Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

2 Samueli 23 - Swahili Revised Union Version


Maneno ya mwisho ya Daudi

1 Basi haya ndiyo maneno ya mwisho ya Daudi. Daudi, mwana wa Yese, anena, Anena huyo mtu aliyeinuliwa juu, Yeye, masihi wake Mungu wa Yakobo, Mtungaji wa nyimbo za Israeli mwenye kupendeza;

2 Roho ya BWANA ilinena ndani yangu, Na neno lake likawa ulimini mwangu.

3 Mungu wa Israeli alisema, Mwamba wa Israeli aliniambia, Atawalaye wanadamu kwa haki, Akitawala katika kicho cha Mungu,

4 Atakuwa kama nuru ya asubuhi jua lichapo, Asubuhi isiyo na mawingu. Likichipuza mimea ardhini, Kwa mwangaza baada ya mvua;

5 Je! Sivyo ilivyo nyumba yangu mbele za BWANA? Kwa kuwa amefanya nami agano la milele; Ina taratibu katika yote, ni thabiti, Maana ni wokovu wangu wote, na shauku langu lote.

6 Lakini hatawachipuza watu wasiofaa; Watakuwa wote kama miiba ya nyikani ya kutupwa, Maana haichukuliki kwa mkono,

7 Mtu atakayeigusa hiyo, Na awe na chuma na mpini wa mkuki, Nao watateketezwa papo hapo kwa moto.


Mashujaa wa Daudi

8 Haya ndiyo majina ya mashujaa aliokuwa nao Daudi; Yashobeamu Mhakmoni, Hamkuu wa wakuu wa majeshi; huyo aliliinua shoka lake juu ya watu mia nane waliouawa pamoja.

9 Na baada yake kulikuwa na Eleazari, mwana wa Dodai, Mwahohi, mmojawapo wa wale mashujaa watatu waliokuwa pamoja na Daudi; walipowatukana Wafilisti waliokuwa wamekusanyika huko ili kupigana, na watu wa Israeli walikuwa wamekwenda zao;

10 huyo aliinuka, akawapiga Wafilisti hata mkono wake ukachoka, na mkono wake ukaambatana na upanga; naye BWANA akafanya wokovu mkuu siku ile; nao watu wakarudi nyuma yake ili kuteka nyara tu.

11 Na baada yake kulikuwa na Shama, mwana wa Agee, Mharari; nao Wafilisti walikuwa wamekusanyika huko Lehi, palipokuwapo shamba lililojaa midengu; nao watu wakawakimbia Wafilisti;

12 ila huyo alisimama katikati ya konde lile, akalipigania, akawaua Wafilisti; naye BWANA akafanya wokovu mkuu.

13 Tena, watatu miongoni mwa wale thelathini waliokuwa wakuu wakashuka, wakamwendea Daudi wakati wa mavuno mpaka pango la Adulamu, na kikosi cha Wafilisti walikuwa wamefanya kambi katika bonde la Warefai.

14 Naye Daudi wakati ule alikuwako ngomeni, na jeshi la Wafilisti wakati ule walikuwako Bethlehemu.

15 Daudi akatamani, akasema, Laiti mtu angeninywesha maji ya kisima cha Bethlehemu, kilicho karibu na lango!

16 Basi hao mashujaa watatu wakapenya jeshi la Wafilisti, wakateka maji kutoka kile kisima cha Bethlehemu, kilichokuwa karibu na lango, wakayachukua, wakamletea Daudi; lakini yeye hakukubali kuyanywa, akayamimina mbele za BWANA.

17 Akasema, Hasha, BWANA, nisifanye hivi; je! Si damu hii ya watu hao waliohatarisha nafsi zao? Kwa hiyo hakukubali kuyanywa. Hayo ndiyo waliyoyafanya wale mashujaa watatu.

18 Tena, Abishai, nduguye Yoabu, mwana wa Seruya, alikuwa mkuu wa wale watatu. Huyo aliuinua mkuki wake juu ya watu mia tatu, akawaua, akawa na jina kati ya wale watatu.

19 Je! Huyo hakuwa na heshima maalumu miongoni mwa wale watatu? Kwa hiyo akawekwa kuwa kamanda wao; ila hakuweza kuwa kama wale watatu.

20 Tena Benaya, mwana wa Yehoyada, mtu hodari wa Kabseeli aliyekuwa amefanya mambo makuu; aliwaua simba wawili wakali wa Moabu, pia aliingia katika shimo na kumwua simba wakati wa theluji;

21 huyo naye akamwua Mmisri, mtu mrefu; naye huyo Mmisri alikuwa na mkuki mkononi; lakini yeye alimshukia na gongo, akamnyang'anya Mmisri mkuki mkononi mwake, akamwua kwa mkuki wake mwenyewe.

22 Hayo ndiyo aliyoyafanya Benaya, mwana wa Yehoyada, akawa na jina kati ya wale mashujaa watatu.

23 Alikuwa mwenye heshima kuliko wale thelathini, ila hakudiriki kuwamo katika wale watatu. Naye Daudi akamteua kuwa mkuu wa walinzi wake.

24 Asaheli, nduguye Yoabu, alikuwa mmojawapo wa wale thelathini; na Elhanani, mwana wa Dodo, wa Bethlehemu;

25 na Shama, Mharodi, na Elika, Mharodi;

26 na Helesi, Mpeloni, na Ira, mwana wa Ikeshi, Mtekoi;

27 na Abiezeri, Mwanathothi, na Sibekai, Mhushathi;

28 na Salmoni, Mwahohi, na Maharai, Mnetofathi;

29 na Heledi, mwana wa Baana, Mnetofathi, na Itai, mwana wa Ribai, wa Gibea wa wana wa Benyamini;

30 na Benaya, Mpirathoni, na Hurai, wa vijito vya Gaashi;

31 na Abieli, Mwarbathi, na Azmawethi, Mbarhumi;

32 na Eliaba, Mshaalboni, na wana wa Yasheni; na Yonathani,

33 mwana wa Shama, Mharari, na Ahiamu, mwana wa Shalali, Mharari;

34 na Elifeleti, mwana wa Ahasbai, na Heferi, Mmaakathi, na Eliamu, mwana wa Ahithofeli, Mgiloni;

35 na Hezro, Mkarmeli, na Paarai, Mwarbi;

36 na Igali, mwana wa Nathani, wa Soba, na Bani, Mgadi;

37 na Seleki, Mwamoni, na Naharai, Mbeerothi, ambao ni wachukua silaha wa Yoabu, mwana wa Seruya;

38 na Ira, Mwithri, na Garebu, Mwithri;

39 na Uria, Mhiti; idadi yao ilikuwa watu thelathini na saba.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo