Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Hesabu 22 - Swahili Revised Union Version


Balaki amwita Balaamu na awalaani Waisraeli

1 Kisha wana wa Israeli wakasafiri na kupanga katika nchi tambarare za Moabu ng'ambo ya pili ya Yordani karibu na Yeriko.

2 Na Balaki mwana wa Sipori akaona mambo yote ambayo Israeli wamewatendea Waamori.

3 Moabu akawaogopa hao watu sana, kwa kuwa walikuwa wengi; Moabu akafadhaika kwa sababu ya wana wa Israeli.

4 Moabu akawaambia wazee wa Midiani, Sasa jeshi hili la watu litaramba vitu vyote vinavyotuzunguka, kama vile ng'ombe arambavyo majani ya mashamba. Na Balaki, mwana wa Sipori, alikuwa mfalme wa Moabu zamani zile.

5 Basi akatuma wajumbe kwa Balaamu mwana wa Beori, hadi Pethori, ulio kando ya Mto, mpaka nchi ya wana wa watu wake, kwenda kumwita, akisema, Tazama, kuna watu waliotoka Misri; tazama, wanaufunika uso wa nchi, tena wanakaa kunikabili mimi.

6 Basi, njoo wewe, nakusihi unilaanie watu hawa; maana wana nguvu kunishinda mimi. Labda nitawaweza, tupate kuwapiga, niwafukuze watoke katika nchi yangu, kwa maana najua ya kuwa yeye umbarikiye hubarikiwa, na yeye umlaaniye hulaaniwa.

7 Wazee wa Moabu, na wazee wa Midiani, wakaenda, wakichukua ujira wa uganga mikononi mwao; wakamfikia Balaamu, wakamwambia maneno ya Balaki.

8 Akawaambia, Kaeni hapa usiku huu, nami nitawaletea jawabu kama BWANA atakavyoniambia; wakuu wa Moabu wakakaa na Balaamu.

9 Mungu akamjia Balaamu, akasema, Ni watu gani hawa ulio nao pamoja nawe?

10 Balaamu akamwambia Mungu, Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, amewatuma kwangu, akisema,

11 Tazama, kuna watu waliotoka Misri, wanaufunika uso wa nchi; basi njoo unilaanie watu hawa; labda nitaweza kupigana nao, na kuwafukuza.

12 Mungu akamwambia Balaamu, Usiende pamoja nao; wala usiwalaani watu hawa, maana wamebarikiwa.

13 Balaamu akaondoka asubuhi akawaambia wakuu wa Balaki, Nendeni zenu hadi nchi yenu; kwa maana BWANA amekataa kunipa ruhusa niende pamoja nanyi.

14 Wakuu wakaondoka wakaenda kwa Balaki, wakasema, Balaamu, anakataa kuja pamoja nasi.

15 Basi Balaki akatuma wakuu mara ya pili, wengi zaidi, wenye cheo cha juu kuliko wale wa kwanza.

16 Wakamfikia Balaamu, wakamwambia, Balaki mwana wa Sipori asema hivi, Nakusihi, neno lolote lisikuzuie usinijie;

17 maana nitakutunukia heshima kubwa sana, na neno lolote utakaloniomba nitalitenda; basi njoo, nakusihi, unilaanie watu hawa.

18 Balaamu akajibu akawaambia watumishi wa Balaki, Hata kama Balaki angenipa nyumba yake imejaa fedha na dhahabu, siwezi kukiuka neno la BWANA, Mungu wangu, kulipunguza au kuliongeza.

19 Basi sasa nawasihi, kaeni hapa tena usiku huu, nipate kujua BWANA atakaloniambia zaidi.

20 Mungu akamjia Balaamu usiku, akamwambia, Kwa kuwa watu hawa wamekuja kukuita, nenda pamoja nao; lakini neno lile nitakalokuambia ndilo utakalolitenda, basi.

21 Balaamu akaondoka asubuhi, akatandika punda wake, akaenda pamoja na wakuu wa Moabu.


Balaamu, punda na malaika

22 Hasira ya Mungu ikawaka kwa sababu alikwenda; malaika wa BWANA akajiweka njiani, ili kumpinga. Basi alikuwa amepanda punda wake, na watumishi wake wawili walikuwa pamoja naye.

23 Na yule punda akamwona malaika wa BWANA amesimama njiani, na upanga wake mkononi mwake amekwisha kuufuta; punda akageuka upande ili kuiacha njia, akaingia shambani. Balaamu akampiga punda ili kumrejesha njiani.

24 Kisha malaika wa BWANA akasimama mahali penye bonde, katikati ya mashamba ya mizabibu, tena penye kitalu upande huu na kitalu upande huu.

25 Yule punda akamwona malaika wa BWANA, akajisukuma ukutani, akaubana mguu wake Balaamu, basi akampiga mara ya pili.

26 Malaika wa BWANA akaenda mbele akasimama mahali pembamba sana, hapakuwa na nafasi ya kugeukia mkono wa kulia, wala mkono wa kushoto.

27 Yule punda akamwona malaika wa BWANA, akajilaza chini ya Balaamu; hasira yake Balaamu ikawaka, akampiga punda kwa fimbo yake.

28 BWANA akakifunua kinywa cha yule punda, naye akamwambia Balaamu, Nimekutenda nini, hata ukanipiga mara tatu hizi?

29 Balaamu akamwambia punda; Kwa sababu umenidhihaki; laiti ningekuwa na upanga mkononi mwangu ningekuua sasa hivi.

30 Yule punda akamwambia Balaamu, Je! Mimi si punda wako, nawe umenipanda maisha yako yote hata leo? Nimezoea kukutenda hayo? Akasema, La!

31 Ndipo BWANA akafunua macho ya Balaamu akamwona malaika wa BWANA amesimama njiani, akiwa na upanga mkononi mwake, umekwisha kufutwa, naye akainamisha kichwa, akaanguka kifudifudi.

32 Malaika wa BWANA akamwambia, Mbona umempiga punda wako mara tatu hizi? Tazama mimi nimekuja ili kukupinga, kwa sababu njia yako imepotoka mbele zangu,

33 punda akaniona, akageuka upande mbele zangu mara tatu hizi; kama asingejiepusha nami, bila shaka ningalikuua wewe, nikamwacha yeye hai.

34 Balaamu akamwambia malaika wa BWANA, Nimefanya dhambi; maana sikujua ya kuwa wewe umesimama njiani ili kunipinga; basi sasa, ikiwa umechukizwa, nitarudi tena.

35 Malaika wa BWANA akamwambia Balaamu Nenda pamoja na watu hawa, lakini neno lile nitakalokuambia, ndilo utakalosema. Basi Balaamu akaenda pamoja na wakuu wa Balaki.

36 Balaki aliposikia ya kuwa Balaamu amefika, akatoka kwenda kumlaki, mpaka Mji wa Moabu, ulioko katika mpaka wa Arnoni, ulioko katika upande wa mwisho wa mpaka huo.

37 Balaki akamwambia Balaamu, Je! Mimi sikutuma watu kwako kwa bidii ili kukuita? Mbona hukunijia? Je! Siwezi mimi kukufanyizia heshima nyingi?

38 Balaamu akamwambia Balaki, Tazama, nimekujia. Je! Mimi sasa nina uwezo wowote kusema neno lolote? Neno lile Mungu atakalolitia kinywani mwangu, ndilo nitakalolisema.

39 Balaamu akaenda pamoja na Balaki wakafika Kiriath-husothi.

40 Balaki akachinja ng'ombe, na kondoo, akampelekea Balaamu na wale wakuu waliokuwa pamoja naye.


Aguzi la kwanza la Balaamu

41 Ikawa asubuhi Balaki akamchukua Balaamu, akampandisha hadi Bamoth-baali; na kutoka huko aliweza kuwaona baadhi ya Waisraeli hadi pande zao za mwisho.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo