Mwanzo 34 - Swahili Revised Union VersionDina abakwa 1 Basi Dina, binti Lea, ambaye Lea alimzalia Yakobo, akatoka kuwaona binti za nchi. 2 Shekemu, mwana wa Hamori, Mhivi, mkuu wa nchi, akamwona akamtwaa, akalala naye, akambikiri. 3 Moyo wake ukaambatana na Dina binti Yakobo, akampenda huyu msichana, akasema na huyu msichana kwa maneno mazuri. 4 Shekemu akamwambia Hamori, babaye, akasema, Unipatie msichana huyu awe mke wangu. 5 Basi Yakobo akasikia ya kwamba amembikiri Dina, binti yake. Na wanawe walikuwako pamoja na wanyama wake nyikani. Yakobo akanyamaza, hadi walipokuja. 6 Akatoka Hamori, babaye Shekemu, kumwendea Yakobo, aseme naye. 7 Wanawe Yakobo waliposikia hayo, wakaja kutoka malishoni; nao wakasikitika sana, wakakasirika mno, kwa sababu amefanya upumbavu katika Israeli kwa kulala na binti Yakobo, jambo lisilostahili kutendeka. 8 Hamori akasema nao, akinena, roho ya Shekemu, mwanangu, inamtamani binti yenu, tafadhalini, mpeni amwoe. 9 Mkaoane na sisi, mtupe sisi binti zenu, nanyi mkatwae binti zetu. 10 Nanyi mtakaa nasi, na nchi hii itakuwa mbele yenu; kaeni, na kufanya biashara humo, mkapate mali humo. 11 Shekemu akamwambia babaye yule msichana na nduguze, Na nikubalike machoni penu, na mtakavyoniambia nitatoa. 12 Mjapoongeza sana mahari na zawadi, nitatoa kadiri ya mtakavyoniambia, lakini mnipe huyu msichana, awe mke wangu. 13 Wana wa Yakobo wakawajibu Shekemu na Hamori babaye, kwa hila, maana amemharibu Dina, dada yao, 14 wakawaambia, Hatuwezi kufanya neno hili, tumpe dada yetu mtu asiyetahiriwa; ingekuwa aibu kwetu. 15 Lakini kwa sharti hii tu tutapatana nanyi; mkiwa kama sisi, akitahiriwa kila mwanamume wenu, 16 ndipo tutawapa ninyi binti yetu, na sisi tutatwaa binti zenu tutakaa pamoja nanyi, nasi tutakuwa watu wamoja. 17 Lakini kama hamtusikii na kutahiriwa, basi tutamtwaa binti yetu, nasi tutakwenda zetu. 18 Maneno yao yakawa mema machoni pa Hamori, na machoni pa Shekemu, mwana wa Hamori. 19 Na yule kijana hakukawia kulifanya neno lile, maana amependezewa na binti Yakobo, naye alikuwa mwenye heshima kuliko wote nyumbani mwa babaye. 20 Hamori, na Shekemu mwanawe, wakaja langoni pa mji wao, wakasema na watu wa mji wao, wakinena, 21 Watu hawa wana amani nasi, basi na wakae katika nchi, na kufanya biashara humo; kwa maana nchi ni kubwa, yawatosha; na tuwatwae binti zao kuwa wake zetu, na binti zetu tuwape wao. 22 Lakini kwa sharti hiyo moja tu watapatana nasi wakae wote kwetu, tuwe watu wamoja, kama tukitahiriwa kila mwanamume, kama wao walivyotahiriwa. 23 Je! Kondoo zao, na mali zao, na wanyama wao wote hawatakuwa mali zetu? Basi na tupatane nao tu, nao watakaa kwetu. 24 Wakawasikia Hamori na Shekemu mwanawe, wote watokeao katika lango la mji wake. Wakatahiriwa kila mwanamume, wote watokao katika lango la mji wake. Ndugu zake Dina walipiza Kisasi 25 Ikawa siku ya tatu, walipokuwa wakiumwa sana, wana wawili wa Yakobo, Simeoni na Lawi, nduguze Dina, wakatwaa kila mtu upanga wake, wakaujia mji kwa ujasiri, wakawaua wanaume wote. 26 Wakawaua Hamori, na Shekemu mwanawe, kwa upanga, wakamtwaa Dina katika nyumba ya Shekemu, wakatoka. 27 Wana wa Yakobo wakawajia hao waliouawa, wakaupora mji kwa sababu wamemharibu dada yao. 28 Wakachukua kondoo wao, na ng'ombe wao, na punda wao, na vitu vilivyokuwamo mjini, na vile vilivyokuwako kondeni. 29 Wakatwaa na mali yao zote, watoto wao wote, na wake zao wakateka na hata wakapora vyote vilivyokuwemo nyumbani. 30 Yakobo akawaambia Simeoni na Lawi, Mmenitaabisha, kunifanya ninuke vibaya kati ya watu wa nchi hii, Wakanaani na Waperizi; na mimi, kwa kuwa watu wangu ni haba, watanikusanyikia, na kunipiga, nami nitaangamizwa, mimi na nyumba yangu. 31 Nao wakasema, Je! Ni vema amtendee dada yetu kama kahaba? |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya