Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

1 Samueli 14 - Swahili Revised Union Version

1 Basi ikatukia siku moja, ya kwamba Yonathani, mwana wa Sauli, akamwambia yule kijana aliyembebea silaha zake, Haya! Na tuvuke twende kwa Wafilisti ngomeni, pale ng'ambo ya pili. Lakini hakumwarifu babaye.

2 Naye Sauli alikuwa akikaa katika Viunga vya Gibea, chini ya mkomamanga uliokuwa kwenye uwanja huko Migroni; na hao watu waliokuwa pamoja naye walikuwa watu mia sita;

3 pamoja na Ahiya, mwana wa Ahitubu nduguye Ikabodi, mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani wa BWANA huko Shilo, aliyevaa naivera. Tena hao watu hawakujua ya kwamba Yonathani ameondoka.

4 Na katikati ya mapito, ambayo Yonathani alitaka kuipitia ili kuifikia hiyo ngome ya Wafilisti, palikuwa na kilima cha mwamba upande huu, na kilima cha mwamba upande huu; kimoja kiliitwa Bosesi, na cha pili Sene.

5 Hicho kilima kimoja kimesimama upande wa kaskazini, mbele ya Mikmashi, na hicho cha pili upande wa kusini, mbele ya Geba.

6 Basi, Yonathani akamwambia yule kijana aliyembebea silaha zake, Haya! Na twende tukavuke ngomeni mwa hao wasiotahiriwa; yamkini BWANA atatutendea kazi; kwa maana hakuna la kumzuia BWANA asiokoe, kama ni kwa wengi au kama ni kwa wachache.

7 Naye huyo mbebaji silaha akamjibu, Fanya yote yaliyomo moyoni mwako; angalia, mimi hapa ni pamoja nawe, moyo wangu ni kama moyo wako.

8 Ndipo Yonathani akasema, Tazama, sisi tutavuka kwa watu hawa, na kujidhihirisha kwao.

9 Nao wakituambia hivi, Ngojeni, hadi sisi tuwafikie; ndipo tusimame pale pale mahali petu, tusiwaendee.

10 Lakini wakisema hivi, Haya! Ninyi, njoni; hapo ndipo tutakapoenda; kwa maana BWANA amewatia mikononi mwetu; na hii itakuwa ndiyo ishara kwetu.

11 Basi, hao wote wawili wakajidhihirisha mbele ya ngome ya Wafilisti, na wale Wafilisti wakasema, Kumbe! Wale Waebrania wanatoka katika mashimo walimojificha!

12 Nao watu wa ngomeni wakamjibu Yonathani na mbebaji silaha zake, wakasema, Haya! Ninyi, pandeni juu hapa tulipo, na sisi tutawaonesha jambo. Yonathani akamwambia yule aliyezichukua silaha, Haya! Panda nyuma yangu; kwa kuwa BWANA amewatia mikononi mwa Israeli.

13 Basi Yonathani akapanda kwa mikono na miguu yake, na mbebaji silaha nyuma yake; na hao watu wakaanguka mbele ya Yonathani; na huyo mbemba silaha zake akawaua akiwa nyuma yake.

14 Na uuaji huo wa kwanza walioufanya Yonathani na mchukua silaha zake, ulikuwa kama watu ishirini, katika eneo la kama nusu ya kiwanja kiwezacho kulimwa katika siku nzima.

15 Kukawa na tetemeko katika kambi, na katika mashamba, na katikati ya watu wote; watu wa ngomeni, na watekaji nyara, wakatetemeka nao; hata na nchi ikatetemeka pia; basi kulikuwa na tetemeko kubwa mno.

16 Nao wale walinzi wa Sauli huko Gibea ya Benyamini wakaangalia, na tazama, mkutano ule ulikuwa ukitoweka, na watu walikuwa wakienda huku na huko.

17 Ndipo Sauli akawaambia watu waliokuwa pamoja naye, Haya! Hesabuni sasa, mkaone ni nani aliyeondoka kwetu. Nao walipokwisha hesabu, tazama Yonathani na yule aliyembebea silaha zake hawakuwapo.

18 Basi Sauli akamwambia Ahiya, Lilete hapa sanduku la Mungu. Kwa kuwa hilo sanduku la Mungu, wakati huo lilikuwapo pamoja na wana wa Israeli.

19 Ikawa Sauli alipokuwa akisema na kuhani, hayo makelele katika kambi ya Wafilisti yakaongezeka zaidi na zaidi; basi Sauli akamwambia kuhani, Rudi, usiendee sanduku la Mungu.

20 Naye Sauli na watu wote waliokuwapo pamoja naye wakakusanyika, wakaenda vitani; na tazama, huko upanga wa kila mtu ulikuwa juu ya mwenziwe, kukawa fujo tele kabisa.

21 Basi na wale Waebrania waliokuwa pamoja na Wafilisti tangu zamani, wale waliopanda pamoja nao mpaka kambini toka nchi iliyozunguka; watu hao nao wakageuka kuwa upande wa Waisraeli waliokuwa pamoja na Sauli na Yonathani.

22 Na vile vile watu wote wa Israeli waliokuwa wamejificha katika nchi ya milima milima ya Efraimu, waliposikia ya kwamba Wafilisti wamekimbia, hata hao nao wakawafuatia mbio vitani.

23 Hivyo BWANA akawaokoa Israeli siku ile; na vita ilienea mpaka kupita Beth-aveni, na watu wote waliokuwa pamoja na Sauli walikuwa kama wanaume elfu kumi. Vita ikanenea katika nchi yenye milima milima ya Efraimu.


Sauli awaapisha watu

24 Nao watu wa Israeli walisumbuka sana siku ile; lakini Sauli alikuwa amewaapisha watu, akisema, Na alaaniwe mtu awaye yote alaye chakula chochote hadi jioni, nipate kujilipiza kisasi juu ya adui zangu. Basi hakuna mtu miongoni mwao aliyeonja chakula.

25 Nao watu wote wakaingia mwituni; na humo mlikuwa na asali juu ya nchi.

26 Na hapo watu walipoingia mwituni, tazama, hiyo asali ilikuwa ikidondoka; lakini hakuna mtu hata mmoja aliyetia mkono wake kinywani; kwa sababu hao watu walikuwa wakikiogopa kile kiapo.

27 Ila Yonathani hakusikia, hapo babaye alipowaagiza watu kwa kiapo; basi yeye akainyosha ncha ya fimbo iliyokuwa mkononi mwake, na kuichovya katika sega la asali, kisha akatia mkono wake kinywani; na macho yake yakatiwa nuru.

28 Ndipo mmojawapo wa watu akamjibu, akasema, Baba yako aliwaagiza watu sana kwa kiapo, akisema, Na alaaniwe mtu alaye chakula leo. Na hao watu walikuwa wamepungukiwa na nguvu.

29 Ndipo Yonathani akasema, Babangu ameifadhaisha nchi; tafadhali, angalia jinsi macho yangu yalivyotiwa nuru, kwa sababu nilionja asali hii kidogo.

30 Je! Si ingekuwa bora zaidi kama watu wangalikula na kushiba leo katika nyara hizi za adui zao walizoziteka? Kwa maana haukuwa uuaji mkuu sasa katikati ya Wafilisti.

31 Nao wakawapiga watu miongoni mwa Wafilisti siku ile kutoka Mikmashi mpaka Ayaloni; na hao watu walikuwa wamepungukiwa sana na nguvu.

32 Basi watu wakazirukia zile nyara, wakatwaa kondoo, na ng'ombe, na ndama, na kuwachinja papo hapo juu ya nchi, nao wale watu walikuwa wakiwala pamoja na damu.

33 Ndipo wakamwambia Sauli, wakisema, Angalia, watu hao wanakosa juu ya BWANA, kwa jinsi wanavyokula pamoja na damu. Naye akasema, Ninyi mmefanya kwa hiana; vingirisheni kwangu leo jiwe kubwa.

34 Kisha Sauli akasema, Haya! Tawanyikeni katikati ya watu mkawaambie, Nileteeni hapa kila mtu ng'ombe wake, na kila mtu kondoo wake, mkawachinje hapa na kula; wala msikose juu ya BWANA, kwa kula pamoja na damu. Nao watu wote wakaleta kila mtu ng'ombe wake pamoja naye usiku ule, nao wakawachinja hapo.

35 Naye Sauli akamjengea BWANA madhabahu; hiyo ndiyo madhabahu ya kwanza aliyomjengea BWANA.


Yonathani hatarini

36 Kisha Sauli akasema, Haya! Na tushuke kuwafuata Wafilisti wakati wa usiku, na kuwateka nyara hata mapambazuko, wala tusiwaache hata mmoja wao. Nao wakamjibu, Fanya lolote uonalo kuwa ni jema. Ndipo yule kuhani akasema, Na tumkaribie Mungu hapa.

37 Basi Sauli akataka shauri kwa Mungu, Je! Nishuke ili kuwafuatia Wafilisti? Je! Utawatia mikononi mwa Israeli? Lakini hakumjibu neno lolote siku ile.

38 Ndipo Sauli akasema, Karibieni hapa, enyi wakuu wote wa watu; mjue na kuona dhambi hii ya leo imekuwa katika kosa gani.

39 Kwa maana, kama aishivyo BWANA, awaokoaye Waisraeli, hata ikiwa iko kwa Yonathani, mwanangu, hakika atakufa. Lakini miongoni mwa watu wote hakuna mtu yeyote aliyemjibu.

40 Ndipo akawaambia Waisraeli wote, Ninyi mtakuwa upande mmoja, na mimi na mwanangu Yonathani tutakuwa upande wa pili. Basi wakamwambia Sauli, Fanya uonayo kuwa ni mema.

41 Kwa hiyo Sauli akamwambia BWANA, Mungu wa Israeli, [Kwa nini usimjibu mtumishi wako leo? Ikiwa dhambi iko ndani yangu, au ndani yake Yonathani mwanangu, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, utoe Urimu; bali ukisema hivi, Dhambi iko katika watu wako Israeli,] utoe Thumimu. Basi Yonathani na Sauli wakatwaliwa, lakini watu wakapona.

42 Basi Sauli akasema, Sasa piga kati ya mimi na mwanangu Yonathani, [yeyote ambaye BWANA atamtwaa, atakufa. Nao watu wakamwambia Sauli, La! Sivyo hivyo; lakini Sauli akawaweza watu. Nao wakapiga kati ya yeye na mwanawe Yonathani,] naye Yonathani akatwaliwa.

43 Ndipo Sauli akamwambia Yonathani, Niambie ulilolifanya. Basi Yonathani akamwambia, akasema, Ni kweli, mimi nilionja asali kidogo kwa ncha ya fimbo ile iliyokuwa mkononi mwangu; na tazama, imenipasa kufa.

44 Naye Sauli akasema, Mungu anifanyie hivi, na kuzidi; kwa kuwa hakika utakufa, Yonathani.

45 Lakini watu wakamwambia Sauli, Je! Atakufa Yonathani, ambaye ndiye aliyeufanya huo wokovu mkuu katika Israeli? Hasha! Kama aishivyo BWANA, hautaanguka chini hata unywele mmoja wa kichwa chake; kwa maana ametenda kazi pamoja na Mungu leo. Hivyo hao watu wakamponya Yonathani, asife.

46 Ndipo Sauli akakwea kuacha kuwafuata Wafilisti; nao Wafilisti wakaenda zao kwao.


Sauli apigana vita zaidi

47 Basi Sauli alipokwisha kuutwaa ufalme juu ya Israeli, alipigana na adui zake wote pande zote, juu ya Moabu, na juu ya wana wa Amoni, na juu ya Edomu, na juu ya wafalme wa Soba, na juu ya Wafilisti; na popote alipogeukia, akawashinda.

48 Naye kwa ushujaa, akawapiga Waamaleki, na kuwaokoa Waisraeli kutoka kwa mikono ya waliowateka nyara.

49 Basi, wana wa Sauli walikuwa ni hawa, Yonathani, na Ishvi, na Malkishua; na majina ya binti zake wawili yalikuwa haya; jina lake wa kwanza aliitwa Merabu, na jina lake mdogo aliitwa Mikali;

50 na jina lake mkewe Sauli aliitwa Ahinoamu, binti Ahimaasi. Tena, jina la jemadari wa jeshi lake aliitwa Abneri, mwana wa Neri, aliyekuwa baba mdogo wa Sauli.

51 Na Kishi, babaye Sauli, na Neri, babaye Abneri, walikuwa wana wa Abieli.

52 Tena, kulikuwa na vita kali sana juu ya Wafilisti siku zote za Sauli, naye Sauli alipomwona mtu yeyote aliyekuwa hodari, au mtu yeyote aliyekuwa shujaa, humtwaa ili awe pamoja naye.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo