Isaya 21 - Swahili Revised Union VersionUtabiri juu ya Babeli, Edomu na Arabuni 1 Ufunuo juu ya nyika kando ya bahari. Kama tufani za Negebu zikaribiavyo kwa kasi, inakuja kutoka kwa nyika, toka nchi itishayo. 2 Nimeoneshwa maono magumu; atendaye hila anatenda hila, mharibu anaharibu. Panda juu, Ee Elamu; husuru, Ee Umedi; mimi ninakomesha maombolezo yake yote. 3 Kwa sababu hiyo viuno vyangu vimejaa maumivu, uchungu umenishika, kama uchungu wa mwanamke azaaye; ninaumwa sana, nisiweze kusikia; nimefadhaishwa wa hofu, nisiweze kuona. 4 Moyo wangu unapigapiga, utisho umenitaabisha, gizagiza la jioni nilipendalo limegeuka likanitetemesha. 5 Wanaandaa meza, wanaweka ulinzi, wanakula, wanakunywa. Simameni, enyi wakuu, itieni ngao mafuta. 6 Maana Bwana ameniambia hivi, Nenda, weka mlinzi; aonayo na ayatangaze. 7 Naye akiona kundi la wapanda farasi, wakienda wawili wawili, na kundi la punda, na kundi la ngamia; na asikilize kwa makini, kwa makini sana. 8 Ndipo akalia kama simba, Ee Bwana, mimi nasimama daima juu ya mnara wakati wa mchana, na kila usiku ninakaa katika zamu ya ulinzi wangu. 9 Na, tazama, linakuja kundi la watu, wapanda farasi, wakienda wawili wawili. Akajibu na kusema, Babeli umeanguka, umeanguka; na sanamu zote za miungu yake zimevunjwa chini. 10 Ewe wangu niliyekufikicha na kukupura; Hayo niliyoyasikia kwa BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, nayatangaza kwenu. 11 Ufunuo juu ya Duma. Mtu ananililia toka Seiri, Ee mlinzi, habari gani za usiku? Ee mlinzi, habari gani za usiku? 12 Mlinzi akasema, Mchana unakuja na usiku pia; mkitaka kuuliza, ulizeni; njoni tena. 13 Ufunuo juu ya Arabuni. Ndani ya msitu wa Arabuni mtalala, Enyi misafara ya Wadedani. 14 Waleteeni wenye kiu maji, Enyi wenyeji wa nchi ya Tema; Nendeni kuwalaki wakimbiao na chakula chao. 15 Kwa maana wanakimbia mbele ya panga, Upanga uliofutwa, na upinde uliopindwa, Na mbele ya ukali wa vita. 16 Kwa sababu Bwana ameniambia hivi, Katika muda wa mwaka, kama miaka ya mtu mwenye kuajiriwa, utaangamia utukufu wote wa Kedari. 17 Na mabaki ya hesabu ya wavuta pinde, hao mashujaa wa Kedari watakuwa wachache; maana BWANA, Mungu wa Israeli, amenena neno hili. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya