Isaya 47 - Swahili Revised Union VersionKuaibishwa kwa Babeli 1 Haya, shuka, keti mavumbini, Ewe bikira, binti Babeli; Keti chini pasipo kiti cha enzi, Ewe binti wa Wakaldayo; Maana hutaitwa tena mwororo, mpenda anasa. 2 Twaa mawe ya kusagia, usage unga; Vua utaji wako, ondoa mavazi yako, Funua mguu wako, pita katika mito ya maji. 3 Uchi wako utafunuliwa, Naam, aibu yako itaonekana. Nitalipa kisasi; simkubali mtu yeyote. 4 Mkombozi wetu, BWANA wa majeshi ndilo jina lake, Mtakatifu wa Israeli. 5 Kaa kimya, ingia gizani, Ee binti wa Wakaldayo; Maana hutaitwa tena Malkia wa falme. 6 Nilikuwa nimekasirika na watu wangu, niliutia unajisi urithi wangu, nikawatia mkononi mwako; wewe hukuwatendea rehema; kwa wazee uliifanya nira yako kuwa nzito sana. 7 Ukasema, Mimi nitakuwa malkia milele; hata hukuyatia hayo moyoni mwako, wala hukukumbuka mwisho wa mambo hayo. 8 Sasa, basi, sikia haya, wewe upendaye anasa, ukaaye na kujiona salama, wewe usemaye moyoni mwako, Mimi ndiye, wala hapana mwingine zaidi yangu mimi; sitaketi kama mjane, wala sitajua kufiwa na watoto; 9 lakini mambo haya mawili yatakupata katika dakika moja siku moja, kufiwa na watoto, na ujane; yatakupata kiasi kamili, uchawi wako ujapokuwa mwingi, na uganga wako mwingi mno. 10 Maana umeutumainia ubaya wako; umesema, Hapana anionaye; hekima yako, na maarifa yako yamekupotosha, nawe umesema moyoni mwako, Mimi ndiye, wala hapana mwingine zaidi yangu mimi. 11 Kwa sababu hiyo uovu utakupata; wala hutaweza kuuagua; na msiba utakuangukia; hutaweza kuuondoa; na ukiwa usioujua utakupata kwa ghafla. 12 Simama sasa na uganga wako, na wingi wa uchawi wako, uliojitaabisha nao tangu ujana wako; labda utaweza kupata faida, labda utaweza kushinda. 13 Umechoka kwa wingi wa mashauri yako; basi, na wasimame hao wanajimu, wazitazamao nyota, watabirio kila mwezi mambo ya mwezi huo, wakakuokoe kutoka kwa mambo yatakayokupata. 14 Tazama, watakuwa kama mabua makavu; moto utawateketeza; hawatajiokoa kutoka kwa nguvu za muali wa moto; hili halitakuwa kaa la kujipasha moto, wala moto wa kuota. 15 Ndivyo yatakavyokuwa mambo hayo uliyojitaabisha nayo; wale waliofanya biashara nawe tangu ujana wako watatangatanga mbali nawe, kila mtu akienda zake; hapatakuwa na mtu wa kukuokoa. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya