Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Mathayo 17 - Swahili Revised Union Version


Kugeuka sura

1 Na baada ya siku sita Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani;

2 akageuka sura yake mbele yao; uso wake ukang'aa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama nuru.

3 Na tazama, wakatokewa na Musa na Eliya, wakizungumza naye.

4 Petro akajibu akamwambia Yesu, Bwana, ni vizuri sisi kuwapo hapa; ukitaka, nitafanya hapa vibanda vitatu, kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya.

5 Alipokuwa bado akisema, tazama, wingu jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka katika lile wingu, ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye.

6 Na wale wanafunzi waliposikia, walianguka kifudifudi na kuogopa sana.

7 Yesu akaja, akawagusa, akasema, Inukeni, wala msiogope.

8 Wakainua macho yao, wasione mtu ila Yesu peke yake.

9 Na walipokuwa wakishuka mlimani, Yesu aliwaagiza, akasema, Msimwambie mtu yeyote habari ya maono hayo, hadi Mwana wa Adamu atakapofufuka katika wafu.

10 Wanafunzi wake wakamwuliza, wakisema, Basi kwa nini waandishi hunena ya kwamba imempasa Eliya kuja kwanza?

11 Naye akajibu, akawaambia, Kweli Eliya yuaja kwanza, naye atatengeneza yote,

12 ila nawaambia, ya kwamba Eliya amekwisha kuja, wasimtambue, lakini wakamtenda yote waliyotaka. Vivyo hivyo Mwana wa Adamu naye yuaenda kuteswa kwao.

13 Ndipo wale wanafunzi walipofahamu ya kuwa amesema nao habari za Yohana Mbatizaji.


Yesu aponya mvulana mwenye pepo

14 Nao walipoufikia mkutano, mtu mmoja akamjia, akampigia magoti, akisema,

15 Bwana, umrehemu mwanangu, kwa kuwa ana kifafa, na kuteswa vibaya; maana mara nyingi huanguka motoni, na mara nyingi majini.

16 Nilimleta kwa wanafunzi wako, wasiweze kumponya.

17 Yesu akajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, kilichopotoka, nitakaa pamoja nanyi hadi lini? Nitachukuliana nanyi hadi lini? Mleteni huku kwangu.

18 Yesu akamkemea pepo, naye akamtoka; yule mvulana akapona tangu saa ile.

19 Kisha wale wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha wakasema Mbona sisi hatukuweza kumtoa?

20 Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu. [

21 Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.]


Yesu asema tena juu ya kufa na kufufuka kwake

22 Nao walipokuwa wakikaa Galilaya, Yesu akawaambia, Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua, na siku ya tatu atafufuka.

23 Wakasikitika sana.


Yesu na ushuru wa hekalu

24 Na walipofika Kapernaumu, wale watozao nusu-shekeli walimwendea Petro, wakasema, Je! Mwalimu wenu hatoi ushuru wa hekalu? Akasema, Hutoa.

25 Naye alipoingia nyumbani, Yesu alitangulia kumwuliza, akisema, Waonaje, Simoni? Wafalme wa dunia hutwaa kodi ama ushuru kwa watu gani? Kwa wana wao au kwa wageni?

26 Naye aliposema, Kwa wageni, Yesu alimwambia, Basi, kama ni hivyo, wana wako huru.

27 Lakini tusije tukawakwaza, nenda baharini ukatupe ndoana, ukatwae samaki yule azukaye kwanza; na ukifumbua mdomo wake utaona shekeli; ichukue hiyo ukawape kwa ajili yangu na kwa ajili yako.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo