Hosea 7 - Swahili Revised Union Version1 Wakati nitakapo kumponya Israeli, ndipo yafunuliwapo maovu ya Efraimu, na ubaya wa Samaria; maana wanatenda uongo, na mwizi huvunja nyumba za watu, na kundi la magaidi hushambulia nje. 2 Wala hawafikiri mioyoni mwao ya kwamba naukumbuka uovu wao wote; sasa matendo yao wenyewe yamewazunguka pande zote; yako mbele za uso wangu. 3 Humfurahisha mfalme kwa uovu wao, na wakuu wao kwa uongo wao. 4 Hao wote ni wazinzi; wamekuwa kama tanuri iliyotiwa moto na mwokaji; asiyehitajika kuuchochea moto, tangu kuukanda unga hadi utakapokwisha kutiwa chachu. 5 Sikukuu ya mfalme wetu, wakuu waliugua kwa ukali wa divai; alinyosha mkono wake pamoja na wenye mzaha. 6 Maana wamefanya moyo wao kuwa tayari kama tanuri, wakati waoteapo; hasira yao hulala usiku kucha; asubuhi yawaka kama moto utoao miali. 7 Wote wamepata moto kama tanuri, nao hula watawala wao; wafalme wao wote wameanguka; hakuna hata mmoja wao aniitaye mimi. 8 Efraimu ajichanganya na mataifa; Efraimu ni mkate usiogeuzwa. 9 Wageni wamekula nguvu zake, naye hana habari; naam, nywele za mvi zimeonekana huku na huko juu yake, naye hana habari. 10 Na kiburi cha Israeli chamshuhudia mbele ya uso wake; ila hata hivyo hawakumrudia BWANA, Mungu wao, wala hawakumtafuta kwa ajili ya hayo yote. Tegemeo batili kutoka kwa mataifa 11 Naye Efraimu amekuwa kama njiwa mpumbavu, asiye na fahamu; humwita Misri, huenda Ashuru. 12 Watakapokwenda nitatandika wavu wangu juu yao; nitawashusha kama ndege wa angani; nitawarudi, kama vile mkutano wao ulivyosikia. 13 Ole wao! Kwa kuwa wamenikimbia; uharibifu na uwapate! Kwa kuwa wameniasi; ingawa ninataka kuwakomboa, hata hivyo wamenena uongo juu yangu. 14 Wala hawakunililia kwa moyo, lakini wanalalamika vitandani mwao; hujikutanisha ili kupata nafaka na divai; huniasi mimi. 15 Ingawa nimewafundisha na kuwatia nguvu mikono yao, hata hivyo hukusudia udhalimu juu yangu. 16 Wao hurudi, lakini si kwake Aliye Juu; wamekuwa kama upinde usiotumainika; wakuu wao wataanguka kwa upanga, kwa sababu ya ujeuri wa ndimi zao; na kwa sababu hiyo watachekwa katika nchi ya Misri. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya