Hesabu 5 - Swahili Revised Union VersionWatu najisi 1 Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, 2 Waamrishe wana wa Israeli kwamba wamtoe kila mwenye ukoma kambini, na kila mtu aliye na kisonono, na kila aliye najisi kwa ajili ya maiti; 3 mtawatoa nje wote, wanaume kwa wanawake, mtawaweka nje ya kambi; ili wasizitie unajisi kambi zao, ambazo mimi naketi katikati yazo. 4 Wana wa Israeli wakafanya hivyo, wakawatoa na kuwaweka nje ya kambi; kama BWANA alivyonena na Musa, ndivyo walivyofanya wana wa Israeli. Toba na Ukombozi 5 Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, 6 Uwaambie wana wa Israeli, Mtu mume au mke atakapofanya dhambi yoyote, ifanywayo na binadamu, kumwasi BWANA, na mtu huyo akawa na hatia; 7 ndipo watakapoungama dhambi yao waliyoifanya; naye atatoa fidia kwa hatia yake, kwa utimilifu wake, tena ataongeza juu yake sehemu ya tano, na kumpa huyo aliyemkosea. 8 Lakini ikiwa mtu huyo hana jamaa ya karibu ambaye inampasa kurudishiwa kwa ajili ya hiyo hatia, kile kitakachorudishwa kwa BWANA kwa hiyo hatia kitakuwa cha kuhani, pamoja na kondoo dume wa upatanisho, ambaye kwa huyo utafanywa upatanisho kwa ajili yake. 9 Tena kila sadaka ya kuinuliwa, ya vitu vitakatifu vya wana wa Israeli, watakavyovileta kwa kuhani, vitakuwa ni vyake. 10 Tena vitu vilivyowekwa wakfu na mtu awaye yote, vitakuwa ni vya kuhani; kitu chochote mtu atakachompa kuhani, kitakuwa chake. Kuhusu Mke asiye Mwaminifu 11 Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, 12 Nena na wana wa Israeli, uwaambie, kama mke wa mtu yeyote akikengeuka, na kumkosa mumewe, 13 na mwanamume akalala naye kwa uasherati, na jambo hilo likafichika kwa mumewe, likawa jambo lisilojulikana, na huyo mwanamke akawa najisi, wala hapana shahidi aliyeshuhudia juu yake, wala hakufumaniwa; 14 kisha mumewe akashikwa na roho ya wivu, akamwonea wivu mkewe, naye akawa najisi huyo mwanamke; au kama akiingiwa na roho ya wivu, akamwonea wivu mkewe, naye hakuwa na unajisi huyo mke; 15 ndipo huyo mume atamchukua mkewe, aende naye kwa kuhani, naye ataleta sadaka yake kwa ajili yake, yaani, sehemu ya kumi ya efa; asitie mafuta juu yake, wala asitie ubani juu yake; maana, ni sadaka ya unga ya wivu, ni sadaka ya unga ya ukumbusho ya kukumbukia uovu. 16 Basi kuhani atamleta mwanamke akaribie, na kumweka mbele za BWANA; 17 kisha kuhani atatwaa maji matakatifu katika chombo cha udongo; kisha kuhani atatwaa katika vumbi lililo pale chini ya maskani, na kulitia katika hayo maji; 18 kisha kuhani atamweka mwanamke mbele za BWANA, naye atazifungua nywele za kichwani mwa huyo mwanamke, kisha atampa hiyo sadaka ya unga ya ukumbusho mikononi mwake, ambayo ni sadaka ya unga ya wivu, naye kuhani atakuwa na hayo maji ya uchungu yaletayo laana mkononi mwake; 19 tena kuhani atamwapisha huyo mwanamke, naye atamwambia mwanamke, Kwamba hakulala mtu mume pamoja nawe, tena ikiwa hukukengeuka kutenda maovu, ukiwa chini ya mumeo, maji haya ya uchungu yaletayo laana yasikudhuru; 20 lakini ikiwa umekengeuka ukiwa chini ya mumeo, na kwamba u hali ya unajisi, na mwanamume amelala nawe, asiyekuwa mumeo; 21 hapo ndipo kuhani atamwapisha mwanamke kwa kiapo cha kuapiza, kisha kuhani atamwambia huyo mwanamke maneno haya, BWANA na akufanye wewe uwe laana na kiapo kati ya watu wako, hapo BWANA akufanyapo paja lako kupooza, na tumbo lako kuvimba; 22 na maji yaletayo laana yatakuingia matumboni mwako, na kukuvimbisha tumbo, na kukupoozesha paja lako; na mwanamke ataitika, Amina, Amina. 23 Kisha kuhani ataziandika laana hizo ndani ya kitabu, na kuzifuta katika maji ya uchungu; 24 kisha atamnywesha mwanamke hayo maji ya uchungu yaletayo laana; nayo maji yaletayo laana yataingia ndani yake, nayo yatageuka kuwa uchungu. 25 Kisha kuhani ataitwaa hiyo sadaka ya unga ya wivu, kwa kuiondoa mkononi mwa huyo mwanamke, naye ataitikisa sadaka ya unga mbele ya BWANA, na kuisongeza pale madhabahuni; 26 kisha kuhani atatwaa konzi moja ya sadaka ya unga, kuwa ni ukumbusho wake, na kuuteketeza madhabahuni, baadaye atamnywesha mwanamke hayo maji. 27 Kisha hapo atakapokwisha kumnywesha maji, ndipo itakapokuwa, kama amekuwa hali ya unajisi na kumkosea mumewe, hayo maji yaletayo laana yatamwingia ndani yake, nayo yatakuwa uchungu, na tumbo lake litavimba, na paja lake litapooza; na huyo mwanamke atakuwa laana kati ya watu wake. 28 Na kama mwanamke hakuwa na unajisi lakini yu safi; ndipo ataachiliwa, naye atazaa wana. 29 Hii ndiyo sheria ya wivu, mwanamke, ambaye yu chini ya mumewe, akikengeuka, na kupata unajisi; 30 au, roho ya wivu ikimwingia mtu mume, naye akamwonea wivu mkewe; ndipo atakapomweka huyo mwanamke mbele za BWANA, na kuhani atatenda juu yake sheria hii yote. 31 Na huyo mume atakuwa hana uovu, na mwanamke atauchukua uovu wake. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya