Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Luka 5 - Swahili Revised Union Version


Yesu awaita wanafunzi wa kwanza

1 Ikawa makutano walipomsonga wakilisikiliza neno la Mungu, yeye alikuwa amesimama kando ya ziwa la Genesareti,

2 akaona mashua mbili zimekaa kando ya ziwa, lakini wavuvi wametoka, wanaosha nyavu zao.

3 Akaingia katika mashua moja, ndiyo yake Simoni, akamtaka aipeleke mbali kidogo na pwani. Akaketi, akawafundisha makutano akiwa katika mashua.

4 Na alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki.

5 Simoni akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu.

6 Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika;

7 wakawapungia mikono washiriki wenzao waliokuwa katika mashua nyingine, waje kuwasaidia; wakaja, wakazijaza mashua zote mbili, hata zikakaribia kuzama.

8 Simoni Petro alipoona hayo, alianguka magotini mbele ya Yesu, akisema, Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana.

9 Maana alishikwa na mshangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye, kwa sababu ya wingi wa samaki waliowapata;

10 na kadhalika Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, waliokuwa washirika wa Simoni. Yesu akamwambia Simoni, Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu.

11 Hata walipokwisha kuziegesha mashua zao pwani, wakaacha vyote wakamfuata.


Yesu Amtakasa mwenye Ukoma

12 Ikawa, alipokuwa katika mmojawapo wa miji ile, tazama, palikuwa na mtu amejaa ukoma; naye alipomwona Yesu alianguka kifudifudi, akamwomba akisema, Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa.

13 Naye akaunyosha mkono wake, akamgusa akisema, Nataka; takasika. Na mara ukoma wake ukamwondoka.

14 Akamkataza asimwambie mtu, ila, Nenda ukajioneshe kwa kuhani; ukatoe sadaka kwa ajili ya kutakasika kwako kama Musa alivyoamuru, iwe ushuhuda kwao.

15 Lakini habari zake zikazidi kuenea, wakakutanika makutano mengi wamsikilize na kuponywa magonjwa yao.

16 Lakini yeye alikuwa akijiepua, akaenda mahali pasipokuwa na watu, akaomba.


Yesu amponya mwenye kupooza

17 Ikawa siku zile mojawapo alikuwa akifundisha, na Mafarisayo na waalimu wa torati walikuwa wameketi hapo, waliotoka katika kila kijiji cha Galilaya, na Yudea, na Yerusalemu; na uweza wa Bwana ulikuwapo apate kuponya.

18 Na tazama, wakaja watu wanamchukua kitandani mtu mwenye kupooza; wakataka kumpeleka ndani na kumweka mbele yake.

19 Hata walipokosa nafasi ya kumpeleka ndani kwa ajili ya lile kundi la watu, walipanda juu ya dari wakampitisha katika matofali ya juu, wakamshusha yeye na kitanda chake katikati mbele ya Yesu.

20 Naye alipoiona imani yao, alimwambia, Ee rafiki, umesamehewa dhambi zako.

21 Basi, wale Waandishi na Mafarisayo wakaanza kuulizana wakisema, Ni nani huyu asemaye maneno ya kukufuru? Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?

22 Na Yesu alijua hoja zao, akajibu akawaambia, Mnajiuliza nini mioyoni mwenu?

23 Lililo jepesi ni lipi? Kusema, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, uende?

24 Lakini, mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (alimwambia yule mwenye kupooza). Nakuambia, Ondoka, ujitwike kitanda chako, ukaende zako nyumbani kwako.

25 Mara hiyo akasimama mbele yao, akajitwika kile alichokilalia, akaenda zake nyumbani kwake, huku akimtukuza Mungu.

26 Mshangao ukawashika wote, wakamtukuza Mungu; wakajaa hofu, wakisema, Leo tumeona mambo ya ajabu.


Yesu amwita Lawi

27 Baada ya hayo akatoka, akaona mtoza ushuru, jina lake Lawi, ameketi forodhani, akamwambia, Nifuate.

28 Akaacha vyote, akaondoka, akamfuata.

29 Na Lawi akamfanyia karamu kubwa nyumbani mwake; palikuwa na mkutano mkuu wa watoza ushuru na watu wengineo waliokuwa wameketi chakulani pamoja nao.

30 Ikawa Mafarisayo na waandishi wao kuwanung'unikia wanafunzi wake, wakisema, Mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?

31 Yesu akajibu akawaambia, Wenye afya hawana haja na tabibu, isipokuwa walio wagonjwa.

32 Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu.

33 Nao wakamwambia, Wanafunzi wa Yohana hufunga mara nyingi, na kuomba dua; na kadhalika wanafunzi wa Mafarisayo; lakini wanafunzi wako hula na kunywa!

34 Lakini Yesu akawaambia, Je! Mwaweza kuwafanya wafunge walioalikwa arusini, akiwapo bwana arusi pamoja nao?

35 Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi, ndipo watakapofunga siku zile.

36 Akawaambia na mithali, Hakuna akataye kiraka cha vazi jipya na kukitia katika vazi kuukuu; na kama akitia, amelikata lile jipya, na kile kiraka cha vazi jipya hakilingani na lile vazi kuukuu.

37 Wala hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu; na kama akitia, ile divai mpya itavipasua vile viriba, divai yenyewe itamwagika, na viriba vitaharibika.

38 Lakini divai mpya sharti kutiwa katika viriba vipya.

39 Wala hakuna anywaye divai ya kale akatamani divai mpya; kwa kuwa asema, Ile ya kale ndiyo iliyo njema.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo