Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Yoshua 18 - Swahili Revised Union Version


Nchi ya makabila yaliyobaki

1 Kisha mkutano mzima wa wana wa Israeli walikutana pamoja hapo Shilo, wakasimamisha hema ya kukutania huko; nayo nchi ilikuwa imeshindwa mbele zao.

2 Yalikuwa yamebaki kati yao makabila saba ya wana wa Israeli ambayo yalikuwa hayajagawiwa urithi wao.

3 Yoshua akawauliza wana wa Israeli, akasema, Je! Hata lini mtakuwa walegevu katika kuingia kwenu na kuimiliki hiyo nchi, ambayo yeye BWANA, Mungu wa baba zenu, amewapa?

4 Haya, jichagulieni watu watatu kwa ajili ya kila kabila; nami nitawatuma, nao watainuka waende kati ya hiyo nchi, na kuiandika kama urithi wao ulivyo; kisha watanijia.

5 Watu hao wataigawanya nchi iwe mafungu saba; Yuda atakaa katika mpaka wake huko upande wa kusini, na nyumba ya Yusufu watakaa katika mpaka wao upande wa kaskazini.

6 Nanyi mtaiandika nchi iwe mafungu saba, kisha hayo maandiko yake mtaniletea mimi hapa; nami nitawapigia kura hapa mbele ya BWANA, Mungu wetu.

7 Kwa maana Walawi hawana fungu kati yenu; Kwa kuwa huo ukuhani wa BWANA ndio urithi wao; tena Gadi, na Reubeni, na hiyo nusu ya kabila la Manase, wamekwisha pata urithi wao ng'ambo ya pili ya Yordani upande wa mashariki, ambao walipewa na Musa, mtumishi wa BWANA.

8 Basi watu hao wakainuka wakaenda; Yoshua aliwaagiza wale waliokwenda kuichunguza nchi, akawaambia, Nendeni, mkapite katikati ya nchi, na kuandika habari zake, kisha mnijie tena hapa, nami nitawapigia kura kwa ajili yenu hapo mbele za BWANA huko Shilo.

9 Basi watu hao wakaenda, wakapita katikati ya nchi, wakaandika habari zake katika kitabu, na kuigawanya kwa miji yake, hata iwe mafungu saba, kisha wakamrejea Yoshua kambini huko Shilo.

10 Kisha Yoshua akapiga kura kwa ajili yao hapo mbele za BWANA katika Shilo; huko Yoshua akawagawanyia wana wa Israeli hiyo nchi sawasawa na mafungu yao.


Nchi ya Benyamini

11 Kisha ilizuka kura ya kabila la wana wa Benyamini kwa kulingana na jamaa zao; na mpaka wa hiyo kura yao ukatokea kati ya wana wa Yuda na wana wa Yusufu.

12 Mpaka wao upande wa kaskazini ulikuwa kutoka mto wa Yordani; kisha mpaka ukaendelea kufikia ubavuni mwa mji wa Yeriko upande wa kaskazini, kisha ukaendelea kati ya nchi ya vilima kwa kuelekea upande wa magharibi; na matokeo yake yalikuwa hapo penye nyika ya Beth-aveni.

13 Kisha mpaka ukaendelea kutoka hapo na kufikia mji wa Luzu, ubavuni mwa Luzu (ndio Betheli), kwa upande wa kusini; kisha mpaka ukateremkia Ataroth-adari, karibu na mlima ulio upande wa kusini wa Beth-horoni wa chini.

14 Kisha mpaka uliendelea na kuzunguka upande wa magharibi wa kuelekea kusini, kutoka huo mlima ulio mkabala wa Beth-horoni upande wa kusini; na mwisho wake ulikuwa hapo Kiriath-baali (ndio Kiriath-yearimu), ni mji wa wana wa Yuda; huo ndio upande wa magharibi.

15 Na upande wa kusini ulikuwa ukitoka upande wa mwisho wa Kiriath-yearimu, na mpaka ukatokea upande wa magharibi, ukaendelea hadi chemchemi ya maji, pale Neftoa;

16 kisha mpaka uliteremka hadi mwisho wa mlima ulio pale mkabala wa bonde la mwana wa Hinomu, lililo pale katika bonde la Warefai, upande wa kaskazini; nao ukateremkia mpaka bonde la Hinomu, hadi ubavuni mwa Myebusi upande wa kusini, kisha ukateremka hadi Enrogeli,

17 kisha ulipinda upande wa kaskazini, nao ukatokea hapo Enshemeshi, ukatokea hadi kufikia Gelilothi, ambao ni mkabala wa makweleo ya Adumimu; kisha uliteremka hadi jiwe la Bohani mwana wa Reubeni;

18 kisha ukaendelea mbele ubavuni kuikabili Araba, upande wa kuelekea kaskazini, nao ukateremka hadi hiyo Araba;

19 kisha mpaka ukaendelea mbele ubavuni mwa Beth-hogla upande wa kaskazini; na mwisho wa mpaka ulikuwa katika ile hori ya kaskazini ya Bahari ya Chumvi, mwisho wa kusini wa mto wa Yordani; huo ndio mpaka wa upande wa kusini.

20 Na mto wa Yordani ulikuwa ndio mpaka wake upande wa mashariki. Huo ndio urithi wa wana wa Benyamini, kwa kufuata mipaka yake kwa kuuzunguka kotekote, kulingana na jamaa zao.

21 Basi miji ya kabila la wana wa Benyamini kwa kufuata jamaa zao ilikuwa ni Yeriko, na Beth-hogla, na Emek-kesisi,

22 na Bethiaraba, na Semaraimu, na Betheli;

23 na Avimu, na Para, na Ofra;

24 na Kefar-amoni, na Ofni, na Geba; miji kumi na miwili, pamoja na vijiji vyake;

25 na Gibeoni, na Rama, na Beerothi;

26 na Mispa, na Kefira, na Moza;

27 na Rekemu, na Irpeeli, na Tarala;

28 na Zela, na Elefu, na huyo Myebusi (ndio Yerusalemu), na Gibeathi, na Kiriathi; miji kumi na minne, pamoja na vijiji vyake. Huo ndio urithi wa wana wa Benyamini kwa kufuata jamaa zao.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo