Utaratibu wa kazi1 Ndipo akaondoka Eliashibu, kuhani mkuu, pamoja na nduguze makuhani, wakalijenga lango la kondoo; wakazitia boriti zake, wakaisimamisha milango yake; mpaka mnara wa Hamea wakalitakasa, mpaka mnara wa Hananeli. 2 Sehemu iliyofuata ilijengwa na watu wa Yeriko. Na baada yao Zakuri mwana wa Imri akajenga. 3 Na lango la samaki wakalijenga wana wa Senaa; wakazitia boriti zake, wakaisimamisha milango yake, na vyuma vyake, na makomeo yake. 4 Na baada yao akaijenga Meremothi, mwana wa Uria, mwana wa Hakosi. Na baada yao akafanyiza Meshulamu, mwana wa Berekia, mwana wa Meshezabeli. Na baada yao akafanyiza Sadoki, mwana wa Baana. 5 Na baada yao wakajenga Watekoi; lakini wakuu wao hawakutia shingo zao kazini mwa bwana wao. 6 Na lango la kale wakalijenga Yoyada, mwana wa Pasea, na Meshulamu, mwana wa Besodeya; wakazitia boriti zake, wakaisimamisha milango yake, na vyuma vyake, na makomeo yake. 7 Na baada yao wakajenga Melatia, Mgibeoni, na Yadoni, Mmeronothi, watu wa Gibeoni, na wa Mispa, waliokuwa chini ya utawala wa mtawala wa sehemu ya ng'ambo ya Mto. 8 Na baada yao akajenga Uzieli, mwana wa Harhaya, mmoja wa mafundi wa dhahabu. Na baada yake akafanyiza Hanania, mmoja wa mafundi wa manukato, nao wakaujengea Yerusalemu buruji mpaka ule ukuta mpana. 9 Na baada yao Refaya, mwana wa Huri akajenga, mtawala wa nusu ya Yerusalemu. 10 Na baada yao akajenga Yedaya, mwana wa Harumafu, kuielekea nyumba yake. Na baada yake akajenga Hatushi, mwana wa Hashabneya. 11 Malkiya, mwana wa Harimu, na Hashubu, mwana wa Pahath-moabu, wakajenga sehemu nyingine, na mnara wa tanuri. 12 Na baada yake akajenga Shalumu, mwana wa Haloheshi, mtawala wa nusu ya sehemu ya Yerusalemu, yeye na binti zake. 13 Lango la bondeni wakalijenga Hanuni, nao wakaao Zanoa; wakalijenga, wakaisimamisha milango yake, na vyuma vyake, na makomeo yake, na huo ukuta wa dhiraa elfu moja mpaka lango la jaa. 14 Na lango la jaa akalijenga Malkiya, mwana wa Rekabu, mtawala wa sehemu ya wa Beth-hakeremu; akalijenga, akaisimamisha milango yake, na vyuma vyake, na makomeo yake. 15 Na lango la chemchemi akalijenga Shalumu, mwana wa Kolhoze, mkuu wa Mispa akalitengeneza lango la Chemchemi akalijenga na kulifunika, akasimamisha milango yake, na vyuma vyake, na makomeo yake, na huo ukuu wa birika la Shiloa karibu na bustani ya mfalme, mpaka madaraja yashukayo kutoka mji wa Daudi. 16 Baada yake akajenga Nehemia, mwana wa Azbuki, mkuu wa nusu ya mtaa wa Beth-suri, mpaka mahali paelekeapo makaburi ya Daudi, na mpaka birika lililofanyizwa, na mpaka nyumba ya wapiganaji. 17 Baada yake wakajenga Walawi, Rehumu, mwana wa Bani. Baada yake akajenga Hashabia, mkuu wa nusu ya mtaa wa Keila, kwa mtaa wake. 18 Baada yake wakajenga ndugu zao, Binui, mwana wa Henadadi, mkuu wa nusu ya mtaa wa Keila. 19 Na baada yake Ezeri, mwana wa Yeshua, mkuu wa Mispa, akajenga sehemu nyingine, inayoelekeana na njia ya kupanda kwa ghala ya silaha, pembeni mwa ukuta. 20 Baada yake Baruku, mwana wa Zakai, akajenga kwa bidii sehemu nyingine, kutoka pembeni mwa ukuta mpaka mlango wa nyumba ya Eliashibu, kuhani mkuu. 21 Baada yake akajenga Meremothi, mwana wa Uria, mwana wa Hakosi, sehemu nyingine, kutoka mlangoni mwa nyumba ya Eliashibu mpaka mwisho wa nyumba ya Eliashibu. 22 Na baada yake wakafanyiza makuhani, watu wa Uwandani. 23 Baada yao wakajenga Benyamini na Hashubu, kuielekea nyumba yao. Baada yao akajenga Azaria, mwana wa Maaseya, mwana wa Anania, kando ya nyumba yake. 24 Baada yake Binui, mwana wa Henadadi, alitengeneza sehemu nyingine, kuanzia kwenye nyumba ya Azaria mpaka ugeukapo ukuu, na mpaka pembeni. 25 Baada yake akajenga Palali, mwana wa Uzai, kuelekea ugeukapo ukuta, nao mnara utokezao penye nyumba ya juu ya kifalme, iliyopo karibu na uwanda wa walinzi. Baada yake akajenga Pedaya, mwana wa Paroshi, 26 (basi Wanethini hukaa Ofeli), mpaka mahali paelekeapo lango la maji kukabili mashariki, nao mnara utokezao. 27 Baada yake wakajenga Watekoi sehemu nyingine, kuuelekea mnara mkubwa utokezao, na mpaka ukuta wa Ofeli. 28 Juu ya lango la farasi wakajenga makuhani, kila mtu kuielekea nyumba yake. Baada yao akajenga Sadoki, mwana wa Imeri, kuielekea nyumba yake. 29 Na baada yake akajenga Shemaya, mwana wa Shekania, mlinzi wa lango la mashariki. 30 Baada yake wakajenga Hanania, mwana wa Shelemia, na Hanuni, mwana wa sita wa Salafu, sehemu nyingine. Baada yake akafanyiza Meshulamu, mwana wa Berekia, sehemu nyingine kuelekea chumba chake. 31 Baada yake akajenga Malkiya, mmoja wa mafundi wa dhahabu, mpaka nyumba ya Wanethini, na ya wafanya biashara, kulielekea lango la gereza, na mpaka chumba cha juu cha pembeni. 32 Na kati ya chumba cha juu cha pembeni na lango la kondoo wakajenga mafundi wa dhahabu na wafanya biashara. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya