1 Samueli 8 - Swahili Revised Union VersionWaisraeli waomba kuwa na mfalme 1 Na Samweli alipozeeka, aliwafanya wanawe wawe waamuzi juu ya Israeli. 2 Na jina la mwanawe mzaliwa wa kwanza lilikuwa Yoeli; na jina la wa pili Abiya; walikuwa waamuzi katika Beer-sheba. 3 Ila wanawe hawakuenda katika njia zake, bali waliziacha, ili wapate faida; wakapokea rushwa, na kupotosha hukumu. 4 Ndipo wazee wote wa Israeli wakakutana pamoja, wakamwendea Samweli huko Rama; 5 wakamwambia, Angalia, wewe umezeeka, na wanao hawaendi katika njia zako; basi, tuteulie mfalme atutawale kama mataifa yale mengine yote. 6 Lakini neno hilo likawa baya machoni pa Samweli, waliposema, Tupe mfalme atuamue. Naye Samweli akamwomba BWANA. 7 BWANA akamwambia Samweli, Isikilize sauti ya watu hawa katika kila neno watakalokuambia; kwa maana hawakukukataa wewe, bali wamenikataa mimi, ili nisiwe mfalme juu yao. 8 Kwa kadiri ya matendo yote waliyonitenda tokea siku ile nilipowatoa katika Misri hata leo, kwa kuniacha mimi, na kwa kutumikia miungu mingine, ndivyo wanavyokutenda wewe. 9 Basi sasa, isikilize sauti yao; lakini, uwaonye sana, na kuwaonesha desturi ya mfalme atakayewamiliki. 10 Naye Samweli akawaambia wale watu waliotaka mfalme maneno yote ya BWANA. 11 Akasema, Mfalme atakayewatawala ninyi atakuwa na desturi hii; atatwaa wana wenu na kuwaweka kwake, katika magari yake, na kuwa wapanda farasi wake; nao watapiga mbio mbele ya magari yake. 12 Naye atawaweka kwake kuwa wakuu juu ya maelfu, na makamanda juu ya hamsini hamsini; na wengine atawaweka walime shamba lake, na kuvuna mavuno yake, na kufanyiza zana zake za vita, na vyombo vya magari yake. 13 Na binti zenu atawatwaa kuwa watengenezaji wa marhamu, wapishi na waokaji. 14 Atatwaa mashamba yenu, na mashamba yenu ya mizabibu, na ya mizeituni, yale yaliyo mazuri sana, ili awape watumishi wake. 15 Naye atawatoza ushuru wa mbegu zenu na wa mizabibu yenu, awape wakuu wake, na watumishi wake. 16 Atawatwaa watumishi wenu na wajakazi wenu, na ng'ombe wenu walio wazuri sana, na punda wenu, naye atawatia katika kazi zake mwenyewe. 17 Atawatoza fungu la kumi la mifugo wenu; nanyi mtakuwa watumwa wake. 18 Nanyi mtalia siku ile kwa sababu ya mfalme wenu mliyejichagulia; BWANA asiwajibu siku ile. Waisraeli wapewa mfalme 19 Lakini hao watu wakakataa kuisikiliza sauti ya Samweli; wakasema, Sivyo hivyo; lakini tunataka kuwa na mfalme juu yetu; 20 ili sisi nasi tufanane na mataifa yote; tena ili mfalme wetu atuamue, tena atuongoze na kupigana vita vyetu 21 Samweli akayasikia maneno yote ya watu, akayanena masikioni mwa BWANA. 22 BWANA akamwambia Samweli, Isikilize sauti yao, ukawateulie mfalme. Kisha Samweli akawaambia watu wa Israeli, Kila mtu aende nyumbani kwake. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya