Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Mwanzo 29 - Swahili Revised Union Version


Yakobo akutana na Raheli

1 Kisha Yakobo akashika njia yake, akafika nchi ya wana wa mashariki.

2 Naye akaangalia, na tazama, kiko kisima kondeni, na makundi matatu ya kondoo yamelala karibu nacho, kwa sababu katika kisima kile hunywesha makundi; na palikuwa na jiwe kubwa juu ya kinywa cha kisima.

3 Makundi yote hukusanyika huko, watu wakabingirisha hilo jiwe katika kinywa cha kisima wakawanywesha kondoo, na kulirudisha jiwe juu ya kinywa cha kisima mahali pake.

4 Yakobo akawauliza, Ndugu zangu, ninyi ni watu wa wapi? Wakasema, Sisi tu wa Harani.

5 Akawauliza, Je! Mnamjua Labani, mwana wa Nahori? Wakasema, Tunamjua.

6 Akawauliza, Je! Hajambo? Wakasema, Hajambo; tazama, Raheli binti yake anakuja na kondoo.

7 Akasema, Tazama, kungali mchana bado, wala sio wakati wa kukusanya wanyama; wanywesheni kondoo, mwende kuwalisha.

8 Wakasema, Hatuwezi, Mpaka makundi yote yakusanyike, watu wakabingirishe jiwe katika kinywa cha kisima, ndipo tunapowanywesha kondoo.

9 Na alipokuwa akisema nao, Raheli akaja na kondoo wa baba yake, maana aliwachunga.

10 Ikawa Yakobo alipomwona Raheli binti Labani, ndugu wa mamaye, na kondoo wa Labani, ndugu wa mamaye, Yakobo akakaribia, na kulibingirisha lile jiwe litoke katika kinywa cha kisima, akawanywesha kondoo wa Labani, ndugu wa mamaye.

11 Yakobo akambusu Raheli, akalia kwa sauti.

12 Yakobo akamwarifu Raheli ya kuwa yeye ni ndugu wa babaye, na ya kuwa ni mwana wa Rebeka. Basi akapiga mbio akampasha babaye habari.

13 Ikawa Labani aliposikia habari za Yakobo, mwana wa nduguye, akaenda mbio amlaki, akamkumbatia, akambusu, akamleta nyumbani kwake. Naye akamwambia Labani maneno hayo yote.

14 Labani akamwambia, Ndiwe kweli mfupa wangu na nyama yangu. Naye akakaa kwake muda wa mwezi mmoja.


Yakobo awaoa mabinti wa Labani

15 Labani akamwambia Yakobo, Kwa sababu wewe ni jamaa yangu, basi, je! Unitumikie bure? Niambie mshahara wako utakuwa nini?

16 Labani alikuwa na binti wawili, jina la mkubwa ni Lea, na jina la mdogo ni Raheli.

17 Naye Lea macho yake yalikuwa malegevu, lakini Raheli alikuwa mzuri wa umbo, na mzuri wa uso.

18 Yakobo akampenda Raheli akasema, Nitakutumikia miaka saba kwa kumpata Raheli, binti yako mdogo.

19 Labani akasema, Afadhali nikupe wewe kuliko mtu mwingine; kaa kwangu.

20 Yakobo akatumika miaka saba kwa kumpata Raheli. Ikawa machoni pake kama siku chache tu kwa vile alivyompenda.

21 Yakobo akamwambia Labani, Nipe mke wangu, maana siku zangu zimetimia; niingie kwake.

22 Labani akakusanya watu wote wa mahali pale, akafanya karamu.

23 Ikawa wakati wa jioni akamtwaa Lea, binti yake, akamletea Yakobo, naye akaingia kwake.

24 Labani akampa Lea mjakazi wake Zilpa, awe mjakazi wake.

25 Ikawa, kulipokuwa asubuhi, kumbe! Ni Lea. Akamwambia Labani, Nini hii uliyonitenda?

26 Sikukutumikia kwa Raheli? Mbona umenidanganya? Labani akasema, Havitendeki hivi kwetu, kumtoa mdogo kabla ya mkubwa;

27 timiza siku zake saba, nasi tutakupa huyu naye kwa utumishi utakaonitumikia, miaka saba mingine.

28 Yakobo akafanya hivi, akatimiza siku zake saba. Naye Labani akampa Raheli, binti yake, kuwa mkewe.

29 Labani akampa binti yake Raheli mjakazi wake Bilha, awe mjakazi wake.

30 Ndipo Yakobo akaingia kwa Raheli, akampenda Raheli kuliko Lea, akatumika kwa ajili yake miaka saba mingine.

31 BWANA akaona ya kwamba Lea hakupendwa, naye akafungua tumbo lake; bali Raheli alikuwa hazai.

32 Lea akapata mimba akazaa mwana, akampa jina lake, Reubeni, maana alisema, Kwa kuwa BWANA ameona mateso yangu; sasa mume wangu atanipenda.

33 Akapata mimba tena akazaa mwana, akasema, Kwa kuwa BWANA amesikia ya kwamba mimi sikupendwa, amenipa na huyu; akamwita jina lake Simeoni.

34 Akapata mimba tena, akazaa mwana, akasema, Basi wakati huu mume wangu ataungana nami, kwa sababu nimemzalia wana watatu. Kwa hiyo akamwita jina lake Lawi.

35 Akapata mimba tena, akazaa mwana. Akasema, Mara hii nitamsifu BWANA; kwa hiyo akamwita jina lake Yuda; akaacha kuzaa.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo