba mna ndugu mwingine?

7 Wakasema, Mtu yule alituhoji sana habari zetu na za jamaa yetu, akisema, Baba yenu angali hai? Mnaye ndugu mwingine? Nasi tukamjibu sawasawa na maswali hayo. Je! Tungaliwezaje kujua ya kwamba atasema, Shukeni pamoja na ndugu yenu?

8 Yuda akamwambia Israeli baba yake, Mtume kijana pamoja nami, tuondoke, tuende zetu, ili tupate kuishi, wala tusife, sisi na wewe na watoto wetu.

9 Mimi nitakuwa mdhamini wake, umtake mkononi mwangu. Nisipomleta tena kwako, na kumweka mbele yako, nitakuwa mwenye hatia mbele yako daima;

10 maana kama hatungalikawia, hakika tungaliisha kurudi mara ya pili.

11 Israeli, baba yao, akawaambia, Kama ndivyo, fanyeni hivi; twaeni tunu za nchi katika vyombo vyenu, mkamchukulie mtu huyo zawadi, zeri kidogo, na asali kidogo, ubani, na manemane, na jozi, na lozi.

12 Mkatwae fedha maradufu mikononi mwenu, na fedha zile zilizorudishwa kinywani mwa magunia yenu zirudisheni mikononi mwenu; labda zilisahauliwa.

13 Mtwaeni na ndugu yenu, mwondoke na kurudi kwa mtu yule.

14 Mungu Mwenyezi na awape rehema usoni pa mtu yule ili awafungulie ndugu yenu huyo mwingine, na Benyamini. Nami nikifiwa na watoto wangu, nimefiwa.

15 Basi hao watu wakatwaa zawadi ile, wakatwaa na fedha maradufu mikononi mwao, na Benyamini; wakaondoka, wakashuka mpaka Misri, wakasimama mbele ya Yusufu.

16 Naye Yusufu alipomwona Benyamini pamoja nao, akamwambia msimamizi wa nyumba yake, Uwalete watu hawa nyumbani, ukachinje mnyama na kuwaandalia, maana watu hawa watakula pamoja nami adhuhuri.

17 Yule mtu akafanya kama Yusufu alivyomwambia Naye akawaleta watu hao nyumbani mwa Yusufu.

18 Lakini watu hao wakaogopa kwa sababu wameletwa nyumbani mwa Yusufu, wakasema, Kwa sababu ya fedha zile zilizorudishwa katika magunia yetu mara ya kwanza tumeletwa humu; apate kutushitaki, na kutushika, atutwae sisi kuwa watumwa, na punda wetu.

19 Wakamkaribia yule msimamizi wa nyumba ya Yusufu, wakasema naye mlangoni pa nyumba.

20 Wakamwambia, Tazama, bwana, kweli tulishuka mara ya kwanza ili tununue chakula.

21 Ikawa, tulipofika nyumba ya wageni, tukafungua magunia yetu, kumbe! Fedha za kila mtu zilikuwako kinywani mwa gunia lake, fedha zetu kwa uzani wake kamili; nasi tumezileta tena mikononi mwetu.

22 Nasi tumeleta fedha nyingine mikononi mwetu ili tununue chakula; hatujui ni nani aliyezitia fedha zetu katika magunia yetu.

23 Akawaambia, Amani iwe kwenu, msiogope; Mungu wenu, naye ni Mungu wa baba yenu, amewapa akiba katika magunia yenu; fedha zenu zilinifikia. Kisha akawatolea Simeoni kwao.

24 Mtu yule akawaleta wale watu nyumbani mwa Yusufu, akawapa maji, wakanawa miguu, akawapa punda wao chakula.

25 Wakaiweka tayari ile zawadi hadi atakapokuja Yusufu adhuhuri, maana wamesikia ya kwamba watakula chakula huko.

26 Alipokuja Yusufu nyumbani, wakamletea ile zawadi iliyokuwa mikononi mwao nyumbani mwake, wakamwinamia mpaka chini.

27 Akawaulizia hali yao, akasema, Je! Baba yenu, yule mzee mliyemnena, hajambo? Angali hai?

28 Wakasema, Mtumishi wako baba yetu hajambo, angali hai; wakainama, wakasujudu.

29 Akainua macho yake, akamwona Benyamini, nduguye, mwana wa mama yake, akasema, Huyu ndiye ndugu yenu mdogo, mliyeniambia habari zake? Akasema, Mungu akufadhili, mwanangu.

30 Yusufu akafanya haraka, kwa sababu moyo wake ulimwonea shauku nduguye, akatafuta pa kulilia, akaingia chumbani mwake, akalilia humo.

31 Akanawa uso, akatoka, akajizuia, akasema, Leteni chakula.

32 Wakamwandalia yeye peke yake, na wao peke yao, na wale Wamisri waliokula pamoja naye peke yao; maana Wamisri hawawezi kula pamoja na Waebrania, kwa kuwa ni chukizo kwa Wamisri.

33 Wakaketi mbele yake, mzaliwa wa kwanza kwa haki ya uzawa wake, na mdogo kwa udogo wake; watu hao wakastaajabu wao kwa wao.

34 Wakapelekewa sehemu za chakula kutoka mezani pake, lakini akazidisha sehemu ya Benyamini iwe kubwa mara tano kuliko zao. Wakanywa, wakafurahi pamoja naye.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo